Follow us

HATUA 12 ZA KUOMBEA HALI YA KIROHO YA ARDHI ILI UFANIKIWE KIMAISHA

Tangazo

 

MCHUNGAJI LAURENT MPOMA

NCHI YA UKOMBOZI MINISTRY

HATUA 12 ZA KUOMBEA HALI YA KIROHO YA ARDHI ILI UFANIKIWE KIMAISHA.

Ukipita mitaa mingi utakuta kuna nyumba nyingi hazijakamilika kujengwa, kuna wengine wamekamilisha kujenga kabisa lakini wanashindwa kukaa ndani yake, mtu kama huyu unamuombeaje? Tutapitia hatua kadhaa hapa.

HATUA YA KWANZA

1. PELEKA OMBI HILO KWA MUNGU (IWE NI WEWE MWENYEWE AU HITAJI LA MTU MWINGINE)

Mtu akileta hitaji lake kwako sio kwamba hana Mungu, bali anahitaji msaada wa maombi kutoka kwako. Sasa Mungu anaweza akakusemesha moja kwa moja wakati huyo anakuambia hitaji lake au akakusemesha mapema kabla hajaja. Muhimu fikra zako zifikiri kuwa hilo jambo unalipeleka kwa Mungu kwa eneo ulipokwama kimafanikio.

HATUA YA PILI

2. POKEA NENO LA MUNGU UNALOPEWA NA MUNGU KWA AJILI YA HUYO ANAYEOMBA UMWOMBEE

Zaburi 107:19 - 20 “Wakamlilia BWANA katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao. Hulituma neno lake, huwaponya, Huwatoa katika maangamizo yao.”

Isaya 55:11 “ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma.”

Hapo utaona kuna neno la Mungu ambalo ndani yake kuna wazo la Mungu ambalo lina mkakati wa Mungu ambalo ndani yake kuna mvua inayotakiwa kuotesha. Ikimaanisha kila neno linalokuja ndani yake kuna upako wake na linahakikisha linafanikiwa katika lile lilokusudiwa.

Watu wengi wanafikiria maombi peke yake yatawafanikisha, hapana, maombi yanabeba mahitaji yako kwa Mungu na Mungu akitaka kukufanikisha atakupa neno. Ndio maana ni hatari sana unapoenda kanisani, unahitaji maombi na sio neno. Au unafika kwenye mkutano muda wote unawaza ataomba saa ngapi lakini hutaki kukaa chini ili usikilize neno.

 

Ni gharama kubwa kwako kuishi ukitegemea maombi kwa sababu ni maisha yasiyo na mafanikio. Maombi yanabeba mahitaji toka kwako kwenda kwa Mungu, neno linabeba majibu kutoka kwa Mungu kuji kwako. Ni mawasiliano ya njia mbili, na sio Mungu akusikilize wewe tu.

Yesu alisema katika Mathayo 4:4 “Naye akajibu akasema, Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.” Usije ukabadilisha sehemu ya neno ukaweka maombi kwa sababu maombi peke yake hayawezi kukufanikisha. Jaribu kutafuta waombaji wazuri halafu ona na maisha yao. Nchi inaweza ikawa na waombaji wazuri sana lakini wasipokuwa na neno la Mungu hawatakuwa na maendeleo. Pia viongozi wasiopokea neno la Bwana katika nchi yao, wasahau kuwa na maendeleo kabisa.

Hii ni sawa na mtu ambaye mvua imenyesha lakini amesahau kutafuta mbegu za kupanda na anasubiri mavuno, na ukimuuliza anakuambia mvua ilinyesha. Ukimuuliza ulipanda mbegu? Atakujibu aliomba ila hajapanda mbegu. Kwa hiyo ni muhimu sana kuwa na neno la Mungu ili likusaidie wakati wa uhitaji wako wa kimazingira, ndio maana Mungu aliweka msisitizo kwenye neno.

HATUA YA TATU

3. OMBA MUNGU AKUPE KUSIKIA MWONGOZO WAKE KWAKO KUTOKA KWENYE NENO ULILOPEWA NA MUNGU KWA AJILI YA KUMWOMBEA HUYO MTU AU WAKATI ULIPOJIOMBEA MWENYEWE

Warumi 10:17 “Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo.” Kuna kusikia sauti ya neno, na hiyo sauti ndiyo inakutengenezea uhakika ambao unakupa imani. Sawasawa na Waebrania 11:1 na Waebrania 11:3“Imani haiji kwa neno, bali huja kwa kusikia.”

Haijalishi ni imani ya namna gani. Imani yako kwa mganga wa kienyeji au kwa hospitali fulani na daktari fulani zote zilikuja kwa kusikia. Sasa ili ujue ni imani ya namna gani, lakini lazima ujue ulisikia kwa namna gani. Kama ni imani kwa Mungu kupitia Yesu Kristo lazima utasikia kwa kuletwa na neno lake.

Imani humpa mtu ufahamu na kujua kwa hiyo utajua namna ya kuomba ipasavyo ili uweze kutoka mahali ulipo. Ndio maana hiki kipengele cha tatu ni cha muhimu sana kuwa Mungu akupe kusikia kutoka kwenye neno ulilopewa ili imani yako ijengeke na uje ufanye nini.

 

Tuangalie mfano hapa. Kumbukumbu la Torati 8:7, 11-12 “Kwa kuwa BWANA, Mungu wako, yuakuingiza katika nchi nzuri, nchi yenye vijito vya maji, na chemchemi, na visima, vibubujikavyo katika mabonde na milima; Jihadhari, usije ukamsahau BWANA, Mungu wako, kwa kutozishika amri zake, na hukumu zake, na sheria zake, ninazokuamuru leo. Angalia, **utakapokuwa umekula na kushiba, na kujenga** nyumba nzuri na kukaa ndani yake;”

Anapozungumzia ujenzi na kuhusisha na ardhi inamaanisha anazungumzia kumwingiza huyo katika nchi. Nchi maana yake ni ardhi yenye mipaka halali ya kiumiliki.

