SOMO: HATUA ZA KUCHUKUA ILI YESU AWE NA WEWE KATIKA MSIMU MPYA
UTANGULIZI
Maana kibiblia neno msimu mpya lina tafsiri pana kidogo, wakati mwingine wanatumia neno majira au kipindi au nyakati. Jambo la msingi unalohitaji kujua ni kwamba kipindi cha msimu mpya Biblia inatuambia wazi kabisa kuwa Mungu anataka tufanikiwe kwenye hicho kipindi, na haijalishi kinatofautiana kiasi gani na kipindi kilichopita.
Leo nataka tuangalie na tujifunze juu ya hatua ya pili
HATUA YA PILI
2. MKABIDHI YESU HATUA ZAKO ILI AZILINDE NA KUZIONGOZA
USHUHUDA
Miaka kadhaa iliyopita sikumbuki ilikuwa lini bali nakumbuka kitu Yesu alinisemesha. Aliniambia nisome na kutafakari na kuelewa juu ya hatua kwa sababu aliniambia anataka si tu kuniongoza katika njia lakini alitaka kuniongoza na hatua zangu.
Wakati huo nilikuwa sijawahi kusikia somo linalohusu hatua peke yake, hivyo niliitikia kitu Yesu alinisemesha na nikaanza kuingia kwenye Biblia na kusoma na nikawa nauliza hata kwenye maduka ya vitabu kuulizia kama wana vitabu vinavyohusu masuala ya hatua za mtu na Biblia inasemaje.
Havikuwa vitabu vingi sana vilivyoeleza juu ya somo hili lakini nilipata vichache na vingine vilikuwa vikizungumzia juu ya njia. Lakini ukisoma kwenye Biblia utakuta inazungumzia juu ya “njia yake”, “njia zake”, na “hatua”. Na katika Agano jipya ukiona inazungumzia juu ya “njia yake” maana yake inazungumzia juu ya Yesu (Yesu ni njia) na ikizungumzia juu ya “njia zake” maana yake ni mikakati ndani ya njia. Nilianza kufuatilia kidogo kidogo anapozungumzia hatua ana maana gani, na ndipo aliponifundisha kukabidhi hatua zangu na si tu kujikabidhi na kutembea ndani yake.
Hivyo leo na kesho kadri Mungu atakavyonisaidia nitajitahidi kukumegea angalau kwa uchache vitu ambavyo Mungu alinifundisha, na anaendelea kunifundisha juu ya hatua ambavyo ninaamini kabisa kama vile vilivyonisaidia mimi vitaweza kukusadia na wewe na labda katika upana mkubwa zaidi, kwa sababu binafsi imenichukua miaka kadhaa kukusanya kwa pamoja na kuona vitu vikifanya kazi vitu angalau ninavyotaka kukufundisha leo na sijawahi kufundisha kwa mfumo huu ninaotaka kufundisha mahali popote pale. Kwa hiyo kuna mambo kadha wa kadha ambayo ningetaka uone;-
JAMBO LA KWANZA
I. KIBIBLIA HATUA ZA MTU ZIMEHUSISHWA NA MANENO MENGINE YAFUATAYO
Lengo langu ni kwamba utakaposoma haya maneno uyahusishe na hatua, na utakaposoma na kufuatilia habari za hatua jitahidi kutazama na kuangalia Mungu anahusisha na neno gani ili uweze kupata maana ya neno sahihi ya kile ambacho Mungu anakusemesha kufuatana na mazingira uliyonayo, la sivyo unaweza usipate maana ya neno hatua vizuri kibiblia.
Hivyo yako maneno kadhaa ambayo yamehusishwa na neno hatua za mtu:-
NENO LA KWANZA
HATUA KAMA KITENDO CHA IMANI
Zaburi 37:31
“Sheria ya Mungu wake imo moyoni mwake. Hatua zake hazitelezi.”
Kwa hiyo anahusisha hatua na matokeo ya sheria za Mungu wake kuwa moyoni. Kwa lugha tuliyonayo katika Agano jipya Neno la Mungu linasimama kama sheria za Mungu katika upana wake.
Warumi 10:17
“Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo.”
Inamaanisha ya kwamba kazi mojawapo kubwa ya Neno la Mungu moyoni mwako ni kukupa imani. Na maandiko yanasema “Sheria ya Mungu wake imo moyoni mwake. Hatua zake hazitelezi.” maana yake anakuwa na uhakika wa mahali anapokanyaga.
Kwa hiyo hatua ni kile kitendo cha imani cha kuchukua hatua na kukanyaga mahali pengine ili uondoke mahali ulipo kwa nia ya kusonga mbele. Na Biblia inataka ukanyage kwa imani na huwezi kukanyaga kwa imani kama huna neno linalokufanya ukanyage.
