MAMBO 7 YA KUFANYA IKIWA MAFANIKIO
YAKO YAMEFUNGWA NA NGUVU ZA GIZA.
Kuna njia
nyingi za kukwambia kuwa mafanikio yako yamefungwa na nguvu za giza. Njia
mojawapo ni Roho Mtakatifu kukupa mafunuo ya kiini cha kutokufanikiwa kwako
kimaisha. Anaweza kukuambia kwa njia kama ya ndoto, maono, huzuni au kukosa
amani. Siyo wengi wanajua kutumia huzuni au kukosa amani kama sauti ya Roho
Mtakatifu juu ya maisha yao [angalia maandiko yanasemaje]. Pia Mungu hutuma
neno lililobeba sauti itayokuambia itakayokuambia chanzo ni nini ili upone
(Zaburi 107:20). Lakini unahitaji uwe na masikio ya kusikia ili uweze kusikia
sauti hiyo. Wengi huwa wanashindwa kuisikia hii sauti.
1. KUMPA BWANA YESU MAISHA YAKO
Hiki ni
kipengele muhimu sana kwa mtu anayetaka kutembea kuishi sawa na kusudi la
Mungu. Kuokoka ni kumpokea Yesu kama Bwana na Mwokozi wa maisha yako. Pia
mwamini Yesu kama Mfalme wa wafalme (Ufunuo 19:16). Unapookoka, ya kale
yanapita na unakua kiumbe kipya (2 Warorintho 5:17). Ukiokoka Mungu
anayatupilia mbali maovu yako yote (Mika 7:19) na hakumbuki tena dhambi zako
(Isaya 43:25).
Lakini mtu
kama hajaokoka Roho wa Mungu anakuwa hayupo ndani yake na kibiblia mtu huyo
anakuwa amekufa (Yakobo 2:26). Biblia inazumgumzia juu ya kufufuliwa pamoja na
Kristo (Waefeso 2:6). Huwezi kufufuliwa kama hujafa. Maandiko yanasema “Mauti
na Kuzimu zikatupwa katika lile ziwa la moto. Hii ndiyo mauti ya pili, yaani
hilo ziwa la moto. Na iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu
cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto” (Ufunuo 20:14—15). Je mauti ya
kwanza ni ipi?
Nimekuonesha
mistari hiyo makusudi kwani mtu kama hajaokoka kuna vitu Mungu hawezi kukupa
katika maisha yao. Lakini ukiwa na Yesu unakuwa mtoto wa Mungu na Roho
Mtakatifu anashuhudia pamoja na roho yako (Warumi 8:16). Unapokuwa mtoto wa Mungu, unaingizwa kwenye
agano na Mungu lenye muhuri wa Roho Mtakatifu na unapewa kurithi pamoja na
Kristo katika ulimwengu wa roho. Yesu anakutoa kutoka katika ufalme wa giza
kwenda ufalme wa Mwana wa pendo lake (Wakolosai 1:13).
Unapokuwa
ndani ya agano hili, baraka zote za rohoni unapewa (Waefeso 1:3). Lakini
kumbuka kupewa baraka na kutembea ndani ya baraka ni vitu viwili tofauti. Siyo
kila aliyepewa baraka anazifaidi. Yakobo alikuwa ndani ya baraka za agano
lakini Yusufu akaondoka nazo kwenda Misri. Mungu akabariki nyumba ya akida kule
Misri badala ya Yakobo aliyeko ndani ya agano. Kuna baraka za kiagano katika
Kristo Yesu ambazo huwezi kuzipata mpaka uwe mtoto wa Mungu. Ukiwa mtoto wa
Mungu, Roho Mtakatifu anaingia ndani yako na kukufunulia maandiko (Yohana
14:26). Na Roho huyu anakupa macho ya kuona chimbuko la kutokufanikiwa kwako
kimaisha.
2. FAHAMU WAPI UMEFUNGWA
Huwezi
kujifungua kutoka kwenye kifungo ambacho hukijui. Na huwezi kujua
kilichokufunga kama huijui sheria iliyokufunga katika ulimwengu wa roho. Na
huwezi kujifungua kama hujui sheria inayoweza kuitangua ile sheria iliyokufunga
katika ulimwengu wa roho. Na huwezi kujifungua kama hujui kipengele au
vipengele vilivyoko katika ile sheria ambayo shetani ametumia kufunga mafanikio
yako. Lakini je, utaijuaje sheria iliyokufunga?