Maana yake anampa eneo la kujenga kwa hiyo kuna suala la kumiliki ardhi kihalali kiroho na kimwili kabla ya kujenga. Kwa mfano wale wanaojenga karibu na barabara wasisahau kuwa barabara ina haki kuliko wao. Barabara ikiamua kupita, utaipisha tu haijalishi umejenga nini hapo.

Katika misingi sheria ya nchi mbalimbali, sheria ya barabara ina nguvu kuliko sheria ya kumiliki kwako nyumba. Barabara iko tayari ikulipe ili utoke kwenye njia hiyo na kuna muda wanajua kuwa barabara itapanuka patawekwa na eneo la akiba ya barabara sasa nawe usijifanye mjanja ukajenga huko. Haya mambo yote yapo kwenye Biblia ila nitakuonyesha pole pole.

Mungu anapowaambia kuwa atawaingiza katika nchi, kabla kisheria haijawa ya kwao kimwili, ilikuwa ya kwao kwa jinsi ya sheria kiroho.

Agano ni sheria mama ya sheria zote. Ni sawa na katiba ambayo ni sheria juu ya wananchi wote walioko katika mipaka hiyo ya kiutawala. Sasa kiroho kuna kitu kinaitwa agano la Mungu au la miungu ambayo ni sheria mama inayobeba sheria ndogo ndogo kuweko na ndani yake inakuwa na vipengele vya ardhi.

Hakuna agano lolote lisilo na kipengele cha ardhi. Ndio maana Mungu anasema utakapokuwa umekula na kushiba, na kujenga nyumba nzuri na kukaa ndani yake;”

Kwa hiyo kuna suala la kujenga na siyo kujenga tu bali hata kiwango cha ujenzi huo inapaswa iwe nzuri. Je nyumba nzuri ni ipi? Wewe unaweza ukasema hiyo nyumba ni nzuri lakini Mungu anaona sio nzuri. Maana yake kuna kiwango fulani cha nyumba za watu wake alizoziweka.

Si suala tu la kujenga nyumba au barabara bali ni kwa kiwango kipi cha ubora ambacho nyumba hiyo au barabara hiyo imejengwa? La sivyo baada ya miaka michache imeshaharibika.

USHUHUDA

Wakati fulani tulienda kwenye shule ya msingi ambayo mke wangu alisoma zamani. Tulipoenda kuangalia jengo la darasa la kwanza na la pili tukakuta kilichoanza kubomoka ni milango. Madawati yalikuwa yamebaki machache sasa. Cha ajabu tuliona ukutana na sakafu bado vikiwa imara.

Walimu walioko pale wakatupeleka kwenye darasa lingine ambalo ndio limemaliza miaka miwili tangia limejengwa. Na sakafu na ukuta wake ulikuwa umeanza kutoboka toboka. Fedha zilizotumika kujenga jengo hilo lililotimiza miaka miwili ni kubwa sana kuliko fedha jengo la zamani.

Suala la ubora wa jengo ni suala la kiroho kabla halijawa la kimwili. Sasa anazungumza suala la kukaa ndani yake. Haupaswi tu kujenga bila kukaa ndani yake lazima utumie hilo jengo vizuri.

Kwa hiyo kuna umuhimu wa kusikia kwenye mistari ya Biblia unayosoma kila mara. Utakapoomba kwa Mungu kuwa kwa nini umekwama katika ujenzi, Mungu atakujibu kwa kutumia neno kwa kukupa mistari iliyoko kwenye Biblia kwa sababu imani na mbinu yako inajengeka hapo. Ukikosea hapo (kwenye misingi) utapata wakati mgumu sana la sivyo uombe kwa kunena kwa lugha ili Roho Mtakatifu akusaidie kuomba (Warumi 8:26). Pia Roho Mtakatifu anaweza akakupa neno ili ujue mahali pa kukanyaga.

Kwa hiyo Mungu anapokupeleka katika eneo fulani anajua unatakiwa kukaa hapo kwa muda gani sawa na vile alivyowaambia wana wa Israeli kuwa watakapofika Babeli wajenge kwa sababu watakaa muda mrefu kwa sababu hakuwa na mpango wa kuwaondoa haraka (Yeremia 29).

Mungu akishakupa uhamisho atakuambia na la kufanya, mojawapo ni kukuambia ujenge nyumba yako ili ukae kwani sio mpango wa Mungu ukae kwenye nyumba ya kupanga.

HATUA YA NNE

4. OMBA MUNGU AKUPE KUTAMBUA MASHARTI YA KIROHO YALIYOPO KWENYE ARDHI UNAYOKUSUDIA KUJENGA AU UNAYOJENGA JUU YAKE

 

Ukisoma tena ile Kumbukumbu la Torati 8:7, 11-12 utaona cha msingi kukumbuka ni kuwa kuna suala la kufahamu masharti ya kiroho ya ardhi hiyo unayotaka kujengea au ya yule mtu anayetaka kujenga. Katika kumiliki kuna umiliki wa kisheria wa kiroho kwanza kabla haujawa umiliki wa kawaida.

 

Sheria za kiroho za ardhi zina nguvu kuliko sheria za kimwili za ardhi.

Maana yake unaweza ukahalalishwa kwa sheria za kimwili kumiliki ardhi, sheria za kiroho zikakunyima uhalali. Na sheria za kiroho zikikunyima nafasi huwezi ukakata rufaa kule sheria za kimwili zinapowekwa lazima uende kwa aliyeweka sheria za kiroho.