NENO LA PILI
KAZI MOJAWAPO YA MIGUU
Na hii ni kwa sababu hatupimi hatua kwa mikono bali tunapima hatua kwa miguu.
Ayubu 23:11
“Mguu wangu umeshikamana sana na hatua zake; Njia yake nimeishika, wala sikukengeuka.”
Anapozungumza juu ya “Mguu wangu umeshikamana sana na hatua zake” kwa tafsiri nyingine anasema “Hatua zangu zimeshikamana sana na hatua zake”
Lakini ana makusudi kwa nini ametumia neno “mguu”. Ni ili uweze kupata picha kubwa juu ya sehemu ya hatua katika mwendo wake na katika kutembea kwake.
NENO LA TATU
MADARAJA
Ezekieli 40:22,31
“Na madirisha yake, na matao yake, na mitende yake, kipimo chake ni sawasawa na kipimo cha lango lililoelekea upande wa mashariki; nao hupanda kwa madaraja saba; na matao yake yalikuwa mbele yake. Na matao yake yaliuelekea ua wa nje, na mitende ilikuwa juu ya miimo yake; palikuwa na madaraja manane ya kuupandia.”
Ukienda kwenye Biblia ya kiingereza neno madaraja yametoka kwenye neno “steps”. Kwenye ule mstari wa 22 anazungumzia juu ya steps saba/madaraja saba, sasa kwanini asiseme hatua saba au ngazi saba? ni kwa sababu alitaka tujue juu ya neno hatua, maana wenzetu wanaotafsiri Biblia huwa hawasomi Biblia ya kiingereza peke yake bali husoma na kwa lugha ambayo ilikuwa imetumika Agano la kale na ilikuwa ikimaanisha nini hivyo hutafuta na kuangalia kwa lugha ambayo haitapoteza maana.
Kwa hiyo Mungu anapozungumzia hapa juu ya madaraja, anazungumzia juu ya picha. Hivyo anataka tupate picha juu ya vyeo na juu ya viwango. Kwa sababu haya madaraja yanazungumziwa juu ya ndani ya nyumba ya Mungu.
NENO LA NNE
HATUA NI NGAZI.
Mwanzo 28:10 – 22
“Yakobo akatoka Beer-sheba, kwenda Harani. Akafika mahali fulani akakaa huko usiku kucha, maana jua lilikuwa limekuchwa; akatwaa jiwe moja la mahali pale akaliweka chini ya kichwa chake, akalala usingizi pale pale. Akaota ndoto; na tazama, ngazi imesimamishwa juu ya nchi, na ncha yake yafika mbinguni. Tena, tazama, malaika wa Mungu wanapanda, na kushuka juu yake.”
Hapo kwenye Biblia ya Kiingereza waliandika “steps” ila kwenye Kiswahili haijaandikwa “hatua” bali imeandikwa “ngazi” ili kupata picha ya ngazi kwa ajili ya kupanda na kushuka.
NENO LA TANO
HATUA NI KIUNGIO AU KIUNGO AU KINACHOUNGANISHA KATI YA ULIMWENGU WA KIROHO NA WA KIMWILI.
Hii mara nyingi utaikuta kwenye milango.
Mwanzo 28:16 – 17
“Yakobo akaamka katika usingizi wake, akasema, Kweli BWANA yupo mahali hapa, wala mimi sikujua. Naye akaogopa akasema, Mahali hapa panatisha kama nini! Bila shaka, hapa ni nyumba ya Mungu, napo ndipo lango la mbinguni.”
Ukisoma vizuri hii sentensi utaona kitu kinachotuunganisha kati ya ulimwengu wa kiroho na wa kimwili.
NENO LA SITA
HATUA NI NYAYO.
Zaburi 17:5
“Nyayo zangu zimeshikamana na njia zako, Hatua zangu hazikuondoshwa.”
Ametumia hatua, nyayo na njia kwenye mstari mmoja anataka tuone upana wake. Huko mbeleni tutaona kwa upana kidogo juu ya mahali tunakopita na mikakati pamoja na hatua zake. Ila msingi mkuu ni kwenye nyayo. Kwa nini atumie nyayo badala ya hatua?
Warumi 4:12
“Tena awe baba ya kutahiriwa, kwa wale ambao si waliotahiriwa tu, bali pia wanazifuata nyayo za imani yake baba yetu Ibrahimu aliyokuwa nayo kabla hajatahiriwa.”
Na
1 Petro 2:21
“Kwa sababu ndio mlioitiwa; maana Kristo naye aliteswa kwa ajili yenu, akawaachia kielelezo, mfuate nyayo zake.”
