FANYA HAYA ILI UCHUMI WAKO UWE SAWA.
Mambo Matatu ambayo, kwa Mkristo ni lazima uyarekebishe
ili uchumi wako uimarike vizuri.
1. KUWA MWAMINIFU KWA MUNGU WAKO.
Dawa ya kwanza ya mafanikio yoyote yale, yawe ya kimwili
au kiroho, ni kuwa MWAMINIFU KWA BWANA.
Mithali 3:7
“ Usiwe mwenye hekima machoni pako;
Mche BWANA, ukajiepushe na uovu.
8 Itakuwa afya mwilini pako,
Na mafuta mifupani mwako.
Kumcha Bwana ni kuishi maisha matakatifu na
yanayompendeza yeye, ambayo Nuru yako inakuwa inaangaza kila mahali.
Jambo moja kubwa wakristo wengi wasilolijua ni kwamba,
tumewekwa ulimwenguni ili tuhubiri injili, licha ya kwamba Mungu anataka sisi
tupate faida katika mambo yetu kutoka kwake, lakini pia Mbingu inategemea
kupata faida kutoka kwetu.. Na faida yenyewe ni sisi kuwavuta wengine waingie
katika ufalme.
Kwahiyo maana yake ni kwamba kama wewe unafanya biashara,
au kazi yoyote ya kuajiriwa au kujiajiri.. Mungu anategemea maisha yako yawe
sababu ya kuwavuta wengine.
Hivyo Bwana akikuamini, atakuvutia watu wengi kwako, kama
ni wateja au watu wa fursa wakujie, lengo si tu waje kununua bidhaa zako, au
kukupa wewe fursa, bali Mungu anawasogeza kwako ili wapate kuiona nuru yako na
wamgeukie Mungu na kutubu..Hivyo wewe unafanyika daraja la wao kumfikia Mungu
zaidi.
Lakini kama wewe maisha yako hayana ushuhuda wowote,maana
yake ni maisha ya uzinzi, ya wizi, ya ulevi, utukanaji, umbea, usengenyaji n.k.
maana yake Mungu akikuletea watu, ni sawa na kampelekea
shetani kondoo..Hivyo ili awalinde watu wake wasizidi kupotea, anazuia wateja
wasije kwako, kwasababu utawaharibu kwa tabia zako..na Mungu hapendi watu wake
wapotee.
Atawazuia wasije kwako, na atawapeleka kwa watu wengine
wenye staha zaidi..Huku nyuma wewe utabaki kufikiri umelogwa, kumbe ni wewe
mwenyewe umejiharibu kwa kutokuwa mwaminifu kwa Mungu wako.
Mathayo 5:14
“Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa
juu ya mlima.
15 Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi,
bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani.
16 Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate
kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni”. Angaza Nuru
yako ili milango ifunguke.
2. KUWA MWAMINIFU KATIKA KAZI UNAYOIFANYA.
Hili ni jambo la pili ambalo, ni muhimu kulijua.
Wengi wetu hatujui kuwa Mungu si Mungu wa kuwadhuru watu,
bali wa kuwapatia watu mema.. Mteja yeyote Mungu anayemleta kwako, ni kwasababu
Mungu anataka apate huduma bora ya viwango, ili aweze kumshukuru Mungu baada ya
hapo, na Mungu apokee shukrani zake..
lakini hawezi kumleta kwako wewe unayeuza kitu
kilichoisha muda wake wa matumizi (kime-expire). Hapo Mungu atakuwa muuaji na
mkatili na si Mungu mwenye fadhili..
Mathayo 7:9
“9 Au kuna mtu yupi kwenu, ambaye, mwanawe akimwomba
mkate, atampa jiwe?
10 Au akiomba samaki, atampa nyoka?
11 Basi ikiwa ninyi, mlio waovu, mnajua kuwapa watoto
wenu vipawa vyema, je! Si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa mema wao
wamwombao?”
Hiyo ndio maana watu wateja hawawezi kuja kwako,
kwasababu Mungu hawezi kuwaongoza watoto wake kwenda kula sumu, au vitu vilivyo
chini ya ubora..vinginevyo atakuwa mwongo hapo aliposema.. “Basi ikiwa ninyi,
mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Si zaidi sana Baba yenu
aliye mbinguni atawapa mema wao wamwombao?”.
Hebu tengeneza picha wewe umeamka asubuhi, na kumwomba
Baba akulinde na yule mwovu na pia akupe riziki njema..halafu unatoka hapo
Mungu anakuongoza kwenda kununua Soda iliyo-expire! Kwenye duka la mtu
fulani…huyoo Mungu si atakuwa mkatili sana?..
Hivyo ili Mungu kumpa mtoto wake kipawa chema sawasawa na
Neno lake hilo, atamwepusha kuja kwenye duka lako, au kukupa wewe ajira..badala
yake anampeleka kwenye duka lingine au kumpa mtu mwingine ajira ambaye atatoa
huduma iliyo bora na kuleta faida katika ufalme wa mbinguni.