Sasa kwenye mistari hiyo hapo juu, Wanaisraeli walipewa agano zito sana ambalo Mungu alifunga na Ibrahimu, Isaka na Yakobo. Hawakupewa ardhi tu kwanza bali Mungu alichukua kwanza ile ardhi ikawa ya kwake kisheria. Ndio maana Biblia inasema na wao wasipokaa vizuri kule, walioko pale na wao wataondolewa kwa sababu hawajakaa sawasawa na sheria na taratibu alizojiwekea Mungu ili wapate kuenenda (ardhi itawatapika) kwa hiyo walioko pale wanatakiwa wafuate sheria na taratibu zote za Mungu.

Ishmaeli alibarikiwa na Mungu kwa sababu ni mtoto aliyetoka katika viuno vya Ibrahimu lakini alibarikiwa nje ya agano. Wakati Mungu anamwambia Ibrahimu, Ishmaeli alikuwa ameshazaliwa na Ibrahimu akajitetea kuwa Mungu ambariki Ishmaeli kwa sababu Ibrahimu na Sara wanaona hali zao haziruhusu wao kupata mtoto hata kwa mwaka unaofuata.

Ndipo Mungu akamwambia kumbariki Ishmaeli atambariki, lakini agano lake atalifanya imara na Isaka. Kwa hiyo inamaanisha kuna baraka ndani ya agano na kuna baraka nje ya agano. Kitu kimojawapo ambacho kipo ndani ya agano ni umiliki wa ardhi ambayo Mungu aliyeweka agano, anawamilikisha watu anaotaka wabarikiwe kuliko wengine, kihalali.

Ishmaeli na uzao wake walibarikiwa lakini hawakupewa ardhi ya Ibrahimu, na Isaka na Yakobo. Wakati Ibrahimu alipokufa na anazikwa, walikuwepo wake zake rasmi wawili na masuria zake. Mke wa kwanza rasmi ni Sara na wa pili baada ya Sara kufa aliitwa Ketura na alikuwa na watoto watano (Mwanzo 25:1-6).

Katika mgawo Isaka alipewa ardhi, Ishmaeli hakupewa hata watoto wa Ketura hawakupewa. Baada ya Ibrahimu kufa watoto wa Hajiri walielekea eneo tofauti na pale walipokuwepo mwanzoni. Haki mojawapo ya mwananchi wa nchi fulani ni juu ya umiliki wa ardhi, wageni hawawezi wakamiliki ardhi kirahisi rahisi. Ardhi ni sehemu ya baraka katika nchi husika na katika ulimwengu wa roho ni vivyo hivyo. Wale ambao Mungu amewakusudia hao ndio wa muhimu kumiliki eneo hilo kuliko wanaokuja.

 

Wana wa Israeli wakati wanaingia katika nchi ya Kanaani walikuwa chini ya sheria ya kumiliki na kukaa kwenye ardhi ile. Watu wengi sana wanashindwa kumiliki au wanashindwa kujenga nyumba nzuri kwenye ardhi ile kwa ubora unaotakiwa kwa sababu ya kukiuka masharti ya kiroho yaliyoko kwenye ardhi.

Yoshua 6:26 “Naye Yoshua akawaapisha kiapo wakati ule, akasema, Na alaaniwe mbele za BWANA mtu yule atakayeinuka na kuujenga tena mji huu wa Yeriko; ataweka msingi wake kwa kufiliwa na mzaliwa wa kwanza wake, tena atayasimamisha malango yake kwa kufiliwa na mtoto wake mwanamume aliye mdogo.”

1 Wafalme 16:34 “Katika siku zake, Hieli Mbetheli akajenga Yeriko; akatia misingi yake kwa kufiwa na Abiramu mzaliwa wake wa kwanza, na kuyaweka malango yake kwa kufiwa na mwana wake mdogo Segubu; sawasawa na neno la BWANA alilolinena kwa Yoshua mwana wa Nuni.”

Ukipewa huu mstari kwa ajili ya wanaoshindwa kujenga nyumba au kushindwa kumiliki ardhi ujue kwenye msingi na malango kuna kiapo cha laana kinachotakiwa kishughulikiwe kwanza. Sasa kwa sababu Roho Mtakatifu yuko ndani yako atakupa uzito ndani ya moyo wako muda ambao unataka kujenga hapo ili uingie katika maombi.

USHUHUDA

Mtu mmoja alikuwa anajenga nyumba yake na ilifika hatua nzuri sana, ilifika mahali hasogei kabisa kwa sababu pesa iliisha kabisa hadi ndoa yao iliingia mgogoro na hawakujua kitu cha kufanya. Nikiwa kwenye mkoa wao wakanieleza shida yao na wakataka niende kwenye hilo eneo na tulipoenda kwenye eneo hilo tulipoingia getini wakauliza sasa tutaanzia wapi, nikawaambia wakae pembeni kwanza ili nikaombe.

Nikazunguka na kuingia ndani na nikaanza kuomba kumwuliza Mungu kwa nini wale watu wamekwama kwenye ujenzi huo? Ghafla huo mstari ukaja na nikamwita mwenye nyumba kuwa anioneshe mahali walipokuwa wanaingilia kwa gari au miguu kabla hawajajenga ule ukuta. Tulipofika pale nikawaambia pale ndipo penye lango na kuna kitu kipo pale na kinapambana na wao, kwa hiyo tukaombe.

Ndipo tukashikana mikono tukaomba kuvunja laana katika lango lile na kinazuia wale watu kujenga. Wakati tunaomba Mungu akanioneshea mifupa, nikafungua macho na kuwauliza kuwa wakati wanachimba msingi wa ukuta huo walikuta mifupa ya watu? Wakasema ndio.

