1. Usimlaumu, usimlalamikie wala kumkejeli mumeo anaporudi
nyumbani mikono mitupu au anaposhindwa kuhudumia kama alivyotarajiwa tofauti na
tabia yake ya kawaida, badala yake mtie moyo ya kwamba unaelewa hali halisi na
siku moja hali itakuwa sawa tu. Yamkini mtu mmoja pekee wa kumpa maneno hayo
kwenye ulimwengu wake ni wewe tu, usimkatishe tamaa bali uinue moyo wake
uliovunjika. Neno lako moja la faraja lina nguvu kuliko maneno 100 ya mtu
mwingine. Hata kama amekuwa ana tabia za kutokubeba majukumu vile unavyopenda
wewe, fahamu kwamba kejeli, makelele na lawama za mfululizo hazitokupa matokeo
mazuri zaidi ya kuja kukuongezea maumivu tu.
2. Nafahamu fika kuwa mke anaweza kuwa na kazi yake na kipato chake pia, tena mara nyingine kipato kikubwa kuliko cha mume, lakini ukweli ni kwamba katika familia nyingi sana kipato cha baba ndicho kinatumika kuendesha familia. Wako wanawake wengi kwenye ndoa ambao ni wafujaji na wenye matumizi mabaya sana ya fedha na rasilimali za familia na bado hawaoni ni tatizo. Kwa sababu tu mume analeta basi kwao kila kitu kinatakiwa kutumika muda wowote, utaona matumizi mabaya ya fedha na hata ya chakula na hakuna huruma yoyote kwa jasho la mumewe. Nikukumbushe tu wewe mke kwamba jasho la mume wako lina gharama na thamani kubwa sana na halistahili kutothaminiwa na kupotezwa bure. Usisahau kwamba tabia yako ya kawaida ni shule nzuri kwa wanao.
3. Kamwe usijifanyishe kuwa unaumwa au una ugonjwa ili tu kumnyima mume wako tendo la ndoa, msaidie kuitimiza kiu yake kwa kadri anavyotamani kwa sababu tendo hilo ni muhimu zaidi kwa mume wako. Kwa kumnyima au kulitumia tendo hilo kama adhabu haitombadilisha tabia na kumfanya awe mwema utakavyo badala yake itamgeuza kuwa mbaya zaidi na kuna uwezekano mkubwa hiyo ndiyo ikawa tiketi yake ya kwanza ya kutoka nje ya mahusiano yenu, ili kutafuta tendo hilo alilolikosa kwako. Fahamu kwamba ni kitu kigumu sana kwa mwanaume wa kawaida aliyeoa na aliyekamilika kukaa muda mrefu pasipo tendo hilo.
4. Kamwe usimlinganishe au kumfananisha mume wako na yeyote
ambaye amewahi kuwa mpenzi wako huko awali. Hata kama nia yako ni nzuri ila
tafuta mlingano mwingine ila sio na ex wako. Kosa hilo linaweza kuifanya ndoa
yako isipone kirahisi kutoka kwenye hilo jeraha. Kuwa makini sana.
5. Najua tunatofautiana utamaduni na namna tunavyoishi kwenye ndoa zetu ila mara nyingi jaribu kuepuka kumsemea mume wako au kujibu kwa niaba yake pasipo ridhaa yake. Acha achukue jukumu la kusema au kujibu kama yeye ndio amehitajika kufanya hivyo, ingawa mara nyingine yeye akisema kwa niaba yako inaweza isilete shida na bado mambo yakaendelea vizuri tu. Kuna mambo kwenye ndoa ni kama gia za gari, hata kama gia namba moja na mbili na tatu zote ni gia lakini lazima uanze na moja uende mbili halafu tatu, sasa unapo lazimisha kuanzia gia namba nne kwa sababu tu gari ni lako unasababisha tatizo kwenye gari na watu watasema dereva wa hili gari ni kichaa.
MUNGU AKUBARIKI SANA
MCHUNGAJI LAURENT MPOMA
NCHI YA UKOMBOZI MINISTRY
MAOMBI NA MAOMBEZI
0714890889
WHATSAP: +255762756542
YOUTUBE: Chuma Cha Mungu Tv
0 Comments