Ametumia nyayo badala ya hatua ili tuone kazi ya nyayo ambayo ni kwa ajili ya kuacha alama. Kwa hiyo Biblia inapozungumza juu ya hatua na ikatumia neno nyayo maana yake inakanyaga mahali kuacha alama, ili paonekane mahali ulikopita na kama kuna mtu yeyote anataka kukufuata aone hizo alama hata kama hajakuona kwa karibu kwa sababu nyayo hazifanani.
Ukiingia kwenye Biblia utakuta mistari kadhaa inayozungumzia nyayo kwa ngazi kadhaa.
JAMBO LA PILI.
II. HATUA ZA MTU NI ENEO MOJAWAPO AMBALO SHETANI ANALISHAMBULIA SANA NA MARA KWA MARA.
Hii inatokana na jumlisho ya sababu mbalimbali kwa ajili ya kukuzuia hatua zako na usikivu wako wa maelekezo ya Mungu kwako ili apate kuvuruga imani yako.
Shetani yuko njiani ili kuzuia hatua zako na anatafuta tu kuvuruga imani na kesho yako kwa sababu Biblia inasema kwenye
Waebrania 11:1
“Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana.”
Ukivurugiwa imani yako, inavurugwa kesho yako yaani ushindi wako ambao unategemeana na imani yako ambayo unatakiwa utembee nayo kwa maisha uliyonayo.
1 Yohana 5:4b
“na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani yetu.”
Waebrania 11:6
“Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.”
Mtu akivuruga imani yako, anakuvurugia pia na kibali chako kwa Mungu na mahali rahisi sana kuvuruga imani hiyo ni kwenye hatua.
Mambo ya Walawi 8:23 – 24
“Kisha akamchinja; na Musa akatwaa katika damu yake, na kuitia katika ncha ya sikio la kuume la Haruni, na katika chanda chake cha gumba cha mkono wake wa kuume, na katika kidole cha gumba cha guu lake la kuume. Kisha akawaleta wana wa Haruni, na Musa akaitia hiyo damu katika ncha za masikio ya kuume, na katika vyanda vya gumba vya mikono yao ya kuume, na katika vidole vya gumba vya maguu yao ya kuume; kisha Musa akainyunyiza hiyo damu katika madhabahu pande zote.”
Biblia inasema agano la kale ni kivuli cha mambo halisi ya ulimwengu wa roho. Kwa hiyo unapotazama mambo katika Agano la Kale yatazame kwa sura kuwa Mungu alikuwa anajaribu kufundisha kwa mifano mambo halisi yanayofanyika katika ulimwengu wa roho kwa sababu ya ngazi ya agano walilokuwa nalo.
Lakini nataka uone alichukua ile damu akagusa sikio la kulia, akagusa na dole gumba la mguu wa kulia kuonyesha ya kwamba wanahitaji kukabithi usikivu wao na mikono yao na hatua zao, kwa sababu kuna uhusiano na mahali unapokanyaga, hatua unazochukua na usikivu wako na kile unachoshika mkononi, kuna uhusiano kati ya unavyotembea, hatua unazochukua na usikivu wako na kile unachoshika mkononi sasa cheki aliunganisha na madhabahu.
Hiyo imani uliyonayo inatokea madhabahu ipi, maana ndipo mahali ambapo unaamini neno lile linalotoka pale kwa ajili ya kukusaidia, lakini pia alikuwa anatoa ishara nyingine kuhakikisha ya kwamba hatua zao zinasafishwa, zinatakaswa na kutengwa na kitu chochote kile ambacho kinaweza kuzuia wasije wakakanyanga mahali ambapo watashindwa kusikia.
Zaburi 37:23,31
“23 Hatua za mtu zaimarishwa na BWANA, Naye aipenda njia yake. 31 Sheria ya Mungu wake imo moyoni mwake. Hatua zake hazitelezi”
Mahali pengine wametumia _hatua za mtu zinaongozwa na Bwana_. Watu wengi wanataka kusikia Mungu anavyosema mwanzoni, mwanzoni mwa kipindi chao, kwa hiyo wanakuwa na Neno na ni sahihi kabisa lakini Mungu anataka katika hilo Neno alilokupa anataka kila hatua upate neno ndani ya lile neno katika kila hatua.
Kwa sababu ukipata neno utasikia, kwa sababu kusikia huja kupitia neno, na ndio maana lazima ihusishwe na sikio lako la ndani ili utakaposikia kile ambacho Mungu anataka ushike kitakuja mikononi mwako na hakita potea na ukisimama na neno utakuwa na uhakika hauwezi kuteleza mguu wako na huwezi kuyumbishwa.