Wakanionyeshea mahali hapo tukaomba hapo, wakamalizia kujenga nyumba yao na sasa wanakaa kwenye hiyo nyumba yao. Hivi ni vitu halisi na usipojua unaombaje utasumbuka sana. Kiapo cha laana hakikuachiliwa kwenye eneo lote la nyumba hiyo bali kiliachiliwa kwenye misingi tu na kwenye lango. Lazima ujue kila kiwanja kina misingi na kina mlango na isimfungulie katika ulimwengu wa roho kila mtu anayeingia hapo.

Mungu akupe kuona masharti yaliyoko mahali hapo. Kwa mfano unapewa Mwanzo 28 : 10 - 20, Hapa kuna habari za Yakobo kulala katika eneo linaloitwa Luzu baadaye akapaita Betheli baada ya kugundua ya kwamba pale ni malango ya mbinguni kwa kuona kwenye ndoto, malaika wakipanda na kushuka. Halafu Mungu akajifunua na kusema nchi au ardhi alipolala Yakobo, ina umiliki wa kiroho (sio ya kawaida) na atampa yeye sawasawa na agano la Mungu na Ibrahimu na Isaka.

Ukipewa mistari ya namna hiyo na haisemi kitu cha kujenga pale inamaanisha Mungu anajaribu kusema ardhi ile ina madhabahu ya Kimungu na inamilikiwa na Mungu kimkataba/kiagano. Iwe ni Mungu huyu tunayemwabudu katika Kristo Yesu au miungu mingine ila ardhi tayari ilionesha ina madhabahu. Lazima mtu ajue pale kuna mlango wa kiroho na haitakiwi kujenga tu.

USHUHUDA

Tulikutana na mchawi mmoja kwenye mkoa mmoja alitueleza anavyofanya akiwa chumbani kwake. Kuwa alikuwa anapiga filimbi, ardhi inapasuka halafu anapotelea huko ili aende kuzimu (ninyi hapo mtafikiri kuwa yupo ndani kumbe ameshaondoka). Sasa alipotumwa kwenye semina yetu kuja kuloga, alikamatwa na Yesu Kristo na akaishia kuokoka na sasa ni mchungaji.

 

Alitusimulia vitu hivyo lakini kwenye Biblia vitu hivi vipo. Na Yakobo anasema kuwa kumbe pale ni nyumba ya Mungu (mahali Mungu ameamua kukaa na hana mpango wa kuondoka) na pia ni lango la mbinguni. Sasa kama ni Mungu wa kwako na ndio anamiliki hilo eneo halafu wewe ndio unatafuta labda utumie hirizi pale lazima uumie.

 

Marko 5 : 1 - 17 inazungumza habari za Yesu kwenda katika mji wa Wagerasi na kumkuta yule anayekaa makaburini, akamfungua na akapona. Yule mtu alipona baada ya kuhakikisha kwamba nguruwe wameenda kwenye ziwa yule mtu akapona. Wale wafugaji wa nguruwe wakakimbia kwenda kwenye kijiji chao na kueleza habari ya mambo yaliyotokea na kijiji kizima kikaenda pale wakakuta yule mtu miguu pa Yesu na ni mzima kabisa.

Hofu ikawaingia watu wote sasa wakamwomba Yesu aondoke katika mipaka yao; hawana shida na Yesu anayekuja kwenye mipaka yao bali wana shida na Yesu anayebaki kwenye mipaka yao.

Lile neno mipaka lina maana kubwa sana ndio maana hata yale mapepo yaliyojiita jeshi yaliomba asiwaondoe kwenye lile eneo walijua katika ulimwengu wa roho Yesu ana sheria kubwa ambayo inaweza ikawaondoa mapepo kwenye eneo lile.

Yesu naye alijua utaratibu na sheria ya kwamba yale mapepo hayakuingia vivi hivi, lazima kuna chanzo iwe ni ardhi ya pale au wenyeji wa pale ndio walitoa mipaka yao kwa nguvu za giza. Yesu akatii ile shuruti na akaondoka katika mipaka yao. Na alipofika ng'ambo ya pale kuna wengine walikuwa wanamsubiri ili awahudumie.

Wewe unanunua kiwanja kwenye eneo fulani ambapo mipaka yake ipo chini ya himaya ya mungu mwingine halafu unafika pale na Yesu wako bila kushugulikia sheria itakayoondoa mapepo hapo halafu ukabaki na sheria inayosema Yesu akifika aondoke katika mipaka hiyo.

Mwingine ananunua kiwanja halafu anawaambia watu wa nyumbani kwake na kuwaambia waende pale kumshukuru na wanafika na kuomba kuweka wakfu kwa Mungu, siku inayofuata mwenye kiwanja anakuja na kusema amebadilisha mpango, uchukue hela yako.

Saa nyingine unapanga nyumba sehemu halafu unaanza kumshukuru Mungu na kumkaribisha Yesu akae mahali hapo. Hujui misingi na mipaka ya hiyo nyumba angalia baada ya mwezi kidogo wakiona hawana namna ya kukufukuza unapandishiwa kodi kubwa kabisa. Halafu unatishiwa kuwa usipolipa ndani muda huo unafukuzwa lakini kwa wengine hazungumzi kitu chochote nawe unabaki kujiuliza.

Shida yako ni kwamba umemkaribisha Yesu; hawana shida na wewe bali na Yesu uliyemleta. Sasa hawawezi kumfukuza Yesu bila wewe kwa hiyo na wewe lazima uondoke tu ili na Yesu wako aondoke. Iko sheria iliyoko juu ya sheria ndio maana kuna mahakama ya rufaa yaani kuna mtu anaweza akapangua hukumu iliyowekwa.

