Follow us

somo: MBINU 5 ZA KUJIHAMI NA KUPAMBANA NA MAJARIBU

Tangazo

MCH: LAURENT MPOMA
NCHI YA UKOMBOZI MINISTRY TANZANIA


MBINU 5 ZA KUJIHAMI NA KUPAMBANA NA MAJARIBU


1.      1. KESHA UKITAMBUA UDHAIFU WAKO

Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu (Math 26:41)

Mlinzi aliye makini anajua anapaswa kukaa chonjo kulinda maeneo dhaifu ambayo adui anaweza kuyatumia na kumuingilia. Miili yetu ina nyufa za udhaifu. Japokuwa udhaifu wa miili haufanani. Udhaifu wako unaweza kuwa sio udhaifu wa wenzako.

Jaribu moja linaweza kuwangukia watu wawili, lakini wakatofautiana kuhisi uzito wake kulingana na maumbile ya kihaiba au historia ya kiroho ya kila mmoja wao. Hivyo jichunguze. Kama kitendo cha kunusa harufu ya sigara, kusikia muziki wa lege, kugusa kiganja cha mpenzi, au kutazama filamu, kinaamsha hisia au kumbukumbu fulani---inayokusukumia uvuke mstari mwekundu, basi tambua hilo haraka na urudi nyuma kwa usalama wako. Mtume Paulo anatoa ushauri huo huo kwa kijana Timotheo, akimwambia, “zikimbie tamaa za ujanani” (2Tim 2:22). Na tena tunahimizwa na mtume, “tuweke kando kila mzigo mzito, na dhambi ile ituzingayo kwa upesi” (Waeb 12:1.) Unapotambua udhaifu wako jihadhari nao kwa kutobakia katika mazingira hatarishi kwa usalama wako.

Ni muhimu mno kuzingatia tahadhari hiyo. Bora kuwa mwoga wa kukimbia dhambi inayokuotea mlangoni na ukaishia kuishi siku nyingi kama kunguru, kuliko kuwa jasiri wa kumkaribia chatu na kufa mapema kipumbafu kabla ya siku zako. Ni salama kutembea katikati ya njia kuu na kufurahia ujana wako kwa kitambo kirefu, kuliko kuchepuka njia za mkato ukaishia kugongwa na nyoka wenye sumu. Afadhali ufahamu udhaifu wako mapema na uchukue hatua za haraka kuudhibiti kabla haujadhulika.

2.   FIKIRI MADHARA YANAYOWEZA KUKUPATA KWA KUKUBALI USHAWISHI

 Je! Mtu aweza kukanyaga makaa ya moto, Na nyayo zake zisiungue? (Mith 6:28)

Ni ngumu kufikiria madhara ya kishawishika Mjaribu anapokujia na ahadi nyingi. Anakwambia, kula tunda hili nawe utafanana na Mungu. Kunywa kidogo nawe utasahau misongo ya umaskini wako. Achia breki za uaminifu nawe ujimwage katika anasa. Ni hapo baadaye tu, baada ya kuridhia, ndipo unapojiuliza, 'nimefanya nini?' Uzuri wa moto ni pale ukiwa mbali.

 

3.            JITAMBUE WEWE NI NANI NA AMUA MAISHANI MWAKO LA MUHIMU NI LIPI

Kwa imani Musa alipokuwa mtu mzima, akakataa kuitwa mwana wa binti Farao; akaona ni afadhali kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha katika dhambi kwa kitambo. (Waeb 11:24,25)

Dalili ya kuwa mtu mzima ni kujua wewe ni nani na lipi la muhimu katika maisha yako. Musa alipoingia tu utu uzima aljiitambua yeye ni nani. Kwa kujitambua kama mtoto wa Mungu na si wa farao aliweza kuzikimbia anasa za ikulu na kukimbilia mateso pamoja na watu wa Mungu. Upepo wa majaribu hauna nguvu kwa mtu anayejitambua na aliye na vipaumbele  anayoyathamini maishani kabla ya vingine.