Na ili kwenda hatua nyingine kwenye neno hilo hilo ambalo Mungu amekupa kwa mwaka, utapata kitu kingine ambacho Mungu anakusemesha, ndio maana ninaweza kusoma mstari huo huo lakini nakusemesha kitu kingine, Yesu ni neno! Huwezi ukamtazama Yesu ukammaliza.
Ndio maana wale makerubi na maserafi wanapokaa na kukizunguka kile kiti cha enzi kila wakati wanaona ufunuo mpya, kwa sababu hakuna aliyemwona Mungu akasema nimemwona Mungu jinsi alivyo kabisa. Wale maserafi juu ya kiti cha enzi wanaitana Mtakatifu! Mtakatifu! Na wanaitana kwa sababu kila moja amekaa kwenye angle yake halafu anaanza kuona na anaona kitu kipya ambacho hakukiona asubuhi na yule mwingine anaona sasa wanatafuta namna ya kuambiana hivi umeona nilichoona, wanashindwa kutoa maneno kwa sababu ya utukufu wa Bwana ambao umewazunguka pale.
Ndio maana Biblia inasema wanaitana Mtakatifu, Mtakatifu, hawawezi kuitana Mtakatifu wakati Mtakatifu yuko pale lakini inamaanisha neno wanalotaka kusema walishindwa maneno ya kujieleza.
Ndio maana ukisoma Biblia huwezi kusema umeelewa na kupata kila kitu kwa sababu Neno ni Mungu, Neno ni Yesu na kila wakati unaposoma lile Neno unaona kitu kipya, na kila ukiona Mungu anakupa neno la maono ya mai
sha yako, maono ya kazi yako, maono ya biashara yako, haijalishi umepata neno lina mistari mitano au kumi kisikusumbue, uwe na uhakika Mungu kama amekupa hilo neno utembee nalo miezi 12 uwe na uhakika kuna neno kila mwezi, na kuna neno kila wiki, na kuna neno kwa kila siku.
Unapokanyaga namna hiyo Mungu anakusemesha kitu na anapokusemesha kitu ndicho kinachokufanya ufanye sawa sawa na maelekezo na unapofanya sawa sawa na maelekezo shetani anapata shida sana kwa sababu kila hatua imani yako inaimarika! Kila hatua imani yako inaimarika na inapoimarika anapata shida namna ya kukushinda anapata shida namna ya kukuyumbisha, anapata shida namna ya kukunyang’anya imani yako kwa Mungu, anapata shida namna ya kukukosesha imani yako wa ajili ya kesho yako.
Watu wana mistari January inapofika Februari wamepoteza imani kwa Mungu, mwezi wa pili shida ikitokea hawataki hata kumtafuta Mungu na ghafla ile nuru aliyoiona january na akaona kabisa nitafika Desemba kwa ushindi mkubwa lakini kavurugwa tu mwezi wa pili na ghafla ile hali aliyoingia nayo Januari imepotea. Kwa sababu wewe ulipata nguvu ya kuingilia mlangoni Januari hukujifunza kurudi kwenye neno na kulitafakari na Mungu akupe neno la hatua, wewe ulitafuta neno la kupitia njia ulipata neno la mwaka lakini hukujua ndani yake kuna hatua kwa hatua.
Kwa sababu kama chakula haijalishi mwaka mpya umesherekea na kula namna gani bado tarehe 2 utakula, bado tarehe 3 utakula na utaenda kutafuta, kwa nini inapofika kwenye neno la Mungu unapewa mstari january hata kama ni wa chakula cha mwaka mzima hurudi kwa Bwana kumuuliza kila siku nitapata kitu gani, mtu hataishi kwa mkate tu bali kwa kila neno linalotoka katika kinywa chake.
Ndio maana Biblia inasema hatua za mwenye haki, zinaimarishwa na Bwana, zaongozwa na Bwana haisemi tu anakuogoza njia bali hatua na hatua huendi kwa kuruka ruka hata ukiruka ruka bado itakuwa moja, ni hatua moja baada ya nyingine, Mungu ataimarisha mahali ulipokanyaga mpaka akupe mahali pengine pa kukanyanga aimarishe mahali ulipokanyaga ndipo akupe mahali pengine.
Lakini pia anataka akuongoze usije ukapotea, ni rahisi sana unaweza ukapotea na neno unalo ni rahisi sana unaweza kuzama na Neno unalao kwa hiyo ni lazima kuwe na msaada. Unaweza ukaondoka na Neno ukakosa uwepo wake, ni rahisi sana ukaondoka na Neno la Yesu ukosa uwepo wake.