Ili uweze
kuijua sheria hii, lazima uwe na neno la Kristo. Kumbuka “imani chanzo chake ni
kusikia. Na kusikia huja kwa neno la Kristo” (Warumi 10:17). Sauti ya Neno la
Kristo ndiyo inakupa mafunuo ya kujua eneo au maeneo ambayo umefungwa katika
ulimwengu wa roho. Kama huna neno, Mungu anaweza kukuambia kifungo chako kilipo
lakini usielewe au usisikie wakati anasema nawe. Hivyo ili uweze kukijua
kifungo chako kilipo, lazima uwe na maarifa ya neno la Kristo.
3. TOBA
Ukishajua
vifungo vyako vilipo, fanya toba thabiti itayokufungua kutoka kwenye vifungo
hivyo. Kushindwa kufanya toba kunaweza kukufanya uendelee kuishi katika kifungo
hicho. Lakini je ni toba ipi ambayo unatakiwa uifanye katika kifungo fulani?
Utajuaje kama Mungu amekubali toba yako? Ukisoma habari za wana wa Israel
walipoabudu miungu mingine utaona kuwa ilimgarimu Musa toba za 4. Pia soma
habari za Gidion katika kitabu cha Waamuzi. Wakati mwingine inakulazimu ufunge
na kuomba ili uweze kufunguliwa (Matayo 17:21). Je utajuaje toba ambayo lazima
ufunge na kuomba?
Kumbuka Damu
ya Yesu inanena mema (Waebrania12:24). [Waebrania 9:11—27 inaeleza zaidi juu ya
damu ya Yesu]. Damu ya Yesu ni damu pekee inayofuta maagano pamoja na sahihi za
mashahidi wa kipepo katika ulimwengu wa roho. Damu ya Yesu ikishafuta [toba
yako imepokelewa], shetani anakosa uhalali wa kushikiria mafanikio yako. Lakini
hii haina maana huwezi kufungwa tena maeneo mengine. Kumbuka toba inakurudisha
tena kwa Mungu. “Nao watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao” (Yeremia
32:38).
4. RUDISHA MAFANIKIO YAKO
Toba yako
ikishakubaliwa mbele za Mungu, milango ya mafanikio yako inafunguliwa tena.
Unaweza kurudishiwa mafanikio yote ambayo shetani alikuwa ameyafunga katika
maisha yako. “Nami nitawaruishia hiyo miaka iliyoliwa na nzige” (Yoeli 2:25).
Lakini je
utawezaje kurudisha mafanikio yako? Napoongelea “mafanikio” siongelei kupata
hera, kupata kazi fulani, au kuwa na elimu fulani. Nazungumzia kutenda kusudi
katika maisha yako ili kuujenga ufalme wa mbinguni. Hivyo unatakiwa kuomba
Mungu ili akufunulie nini kusudi la maisha yako. Haya ni maombi muhimu kwa kila
aaminie. Lakini je unaombaje ili ujue kusudi lako katika maisha yako? Utajuaje
kama maono uliyonayo ni maono ya Mungu au maono yako?
Kumbuka
unapokuwa unaomba, siyo kila sauti utayoisikia inatoka kwa Mungu. Wakati
mwingine unapoenda kuomba na shetani naye anakuwepo. “Ilikuwa siku moja ambayo
hao wana wa Mungu walikwenda kujihudhurisha mbele za BWANA, Shetani naye
akaenda kati yao” (Ayubu 1:6). Shetani anaweza akafanya usisikie maono Mungu
anakuambia juu ya maisha yako. Badala yake ukaisikia sauti ya shetani ukidhani
ni sauti ya Mungu. Kama sauti siyo ya Mungu, utakosa amani katika moyo wako kwa
njia ya utofauti. Ndo maana ni muhimu sana kila unapokosa amani kujua sababu.
Lakini ukiwa
na neno, Mungu atakuelekeza wapi pana mafanikio aliyokukusudia na utaisikia
sauti yake. Kumbuka mafanikio yako hayategemi maono uliyo nayo na wala
hayategemei maono ya mtu mwingine juu yako. Mafanikio yako yanategemea maono ya
Mungu katika maisha yako. JE UNAYAJUA MAONO YA MUNGU KATIKA MAISHA YAKO?
[Hakikisha jibu la swali hili ni ndio]. Mungu alimwambia Isaka asiende Misri na
kuwa atambariki mahali alipo (Mwanzo 26:2—3). Wengi wanadhani mikoa au maeneo
fulani ndo kuna mafanikio. Muulize kwanza Mungu kwani unaweza kwenda Misri na
kuacha baraka zako ulipotoka.