 

4.           OMBEA WOKOVU DHIDI YA MAJARIBU YANAYOKUKABIRI

Ombeni kwamba msiingie majaribuni (Luk 22:40). Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliye mbinguni,….usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu. (Mat. 6:9,13)

Ombi la kupokea nguvu ya kustahimili majaribu ni ombi ambalo Mungu anatamani kulijibu. Ndiyo maana Yesu alituwekea ombi hiilo mdomoni mwetu akitutaka kila tusalipo tulitaje ili tupokee wokovu. Na Yesu kwa kusema hivyo alijua kuwa, “Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili.” (1 Kor 10:13). Na kwa kuwa Mungu anataka kukusaidia katika mapambano yako dhidi ya majaribu, unapaswa uombe. Lakini, omba ipi inayofika masikioni mwa Mungu?

Omba kwa bidii. Usimwombe Mungu kwa kujaribu. Usim-beep ikiwa kama unashida naye ya dhati. Omba kama Eliya alivyoomba kwa bidii mvua iliyozuiliwa miaka mitatu inyeshe (Yak 5:17; 1Waf 17). Mungu anataka kujua kama unamaanisha unachokiomba. Ukionesha bidii kwamba unajali kupokea wokovu wake hakika utajibiwa. Maana, “Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii.” (Yak 5:16)

Pia omba kwa imani. Usiomwombe Baba Mungu kama watoto wa mitaani wanavyoomba msaada kwa Wapita-njia. Tena, usiombe kama manabii wa kishenzi (wa mungu Baali) wanaoomba wakijitaabisha ili mungu wao aguswe na huruma na kuwaokoa (1 Waf 17). Ombea wokovu  dhidi ya majaribu kama mwana wa nyumbani anayetarajia kupokea zawadi njema kutoka kwa Baba anayejali (Luk 18:7). Omba bila mashaka. Omba kwamba mapenzi ya Baba yatimizwe kwako; ukiamini kuwa, “katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake” (War 8:28).  Nawe kwa imani hiyo utaona mlima wa majaribu uking’oka mbele yako na kuzama katika bahari ya kusahaulika (Mar 11:23)

5.  SIFIA WEMA NA UWEZO WA MUNGU KWA NYIMBO NA PAMBIO

Mtu wa kwenu amepatikana na mabaya? Na aombe. Ana moyo wa kuchangamka? Na aimbe zaburi. (Yak 5:13; linganisha na Kol 3:16; Efe 5:19)

Zaidi ya kuomba kwa imani, unapopatikana na changamoto, changamka katika sifa. Vaa uchangamfu wa Yehoshafati umshinde adui yako (2Nyak 20:20,21). Imba nyimbo za ushindi  ukaribisha ushindi. Imba nyimbo za Paulo na Sila uuone wokovu wa Bwana kwa kishindo na tetemeko (Matendo 16:23-29). Kamwe Mungu hatabakia kwenye kiti chake cha enzi ametulia, anawaangalia wanawe pasipo kufanya kitu—wanawe wanaosifia Mungu wao masikioni mwa adui zao. Kamwe, Mungu hatawaangusha watu wake wanaoshikiria imani yao kwake hata kwa kumuimbia. Na kama wataanguka chini, siku ya tatu atawanyanyua toka mavumbini; maana, hawastahili kuwepo hapo chini. Ita ushindi kwa nyimbo za sifa na shukurani, “Mungu na ashukuriwe atupaye kushinda kwa Bwana wetu Yesu Kristo.” (1Kor 15:57)


<<<<MUNGU AKUBARIKI SANA>>>>

MAOMBI NA MAOMBEZI

WASILIANA NA MCHUNGAJI LAURENT MPOMA

NCHI YA UKOMBOZI MINISTRY TANZANIA

(HUDUMA YA MAOMBEZI)

PIGA AU WHATSAP : +255762756542

 

Post a Comment

0 Comments