Lakini Bwana anakuwa pale kwa ajili ya kukusaidia ufanye kinachotakiwa kufanywa ili uweze kupanda daraja, kupanda ngazi fulani lakini daraja ni bridge linakuvusha uende ghambo nyingine ya msimu ambao Mungu amekusudia na Mungu atakuelekeza ni kitu gani ufanye ofsini, unapandishwa hujui ni kitu gani kimetokea, Roho mtakatifu atakuongoza kitu cha kufanya na atakupandisha daraja la kwenda kwenye madhabahu yake.
Maana yake anakupandisha ngazi na kibali chako mbele za Mungu kinaongezeka hatua kwa hatua. Kuna kibali cha kila mtu aliyeokoka lakini kuna kibali kinachokuja kwa ajili ya uaminifu wako kwa Mungu hatua kwa hatua, ukiwa mwaminifu kwa kidogo Mungu anakupa mali nyingi.
Kwanini Biblia inazungumza kwa hatua kuteleza, kwa sababu shetani anaweka makusudi kabisa ili kukuchelewesha kwa sababu kama unaendesha gari ukaanza kuteleza utaanza kuyumba na hutaenda tena kwa ile speed inayotakiwa, shetani anachowinda ni kitu gani hiyo imani uliyonayo kuna mahali inakupeleka na asingetaka ufike kwa muda unaotakiwa, asingetaka upate hicho kitu kwa muda unaotakiwa kwa hiyo atatafuta kitu chochote kinachoweza kuyumbisha imani yako.
Zaburi 17:5, 11 – 12
“Nyayo zangu zimeshikamana na njia zako, Hatua zangu hazikuondoshwa. Wamenifuatia; na sasa wananizunguka, Na kuyakaza macho yao watuangushe chini. Kama mfano wa simba atakaye kurarua, Kama mwanasimba aoteaye katika maotea yake”
Angalia pia kitabu cha:-
Amosi 3:12
Haya ndiyo asemayo BWANA; Kama vile mchungaji apokonyavyo kinywani mwa simba miguu miwili, au kipande cha sikio; ndivyo watakavyopokonywa wana wa Israeli, wakaao Samaria katika pembe ya kochi, na juu ya mito ya hariri ya kitanda.
Katika kitabu cha Zaburi Biblia inasema wametuzunguka hatua zetu hii ina maana Shetani au watu amb
ao watu shetani anawatumia kukwamisha watu. Pia imeliwalinganisha watu hawa kama Simba kama tulivyosoma katika kitabu cha Amosi.
Mungu anapotaka kuwakomboa wana Israeli huwa hafanyi kila kitu bali aananza kwa kuwakomboa miguu miwili au kipande cha sikio.
Je Mungu anamanisha nini anaposema atawakomboa wana Israeli kama vile mchungaji anavyowakomboa kondoo wake waliochukuliwa na simba maana mchungaji anahitaji kuwahi miguu ya kondoo wake au kipande cha sikio toka kinywani mwa simba.
Hapa anataka tujue kuwa Mungu akiweza kuomboa miguu yako au kusikia kwako maisha yako yanakuwa yamepona.
Shetani akitaka kukushambulia huwa anashambulia kwanza hatua zako. Anafanya hivi kwa sababu nyingi sana Ila sababu mojawapo ni kukufanya ushindwe kuunganisha hatua zako na usiku wako.
Shetani analenga kukamata miguu ya watu na masikio yao ili aweze kuwakwamisha katika msimu mpya.
Wana Israeli walipoona Musa kachelewa kuja kutoka mlimani,wakamwambia Haruni kuwa ameke mtu ambaye atawaongoza kurudi Misri. Haruni aliwaambia kuwa leteni pete za masikioni mwenu.
Hii ni ishara au alama ya kukabidhi usiku wao kwa mungu mwingine ili wasimsikie Mungu. Pia walitoa na bangili zilizokuwa miguuni kwao na kwenda kutengenezea ndama.
Hapa unaweza ukaelewa kwanini Musa alipoteremka kutoka mlimani alikasirika sana . Alisema aliye upande wa Mungu na aje kwangu. Watu wachache sana ndio walioenda upande wa Mungu.
Hawa watu mara ya kwanza walikasirika baada ya Musa kutokuwepo lakini sasa amekuja lakini hawamtaki tena. Hii ni kwa sababu walikuwa wamekwisha banwa na mungu mwingine.
Haijalishi Musa amekuja na Mungu mjini. Lakini hawamtaki. Musa alikasirika sana, kwa sababu hiyo alisema wale walio upande wa Mungu na waje kwangu. Walienda wachache sana. Musa akakasirika sana kwa hiyo akawapa watu mapanga akifikiri kwa kuwatishia watu hao kufa wanaweza kuacha imani waliyopata. Maana ikifika mahali pa namna hiyo pa imani kushikilia mioyo ya watu wanaweza wakakubali kufia imani zao.