Hiyo ndio sababu wakristo wengi Mungu anaifunga milango
ya riziki katika biashara zao, au katika mambo yao mengine na kuishia kudhani
wamelogwa, na kuzunguka huku na huko kutafuta maombezi kumbe ni kwasababu wao
wenyewe sio waaminifu katika kazi zao na hawatoi huduma iliyo bora!.
Na vile vile kuwa mwaminifu katika kumtolea Mungu,
maandiko yanasema wote wasiomtolea Mungu zaka ni wezi, wanamwibia Mungu..hivyo
Mungu hawezi kuwabariki wezi.
Malaki 3:8 “Je! Mwanadamu atamwibia Mungu? Lakini ninyi
mnaniibia mimi. Lakini ninyi mwasema, Tumekuibia kwa namna gani? Mmeniibia zaka
na dhabihu. 9 Ninyi mmelaaniwa kwa laana; maana mnaniibia mimi, naam, taifa
hili lote”
Mithali 3:9 “Mheshimu BWANA kwa mali yako,Na kwa
malimbuko ya mazao yako yote. 10 Ndipo ghala zako zitakapojazwa kwa wingi, Na
mashinikizo yako yatafurika divai mpya”.
3. IMARISHA KAZI YAKO, AU UJUZI WAKO.
Hili ni jambo lingine pia la muhimu kujua.
Wengi wetu hatupendi kuziimarisha kazi zetu, au ni
walegevu katika kuziimarisha, wakati mwingine tukidhani si mpango wa Mungu.
Lakini leo nataka nikuambie kuwa kuiimarisha kazi yako,
ni jambo la muhimu sana na la kimaandiko.
Kila siku buni na tafuta mbinu mpya na ongeza ujuzi
katika shughuli unayojishughulisha nayo au unayoifanya..hayo ni mapenzi ya
Mungu pia!
Bwana Mungu baada ya kuimaliza kazi yake ya uumbaji pale
Edeni, alipumzika, lakini baada ya kipindi fulani alinyanyuka tena na
kusema..”Si vyema mtu huyu awe peke yake nitamfanyizia msaidizi wa kufanana
naye”.Ndipo akamletea Hawa kama msaidizi.
Kadhalika na sisi hatuna budi kusema siku zote “si vyema
kazi hii ikabaki yenyewe, basi niongeze nyingine kama hii, na nyingine na
nyingine”.
Si vyema kazi hii iwe kama ilivyokuwepo mwaka jana, basi
nitaiimarisha hivi na hivi..si vyema ujuzi huu nilionao nikaendelea nao, basi
nitauongeza tena na tena..
Kwa kufanya hivyo, Bwana atakubariki kwasababu na yeye
pia anafanya matengenez kila siku katika maisha yetu.
Haya ndiyo mambo makuu matatu yanayozuia uchumi wetu
kusonga mbele.
Na yaliyo ya muhimu zadi ni hayo mawili ya kwanza.
Tofauti na wengi wanaofikiri kwamba matatizo mengi
yanasababishwa na uchawi.
Uchawi wa kwanza shetani anaologa nao mtu sio kuifanya
biashara yake isifanikiwe..anachokifanya cha kwanza, na tena anakifanya kwa
bidii ni kumfanya MTU AWE MTENDA DHAMBI!.
Kwasababu anajua Dhambi ndio mzizi na chanzo chaatatizo
yote na shida na dhiki.
Mtu aliyejitenga na dhambi kamwe shetani hamwezi, na wala
hakuna uchawi mwingine wowote utakaoweza kufanya kazi juu yake.
Lakini kama mtu hajajitenga na dhambi, basi uchawi
mwingine wowote utafanya kazi juu yake na kumletea madhara.
Swali?
WEWE NI MWAMINIFU KWA MUNGU?…NA JE! NI MWAMINIFU KATIKA
KAZI YAKO?..NA JE UMEJITENGA NA DHAMBI?
Kumbuka hakuna mtu yeyote kwa nguvu zake anaweza
kuishinda dhambi, Bali tunaishinda dhambi kwa Kumwamini kwanza Bwana Yesu,
kwamba yeye ni Bwana na Mwokozi na anaweza kutusamehe dhambi zetu na kutuosha..
Kwa kumwamini huko, na kubatizwa basi yeye mwenyewe
anaingia ndani yetu, na kutupa huo UWEZO WA KIPEKEE WA KUSHINDA DHAMBI, ambao
unatufanya kuwa Wana wa Mungu.
Yohana 1:12 “ Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa
kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake”.
Uwezo huo unatufanya tuwe watu wengine tofauti na
tulivyokuwa hapo kwanza..Ndio hapo zile pombe tulizokuwa hatuwezi kuziacha
ghafla tunajikuta tunaweza kuziacha, ule uasherati tuliokuwa tunaona ni mgumu
kuuacha tunajikuta tunaushinda, yale matusi ambayo tulikuwa tunaona ni mepesi
kuyatamka ulimini mwetu tunajikuta hatuyatoi tena vinywani mwetu n.k.
0 Comments