 

Ukisoma Ezekieli 45:1,4 utaona neno patakatifu. Patakatifu maana yake ni eneo lililotengwa kwa ajili ya Mungu. Kazi yake ni mahali watajenga makuhani, watajenga pa kufanyia ibada yaani patakatifu pa patakatifu.

Unganisha na Ezekieli 48:8, 10, 14 “Na mpakani mwa Yuda, toka upande wa mashariki hata upande wa magharibi, yatakuwapo matoleo mtakayotoa, upana wake mianzi ishirini na tano elfu, na urefu wake sawasawa na moja la mafungu hayo, toka upande wa mashariki hata upande wa magharibi; na mahali patakatifu ni katikati yake. Matoleo hayo matakatifu yatakuwa kwa watu hawa, kwa makuhani; upande wa kaskazini urefu wake ishirini na tano elfu, na upande wa magharibi upana wake elfu kumi, na upande wa mashariki upana wake elfu kumi, na upande wa kusini urefu wake ishirini na tano elfu; na mahali patakatifu pa BWANA patakuwa katikati yake. Wala hawatauza sehemu yake, wala kuibadili, wala hawatawapa wengine malimbuko ya nchi; maana ni matakatifu kwa Bwana.”

Ukisoma mistari yote ya Ezekieli 48:8 - 14 utapata maelezo mazuri zaidi. Hapo utaona ardhi imezuiwa kuuzwa kisheria katika ulimwengu wa roho halafu wewe unanunua bila kujua masharti yake lazima utapoteza hela yako bure. Aliyezuia kuuza ni Mungu au mungu anayemiliki mahali hapo.

Kama eneo limeuzwa kwa miungu na huna namna ya kuyabandua hayo mapepo mahali hapo katika mapatano ya namna hiyo kwa kufanya shughuli zao na kutolewa sadaka ujue hilo ni zuio katika ulimwengu wa roho.

Ukianza kuomba Mungu atakupa mstari kama huo ili ujue kuna zuio katika ulimwengu wa roho na ametaka kujua Mungu anataka ulimiliki la sivyo utapata shida sana.

USHUHUDA

Mtu mmoja alipata eneo la kujengea nyumba yake na mahali alipopata ni eneo la mlima. Sasa alipoanza kujenga mafundi wanajenga vizuri kabisa lakini sehemu iliyojengwa kesho yake wanakuta imebomolewa na hali hiyo ikatokea siku kadhaa. Ndipo wakaenda kwa wenyeji kujua labda kuna watu sio wazuri na wanawafanyia fujo.

Wenyeji wakasema hakuna anayewafanyia fujo bali ule mlima ni wa miungu, hautolewi vivi hivi una masharti. Kama mtu anataka kuchukua lazima mapatano ya amani yawepo kwa kutoa sadaka.

Sasa yule mtu akasema yeye ni Mkristo kwa hiyo hawezi akatoa hiyo sadaka. Wale wenyeji wakasema sio lazima yeye atoe bali awape wao hiyo pesa halafu wao watatoa. Akakubali na kuwapa hela ya sadaka hiyo. Hao wenyeji wakatafuta ng'ombe na kufanya taratibu zingine za kwao wakatoa sadaka ili miungu ya ule mlima imkubalie yule mtu kujenga.

Baada ya kumaliza wakampa taarifa yule ndugu kuwa miungu imekubali sadaka yake sasa anaweza kuendelea kujenga. Akapeleka tena mafundi wakajenga kuanzia siku ya kwanza mpaka alipomaliza ule ujenzi, nyumba haikubomoka. Lakini baada ya pale aliugua. Sasa utajiuliza kwanini aliugua? Pia alifikilisika kabisa. Wakati namwombea Mungu akanipa hii mistari nikapata ufahamu ndipo nikaanza kumhoji maswali akanieleza kila kitu. Nilipaswa kupata ufahamu wa ki-Mungu ili kumsaidia hapo.

Watu wengine walijenga kabla hawajaokoka au wengine hawajajenga kabisa ingawa wana viwanja, au wanaanza kujenga ila hawamalizi au wanajenga ila hawakai ndani yake. Sasa kuna haja ya kufuatilia hili somo kwa mfululizo unaofuata ili tuone kwa undani namna ya kupata msaada wa Mungu kukuokoa.

HATUA YA TANO

5. MUULIZE ALIYEHITAJI KUOMBEWA IKIWA AMEWAHI KUTAFUTA KUPATANISHWA KIROHO NA KUFUATA MASHARTI YALIYOPO KATIKA ARDHI ANAYOJENGA

Ukisoma 2 Wafalme 17:24–29 utaona mfalme wa Ashuru alipoenda kupambana na mfalme wa Israeli. Na akashambulia eneo la Samaria na alishinda. Kwa hiyo alichofanya aliwahamisha wa Israeli walikuwa kwenye mji wa Samaria na kuwapeleka kama mateka alikowapeleka. Na badala yake aliwaleta watu wengine ambao wametajwa ya kwamba ni watu kutoka Babeli, na Kutha, na Ava, na Hamathi, na Sefarvaimu na kuwaweka kwenye Mji wa Samaria badala ya wana wa Israeli.

Biblia kwenye mistari hiyo inasema Mungu wa nchi, maana yake ni Mungu anayemiliki ardhi yenye mipaka halali (maana nchi ni ardhi yenye mipaka halali). Ni Mungu mwenye umiliki kiroho juu ya hilo eneo wanalokaa na ana watumishi wake wanaojua taratibu na sheria za kiroho juu za hiyo ardhi wanaoitwa makuhani.