Hatua za mtu zimeunganishwa na moyo, nafsi na utayari wake katika neno la Mungu. Kwa hiyo shetani akitaka kuufikia moyo wa mtu huwa anawahi kukamata hatua za mtu.
Zaburi 44:18
“Hatukuiacha mioyo yetu irudi nyuma, Wala hatua zetu hazikuiacha njia yako,”
Maana yake kama hatua zikiacha njia basi hata mioyo huwa inarudi nyuma na kama itakuwa hivyo basi hata hatua haziwezi kusonga mbele. Kwa hiyo ujue kuwa kuna uhusiano kati ya moyo wako na hatua zako.
Mithali 16:9
“Moyo wa mtu huifikiri njia yake; Bali BWANA huziongoza hatua zake”
Mungu anajua kabisa mtu akimkabidhi hatua zake baada ya muda atakuwa anaongoza na moyo wake. Maana kuna uhusiano kati ya hatua za mtu na moyo wake.
Zaburi 17:5
“Nyayo zangu zimeshikamana na njia zako, Hatua zangu hazikuondoshwa.”
Pia angalia na
Zaburi 56:6
“Hukutanika, hujificha, huziangalia nyayo zangu, Kwa kuwa waliniotea ili waniue.”
Kwa hiyo wanaoiotea nafsi yako hawahitaji kuangalia nafsi yako bali wanahitaji kuangalia hatua zako ili kuifikia nafsi yako.
Zaburi 57:6
“Wameweka wavu ili kuninasa miguu; Nimevunjika moyo; Wamechimba shimo njiani mwangu; Lakini wao wenyewe wametumbukia humo!”
Kwa hiyo wakitaka kukatisha tamaa huwa wanashika miguu yako na nafsi yako inainama. Hii maana yake wakishika maendeleo yako au hatua zako huwa wanashika na nafsi yako. Kwa hiyo Shetani ili ashike nafsi yako huwa anashika hatua zako kwanza.
Biblia inazungumzia juu ya silaha kubwa ambayo tumepewa katika Waefeso 6:15 Biblia inasema tuvikwe utayari miguuni uletwao na injili ya amani.
Mithali 4:11 – 13
“Nimekufundisha katika njia ya hekima; Nimekuongoza katika mapito ya unyofu. Uendapo, hatua zako hazitadhiikika, Wala ukipiga mbio hutajikwaa. Mkamate sana elimu, usimwache aende zake; Mshike, maana yeye ni uzima wako.”
Watu ambao hawataki kusoma shule huwa wameshikwa hatua zako. Biblia inazungumza hatua kuridhika wakati Mungu anakazana kukufundisha. Kama unahitaji aina fulani ya mafundisho kuweza kufikia kiwango fulani mbele yako na ikiwa shetani ataingilia hatua zako unaweza ukakwama kabisa.
Ayubu 23:11 – 12
“Mguu wangu umeshikamana sana na hatua z
ake; Njia yake nimeishika, wala sikukengeuka. Sikurudi nyuma kuiacha amri ya midomo yake; Nimeyatunza maneno ya kinywa chake zaidi ya riziki yangu”
Mguu wangu umeshikamana sana na hatua zake; Hapa ungeweza kusema hatua zangu zimeshikamana na hatua zake. Maana yake unakuwa na utayari ndani yako ya kulifuatilia neno na hamu au kiu kubwa ya neno kuliko ya riziki yako.
Hii ni kwa sababu neno ndio linalokupa riziki yako na ndilo linalokuongoza. Maana kwa neno hilo ndilo linalofanya Mungu akulishe, akutunze na akuongoze katika maisha yako.Kwa hiyo huwezi kufurahia riziki kuliko neno, kwa sababu Biblia inasema mtu hataishi kwa mkate tu bali kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.
Neno la Bwana litakuongeza hatua na hii itakufanya kujua namna Mungu atakavyokuwa anakuongoza na kukutunza katika msimu mpya.
Kama hatua zako zitakuwa zimeungana na moyo wako, ina maana Mungu atakuwa anakuongoza mahali pa kukanyaga. Hii itafanya utayari wako kutegemea usikivu wako na kama usiku wako utakuwa umekwisha ina maana mguu wako utakuwa umevikwa kitu kingine. Kwa hiyo huwezi kanyanga mahali na ukasikia kitu ambacho Mungu anataka usikie.
Siku ukifika mbinguni ukipata nafasi ya kuongea na Musa wewe mwenyewe uje umuulize kuwa siku ambayo Mungu alisema vua viatu vyako maana mahali hapa ukanyangapo ni patakatifu je alikuwa anamaanisha nini?