5. FUNGA MLANGO WA ADUI ASIKUVAMIE
TENA
Ukisharudisha
mafanikio yako, hakikisha unafunga milango yote ya adui katika ulimwengu wa
roho ili nzige wasirudi kula ghala yako. Unafunga mlango wa adui na kumkabidhi
BWANA awe mmiliki wa kila ulichonacho. Ukimpa Yesu amiliki kila kitu, adui
hawezi kukushinda. Mungu atawatupilia nje adui zako wote (Sefania 3:15).
Kushindwa
kufunga mlango wa adui kunaweza kukusababishia kukwama tena kimaisha na kuwa na
hali mbaya zaidi ya ile ya mwanzo. Hujawahi kuona mtu anafilisika halafu baadae
anafanikiwa kimaisha. Halafu baada ya muda anafilisika tena na anakuwa na hali
mbaya zaidi ya mwanzo. Unadhani tatizo linaweza kuwa nini? Moja ya sababu
inaweza kuwa kushindwa kufunga mlango wa adui. Je unafungaje mlango wa adui
katika ulimwengu wa roho na adui asiweze kuufungua tena?
6. TENDA MAPENZI YA MUNGU
Ni muhimu
sana kuishi maisha ya kumpendeza Mungu ili kuhakikisha kuwa hurudi kwenye hali
yako ya kutofanikiwa. Kuishi katika dhambi kunaweza kukusababisha ukwame tena
kimaisha hata kama ulikuwa tayari umeshanguliwa. Yesu baada ya kumponya yule
mtu aliyekuwa hawezi kwa miaka 38 (Yohana 5:5—9) alimwam
bia:
“usitende dhambi tena, lisije likakupata jambo lililo baya zaidi” (Yohana 5:14).
Unapofunguliwa
kutoka kwenye vifungo vya giza, kuendelea kuishi maisha ya dhambi kunaweza
kukurudishia mapepo wabaya zaidi ili wakukwamishe kimaisha zaidi ya mwanzo.
“Pepo mchafu, amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo maji akitafuta mahali pa kupumzika, asipate. Halafu husema,
Nitarudi nyumbani kwangu nilikotoka; hata akija aiona tupu, imefagiliwa, na
kupambwa. Mara huenda, akawachukua pamoja naye pepo wengine saba walio waovu
kuliko yeye mwenyewe, nao huingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho
huwa mbaya kuliko ya kwanza” (Matayo 12:43—45). Kwa nini huyu pepo awalete pepo
7? Kumbuka 7 na namba ya utimilifu katika ulimwengu wa roho hivyo unaweza
kuelewa kitachotokea.
Hivyo dhambi
ni ufunguo shetani anautumia ili kuharibu zaidi mafanikio yako. “Kwa maana wale
waliokwisha kuyakimbia machafu ya dunia kwa kumjua Bwana na Mwokozi Yesu
Kristo, kama wakinaswa tena na kushindwa, hali yao ya mwisho imekuwa mbaya
kuliko ile ya kwanza” (2 Peter 2:20).
7. MZALIE MUNGU MATUNDA
Mungu
akikurudishia mafanikio yako na ukayatenda mapenzi yake, lazima utamzalia
matunda. Mungu anatutambua kwa matunda yetu (Mayato 7:16). Ukiona bado
unashindwa kumzalia Mungu matunda, yamkini bado unaishi nje ya kusudi la Mungu.
Kipimo cha mafanikio yako kipo kwenye mavuno siyo kwenye mbegu wala kwenye eneo
unalopanda. Kiasi cha mavuno uvunayo hakitegemei kiasi cha mbegu uliyopanda;
wala hakitegemei kile unachotegemea kuvuna. “Mmepanda mbegu nyingi, lakini
mkavuna kidogo; mnakula lakini hamshibi… Mlitazamia vingi, kumbe vikatokea
vichache” (Haggai 1:6,9). Hivyo matunda yako yawe kipimo kujua kama unatembea
katika nafasi Mungu aliyokupa katika ulimwengu wa roho ili kuujenga ufalme wa
mbinguni.
Je utajuaje
kama unaishi chini ya kiwango Mungu amekukusudia? Na ukijua unaishi chini ya
kiwango Mungu amekukusudia unafanya maombi gani ili uweze kuishi sawa na kusudi
la Mungu?
Ubarikiwe
Sana Sana!.
0 Comments