Na ndiyo maana mfalme aliagiza makuhani hao wakaletwe na kupelekwa kukaa kule Samaria na kuweza kuwaeleza wenyeji walioshindwa kukaa kule kawaida ya Mungu wa nchi ile ili wasije kumalizwa na simba. Maana hawa watu walikuwa hawamwabudu huyu Mungu lakini walilazimika kupatana naye, wafuatane masharti yake juu ya ardhiili wakae salama.

 

Sasa basi ile kwamba mtu amehama basi haina maana Mungu wake amehama. Na ndiyo maana lazima uwe mwangalifu kuuliza kwanza juu ya kiwanja unachonunua je huyo mtu alikuwa nani au ni nani aliyekaa kabla yako kwenye hiyo nyumba ya kupanga. Na hii ni kwa sababu wengine wanapokuja kukaa huwa wanakuja na miungu yao na kuikabidhi yale maeneo na wanapohama hawahami na miungu yao wanaiacha hapo hapo na mtu mwingine atakayekuja kumiliki hilo eneo kama mgeni atakutana na masharti ambayo yanatoka kwa mungu mwingine ambaye si wa kwake. Na hampi kibali cha kuendelea kukaa kwa amani kwenye eneo hilo bila kujua masharti na kuyatimiza.

Kwa hiyo unapofika mahali kwa kukabidhi ardhi kwa miungu mingine halafu roho yako na mwili wako umeukabidhi kwa Mungu aliye hai ni kujitafutia ugomvi kwenye hilo eneo unalokwenda kulala na kujenga hapo na huo ugomvi hutaweza kujua namna hata ya kuwa refa. Usitegemee utalala vizuri kwa sababu hiyo miungu lazima itapigana tu na Mungu aliye hai na ikipigana ni lazima tu utapata shida. Na ndiyo maana watu wengi sana ukiwauliza swali la namna hii au watakufika au hawatakujibu au hawatakujibu vizuri. Lakini ukikaa vizuri na Roho Mtakataifu atakupa ufahamu juu ya eneo hilo.

HATUA YA SITA

6. OMBA TOBA KWA MUNGU KWA AJILI YA MAENEO YAFUATAYO:-

KWA KUVUNJA NA KUTOFUATA MASHARTI YA MUNGU YANAYOHUSU ARDHI INAYOTUMIKA KUJENGA. NA HII NI PAMOJA NA KUCHANGANYA MIUNGU — KWA KILICHO SABABISHA SHETANI AKAPATA NAFASI YA KUMILIKI ENEO NA KUWEKA MASHARTI YAKE.

Ukisoma Danieli 9:16 na Maombolezo 5:7 utaona hili ni suala la kisheria la ki-Biblia la msingi sana. Wazee watu wakifanya dhambi sisi hatuchukui dhambi zao bali tunachukua maovu yao yanayotokana na dhambi walizofanya. Kwa hiyo unatubu kwa ajili ya dhambi zako, bali huwezi kutubu kwa ajili ya dhambi za baba au babu zako. Bali unatubu kwa ajili ya uovu wa baba au babu zako.

Kwa mfano Malaki 1:3–4 Anazungumza juu ya watu wawili hapa Esau na Edomu. Sasa ngoja kwanza tuwajue hawa walikuwa ni watu wa namna gani, tusome kile kitabu cha Mwanzo 36:40,43 Kwa hiyo Biblia inapozungumza kwenye Malaki inasema “nimemchukia Esau na kwa sababu hiyo mahali pale pamekuwa ukiwa na nimepazuia pasijengwe na sehemu yake nimewapa mbweha wa nyikani, nimemzuia asijenge”.

Sasa mtoto wake Edomu anasema pamoja na kwamba tumepondwapondwa na hali zetu za kimaisha sina shida tutajenga. Ni mtoto akisema hayo mahali ambapo baba yake alishindwa kupajenga baada ya kubomolewa.

 

Na Mungu anasema wakijenga atabomoa. Kosa la baba aliyekutangulia hapo lakini sasa baba amekufa hajajenga maana alichojenga kilibomoka. Sasa kiwanja kakuachia na wewe unataka kujenga bila kujua kilichosababisha kubomolewa kwa kile alichojenga. Pamoja na kiwango kidogo cha pesa ulichonacho ukishajenga Mungu anakuja kubomoa. Na ndiyo maana wako wengi tu walioachiwa viwanja na mashamba na baba zao lakini wameshindwa kujenga. Au wana nyumba ambazo wameshindwa kuzimalizia ambazo wazazi wao walianza kujenga na kuishia katikati au walijenga zikabomoka.

Na hii yote ni kwamba bila toba huwezi kujenga. Hapawezi kujengeka na si kwamba shetani anazuia bali ni Mungu anayezuia si kwa ajili ya ajili yako bali kwa ajili ya baba zako.

HATUA YA SABA

7. OMBA MUNGU AONDOE MAZINGIRA YA UKIWA ILI ZUIO LA KUJENGA LIONDOKE NA MADHARA YAKE KWAKO/AU KWAKE YEYE UNAYEMUOMBEA YAONDOKE/YAKUACHIE/YAMUACHIE UNAYE MUOMBEA

Ukisoma Ezekiel 35:9 Kwa hiyo tafsiri moja ya ukiwa ni watu kutokukaa kwenye hilo eneo lenye ukiwa. Ukiwa unaondoa watu wasiweze kukaa hapo.

Pia ukisoma Isaya 5:9 utaona ya kwamba kule kwenye Ezekeli tumeona ya kwamba Mji hautakuwa na watu. Na hapa kwenye Isaya imelenga moja kwa moja kwa watu waliokwisha maliza kujenga nyumba na nyumba zao ni nzuri lakini hazina watu. Ukiwa unazuia na kuondoa mpaka wapangaji na hata watu wa kukodisha.