Ukisoma Biblia utaona kuwa Musa alipoona kile kijiti kinawaka lakini hakiteketei. Biblia inasema Musa alichukua hatua kwenda ili akatazame. Lakini Mungu alimzuia ina maana alizuia hatua za Musa kusogea. Hii si kwamba Mungu alikuwa hamtaki Musa bali alikuwa na shida na viatu alivyokuwa kavaa.
Mungu hamkuruhusu Musa kuingia na vile viatu mahali patakatifu, yaani mahali ambapo kapatenga kwa ajili ya kusema nae. Maana vile viatu vingekuwa vinampa tafsiri nyingine na ndio maana alimwambia vua viatu vyako.
Hapo alikuwa anasema vua mavazi yako ambayo unaona kama yatakusaidia msimu huu, bali mimi Mungu nitakupa wazo lingine.
Pia ukisoma hii habari utaelewa ya kuwa kwanini Haruni alipoingizwa kazini ilikuwa ni lazima kidole chake na miguu yake iguswe na damu. Hii ilikuwa ni kwa ajili ya kuondoa kitu chochote ambacho kitawakwamisha wasifanye kile ambacho Mungu kawapa kufanya.
Hata kwa Yoshua ilikuwa ni hivyo hivyo nae alikuwa na mipango yake ya kupamba na mji wa Yeriko. Alikuwa na mipango mbali mbali lakini Malaika alisimama mbele zake. Joshua alitambua kuwa hayuko upande wake wala upande wa adui.
Yule malaika akasema mimi ni amiri jeshi wa Bwana. Joshua akapomoka kiuso uso mbele ya yule Malaika na akasema Bwana aniambia nini. Yule malaika akamjibu akasema vua viatu vyako. Maana yake alikuwa anamwambia Joshua kuwa huu ni msimu mpya kwenu ondoa mipango yako uliyonayo.
Maana Joshua alianza kuweka mipango yake badala ya kumtegemea Mungu ambaye alimvusha mto Yordan na kuwatoa Misri. Sasa yeye Mungu alipomwambia vuka alifikiri ataendelea na nguvu ile ile bali alikuwa anahitaji neno jipya kutoka kwa Bwana.
Kwa hiyo ilikuwa haijalishi namna anavyosujudu mbele ya Malaika lakini hatua zake zilikuwa zinazuia uelewa na utayari wa kufanya kitu ambacho Mungu kamwambia.
Mungu alikuwa anatafuta ili tuweze kuona kuwa shetani akitaka kunyang’anya utayari wa kusoma neno huwa anashika hatua zako au miguu yako.
Wakati Mungu alipokuwa ananiambia kuwa ataongoza hatua zangu njiani aliniambia kuwa soma, tafakari na uelewe neno. Kwa hiyo nilianza kutafuta ndani ya Biblia na niliona mambo ya ajabu sana.
JAMBO LA TATU
III. USIPUUZIE NDOTO UNAZOOTA NA KUONA UNASHAMBULIWA KWENYE MIGUU YAKO.
Ayubu 33:8 – 9
Hakika umenena masikioni mwangu, Nami nimesikia sauti ya maneno yako, ukisema, Mimi ni safi, sina makosa; Sina hatia, wala hapana uovu ndani yangu.
Elihu alikuwa anamwambia kuwa Ayubu haya maneno yamesikika kuwa ukisema, “Mimi ni safi, sina makosa; sina hatia, wala hapana uovu ndani yangu”. Kwa lugha nyingine Ayubu anamwambia Mungu kuwa hakukua na hatia yoyote inayomfanya Ayubu apate yale majaribu. Maana yeye aliona yuko safi hana uovu hamna sababu inayosababisha akaingizwa kwenye shida yote ile.
Maana Ayubu alikuwa kapoteza mali zake na watoto wake. Pia mke wake naye kafarakana nae na hata yeye mwenyewe anaumwa hata marafiki zake walikuwa ni wafariji wataabishaji.
Ayubu 33:15–16
Hunitia miguu yangu katika mkatale, Na mapito yangu yote huyapeleleza. Tazama, nitakujibu, katika neno hili huna haki; Kwa maana Mungu ni mkuu kuliko mwanadamu. Kwa nini unapingana naye, ukisema, Hatajibu hata neno langu moja? Kwa kuwa Mungu hunena mara moja, Naam, hata mara ya pili, ijapokuwa mtu hatambui. Katika ndoto, katika maono ya usiku, Usingizi mzito uwajiapo watu, Katika usingizi kitandani;Ndipo huyafunua masikio ya watu, Na kuyatia mhuri mafundisho yao.