Lakini pia Ezekieli 33:28 inasema Eneo lenye ukiwa hata mtaani unaweza usione watu, hawalitembelei wala kwenda eneo hilo.

Na ukisoma 2 Samweli 13:20 utaona ya kwamba Tamari alikaa kimaombolezo na uchungu uliomfanya awe mzito kutoka ndani ili kufanya kazi nje na kujishughulisha na mambo mengine. Ukiwa huwa unakufurahisha kukaa ndani hata kama huna kazi. Ukiwa unakuhalalisha kutokufanya kazi hata kutokutoka nje.

Kule kwenye Malaki 1:4 tulikosoma utaona ya kwamba ukiwa unazuia ujenzi. Ukiwa aliopewa Esau ulizuia ujenzi. Na ndio maana Edomu alipotaka kujenga ukiwa ulitoa uhalali wa kubomoa kilichojengwa kwa sababu kimejengwa wakati kuna zuio. Na kile kitabu cha Amosi 6:11 kinasema Ukiwa unasababisha na kutegeneza mazingira ya nyumba kubomoka na kupigwa na ufa ili isikaliwe kabisa.

 

Hata ukiongezea kusoma Yeremia 51:26,29 utaona ya kwamba kama unajenga nyumba na kunakuwa na jiwe na pembeni au lile la msingi Biblia inasema utazuiwa. Kutakuwa nakizuizi fulani. Unaweza kuwa na kiwanja na kuchimba mitaro kabisa lakini nyumba yako itakwamia kwenye msingi. Na hii ndiyo gharama ya ukiwa.

Na ukimalizia kusoma Ezekieli 15:8 kwa hatua hii utaona ikisema kwa maana nyingine anasema “Nami nitaifanya ardhi yenye mipaka halali kuwa ukiwa” kwa hiyo ukiwa ni matokeo ya kukosa. Na ndiyo maana baada ya kuomba toba cha msingi kinachofuata ni KUOMBA MUNGU AONDOE ZUIO KWA SABABU KINACHOZUIA NI UKIWA

HATUA YA NANE

8. VUNJA NA ONDOA LAANA ILIYOPO KATIKA ARDHI YA ENEO LA UJENZI

Hii itakusaidia sana kama ulipokuwa ukiomba Mungu alikupa mstari unaofanana kwa na ule wa Yoshua aliposema ataachilia laana kwa mtu yeyote atakayejenga Yeriko, atakayejenga malango na kuta basi watoto wake watakufa wa kwanza na wa mwisho.

Ukisoma Yoshua 6:26 na hata ule wa kitabu cha 1 Wafalme 16:34 kuwa haya mambo yalitokea sawasawa na jinsi ambavyo Yoshua alisema. Kwa hiyo Mungu anapokupa mstari wa namna hii maana yake shughulika na laana iliyopo vunja kwa Damu ya Yesu.

HATUA YA TISA

9. KEMEA ILI VIONDOKE VYOTE VILIVYOKAA KWENYE ENEO UNALOLIOMBEA LILILOSHINDIKANA KUJENGWA AU HALIKALIKI HATA BAADA YA KUWA UMEKWISHA MALIZA UJENZI

Kitabu cha Isaya 13:19–22 utaona ya kwamba ukiwa ukishuka mahali si tu kwamba unazuia watu wasikae bali unaweka zuio watu wasijenge, unaweka zuio waliojenga zibomoke na unaweka zuio kwa wale waliokamilisha nyumba zisikalike lakini pia wale walioamua kubaki kupoteza nguvu za kufanya shughuli mbalimbali wanakuwa mjini lakini mji(nchi) umejaa ukiwa.

Na maandiko yanasema kwamba ukiwa ukiingia mahali ni kama vile Mungu anakuwa anaswaga hivi vitu yaani kuna kibali kinatolewa, linawekwa zuio na si tu zuio lakini kinawekwa kitu kingine cha kusaidia, na maandiko yanasema “hayawani wakali wa nyikani” Isaya 13:21a, ili ukitaka kwenda kujenga wapambane na wewe. Na Biblia inazidi kusema “na nyumba zao zitajaa bundi; mbuni watakaa huko; na majini watacheza huko” Isaya 13:21b.

Kwa hiyo ukiona nyumba haijakaliwa muda mrefu unajua sasa kitu cha kufanya kwa sababu yawezekana kuna majini yamewahi huko ndani. Kwa mfano unapoamua kununua gofu au nyumba ambayo haijaisha usije ukafikiri liko/iko yenyewe tu.

HATUA YA KUMI

10.OMBA MUNGU AKUJULISHE IKIWA UKIWA UMEONDOLEWA NA WAKAAJI HAO WABAYA NA WAMESHALIACHIA ENEO HILO

Hii inamaanisha umeshafanya maombi sasa unataka kujua ya kwamba ukiwa umeondoka. Kwanini basi unataka kujua hili? Kwa sababu ukiwa ni zuio na ni zuio linalotumia kuzia kitu fulani na kumwambia yule mtu aliyewekewa zuio apate kufanya matengenezo.

Sasa si kila mahali kwenye tatizo la ardhi Mungu anatumia ukiwa kama zuio. Maana inategemea na hii ni kutokana na mstari nilioanza nao. Kwa hiyo ukitaka kujenga kwenye kiwanja ambacho kina zuio ni lazima kwanza uweze kuondoa zuio ili uweze kuendelea, kwa sababu zuio liko kisheria.

Ukisoma Yeremia 4:27–28 Biblia inasema Mungu atakupa ndani yako maombi ya kimaombolezo. Kuna mzigo fulani utakuja ndani yako na ukiwa unakuja utakuja na kitu cha maombolezo na maombolezo hayo yatakusukuma kuomba. Hayatakusukuma kukaa ndani bila kufanya kitu.

USHUHUDA

Tulienda mahali fulani kwenye eneo na tulikuwa tukitafuta kujenga kitu cha huduma kwenye mkoa mmoja na tukapewa maeneo kama matatu manne hivi kuchagua na tukachagua eneo moja ambalo lilikuwa kama msitu lakini lipo karibu na mjini na tulishangaa sana kwamba watu hawajengi. Na sisi tukasema tunalitaka hilo eneo, wahusika wakatuambia hata michoro haijachorwa na hata kupimwa halijapimwa lakini lipo mjini. Tukasema sisi tunalitaka na tuko tayari kulipia gharama za awali za mchoro. Wakatukubalia na tukalipa zilizokuwa halali wakachora na kuweka na plan ya mji kwenye lile eneo.

Tukaitwa na kwenda kwenye lile eneo na tukafanya kazi kama ninayokufundisha hapa na tulipozunguka kwenye lile eneo tukagundua kuna madhabahu ya miungu mingine kwenye kichuguu. Na kila baada ya muda alikuwa akitokeza nyoka mkubwa kwenye kile kichuguu na wenyeji wa lile eneo wanakimbia na kuanza kumchezea na kumwimbia. Na tukajiuliza sijui wanajuaje kuwa yule nyoka katoka nje. Lakini alikuwa akishatoka tu wao wanakuja kumwimbia na kumchezea. Watu waliokuwa wakisafisha pale wakataka kumuua wenyeji wakasema mkimuua tutaharibu mvua.

Wakatupigia simu na kutueleza tukawaambia sasa ilikuwaje wakasema wenyeji walimwimbia na kumchezea mpaka alipoona kafurahi alirudi tena kwenye shimo. Sasa kumbuka ni kiwanja cha kwetu. Na wale wasafishaji wakatuuliza wafanyeje sasa tukawaambia hilo watuachie na tukajikusanya baadhi ya waombaji na kwenda pale na tukafanya baadhi ya vitu tunavyofanyaga halafu tukamnyamazisha yule nyoka kule kule shimoni na kuvunja na ile madhabahu na kufungua lile eneo kwa sababu yule nyoka ndiye aliyeweka zuio. Tulipovunja namna hiyo baada ya mwaka watu walipakimbilia na kujaa hata kujenga. Kwa hiyo tulipopangua zuio na majirani wakapata msaada.

HATAU YA KUMI NA MOJA

11. WEKA WAKFU KWA MUNGU HILO ENEO/MKABIDHI MUNGU KWA MAOMBI HILO ENEO

Inawezekana kabisa umemwomba Mungu na ndiye aliyekupa hilo eneo lakini bado anataka uweze kumkabidhi yeye kwa njia ya maombi pia. Mwambie Mungu nakupa ili eneo ni la kwako lifunike kwa damu yako, lilinde na kulitumia jinsi unavyotaka. Ukifanya namna hii na kuwa na nidhamu ya namna hii kwenye eneo hilo ambalo unataka kujenga kila ukikanyaga na kusema maneno hayo ya kumkabidhi Mungu ndani yako Mungu anakupa plan (mpango).

2 Mambo ya Nyakati 6:12–42 Biblia inasema Sulemani alipokwisha kumaliza kujenga nyumba ya Bwana na nyumba yake mwenyewe sawasawa na yote yaliyoingia ndani mwake moyoni mwake kuyafanya. Sulemani aliwekewa moyoni namna ya kujenga nyumba ya Bwana na namna ya kujenga nyumba yake. Kwa hiyo unapoweka wakfu usiweke wakfu kijumla jumla bali weka wakfu ardhi, mipaka na kiwanja, weka wakfu misingi ya kiwanja, weka wakfu malango ya kiwanja, ramani utakayochora mahali hapo.

 

HATUA YA KUMI NA MBILI

12. VISEMESHE ARDHI NA MBINGU VISIKWAMISHE UENDELEZAJI WA UJENZI NA UTUMIAJI WA KILICHOJENGWA

Kumbukumbu ya Torati 32:1 “Sikilizeni, enyi mbingu, nami nitanena; Na nchi isikie maneno ya kinywa changu.” Nchi au ardhi inaweza kusikia. Kwa hiyo ni vizuri kuitangazia kwamba zuio limeondoka. Kwa hiyo ardhi ijue kwamba ardhi hiyo sasa ni mali ya fulani kihalali katika ulimwengu wa roho. Au kama ni wewe mwenyewe unaiombea hiyo ardhi jifunze kuisemesha ardhi kuwa ni mali yako kwamba isijaribu kukupinga bali yenyewe ni mali yako ambayo Mungu amekupa kwa sababu umesha pita hatua zile nyingine zote na kukemea hata yake majini yaliyokuwa yakikaa humo na kuwa umeshaiweka wakfu kwa Mungu na Mungu ameshatamalaki hapo.

Ukishasemesha namna hiyo ardhi inasikia na mbingu inasikia. Na Biblia inasema Mungu anapokuja mahali anaita nchi na mbingu na vitu vyote vinasimama kwa pamoja. Maana yake vinategemeana. Na ndiyo maana ukisoma kwenye Biblia utakuta ikisema mbingu kufunuka na mbingu kumfunukia. Sasa mbingu ikifunuka ni kwa ajili ya watu wengi lakini mbingu kumfunukia mtu ni kwa ajili ya mtu mmoja au wawili au eneo.


MUNGU AKUBARIKI SANA

MAOMBI NA MAOMBEZI

PIGA: +255762756542

WHATSAP: +255762756542

Post a Comment

0 Comments