Hapa alikuwa anaambiwa kuwa kuna kitu Mungu alisema na Ayubu kwa njia ya ndoto na hukufuatilia. Alafu sasa Ayubu anasema sasa yuko safi na hana makosa lakini miguu yake imeshikwa na hasogei. Kwa hiyo Mungu alizungumza nae kwa njia ya ndoto usiku alipokuwa amelala.
Watu wengi sana si rahisi sana kumsikia Mungu mchana, hasa wakiwa wanapita mahali pagumu. Maana wengine wakipita mahali pagumu wanapoteza usiku wao. Ndio maana Mungu anasema nalisema nawe katika saa ya kufanikiwa kwako na hukutaka kusikia.
Ukiwa mzito kusikia kitu ambacho Mungu anakuambia anakusubiri usiku ukiwa umelala atakusemesha kwa njia ya ndoto ili ujue kwanini umekwama. Kwa hiyo watu wengi hawajadaka na hawafuatilii ndoto hizo na wanajikuta wamekwama.
Je umewahi kuona mtu ambaye kaota kuwa miguu yake imefungwa? Mtu akifungwa miguu yake hatua zake hazisogei. Pia ni muhimu kuangalia je miguu yake imefungwa wapi?ni ofisini ina maana hutasogea na kuna ngazi hutapanda.
Pia kuna mtu mwingine anaota kuwa anapanda ngazi alafu hafiki mwisho. Pia kuna mtu kaota anapanda ngazi lakini ni kwa shida sana mpaka anaamka anakuwa bado hajafika.
Pia kuna mwingine anaota miguu yake ni mizito sana hawezi hata kuvuka daraja moja. Pia mwingine anaota anapanda ngazi na anapofika mwisho anakuta mlango umefungwa.
Mungu alizungumza kutoka mwisho wa zile ngazi za Yakobo akisema mimi ni Mungu wa baba yako. Pia kuna mtu anaota anasafiri alafu alifika kwenye daraja anakuta limevunjwa.
Hii ina maana hatua ni daraja, yaani kiungio cha daraja lako moja na lingine kimeondolewa na aliyekiondoa ni shetani. Au hujawahi kuona anapotaka kuvuka kwenye daraja unakutana na geti. Hapo utakuwa unaona husogei katika hatua ya maisha yako, na baada ya muda utaanza kuona katika maisha yako ya kuwa uhisi kuna mahali umekwama.
Watu wengi wamebanwa hapo na hawajui kitu cha kufanya. Pia kuna watu wanaota wameshambuliwa miguu yao na chui au simba na ndoto hizi zina maana kila moja katika ulimwengu wa roho.
Pia unapoumwa na kitu kwenye miguu kuna kitu kinaingizwa ndani yako inaweza ikawa ni sumu au roho inayowakilishwa kile kilichokuuma.
Ukisoma Biblia unaona yule nyoka wa kwenye bustani ya Eden unaona ya kuwa alidanganya fikra za Adamu na Eva mkewe. Maana yake alikamata nafsi zao kwa sababu akili iko kwenye nafsi.
Kama umeumwa na mdudu angalia maana yake nini?Pia kama umechomwa na mwiba pia fuatilia. Mungu anataka ufuatilie hili jambo kwa sababu huwezi kumkabidhi Mungu kitu ambacho wewe mwenyewe huna.
Kama umekabidhi moyo wako kwa mungu mwingine lazima umkatae kwanza, kama mnavyosema kanisani kuwa namkataa shetani na nakukubali wewe Mungu. Katika ulimwengu wa roho hamna raia na falme mbili. Huku Duniani unaweza ukapata ukawa raia wa Marekani na Uingereza kwa muda mmoja.
Ukitaka kuwa katika ufalme wa Mungu lazima urudishe ya shetani pia ukitaka kwenda kwa shetani pia lazima urudishe ya Mungu. Kwa hiyo huwezi kusema unakabidhi hatua zako kwa Mungu wakati hauna au wakati zimeshikwa na kitu kingine. Kwa hiyo lazima utafute namna ya kuzitoa kwanza huko ndipo ukabidhi kwa Mungu.
Je hujawahi kuona mtu ambaye anaota anatembea peku peku au ana viatu lakini anatembea mahali pachafu na haelewi ni kwanini!.
Pia unaweza kuta unang’ang’ana kuomba Mungu akupandishe cheo fulani lakini unakuta umeota ndoto ya kuwa unavaa viatu vikubwa kuliko miguu yako. Mungu anakuambia hapo hicho cheo sio saizi yako.
Na tutaomba juu ya jambo hili na tutatoa sadaka pia ya kumshukuru Mungu kutupa kujifunza somo hili.
0 Comments