Katika injili ya mathayo tunasoma habari za wenye ukoma kumi ambao Yesu aliwaambia wakajionyeshe kwa makuhani na walipokuwa wakiendelea huko wakapokea uponyaji. Tunasoma kuwa kati yao wote kumi waliopona ni mmoja tu aliyerudi kwa Yesu kushukuru kwa uponyaji walioupokea. Watu wengi tumekuwa wepesi kwenda mbele za Mungu na kumweleza mahitaji yetu kwa unyenyekevu na machozi lakini pale tunapopokea majibu ya maombi yetu husahau kurudi kumshukuru. Hatuna budi kujifunza kuonyesha shukrani kwa Mungu kwa yote anayoyatenda katika maisha yetu.
1. Jenga tabia ya
kuonyesha shukurani hata kama hujisikii kufanya hivyo
Shukrani huusisha moyo pamoja na kinywa. Mara nyingine moyo
unakuwa mgumu hivyo huna budi kutamka maneno ya shukrani hata kama moyo hautaki
na kwa kufana hivi utakuwa uhaihuisha moyo tena. Vyovyote vile unavyojisikia,
una wajibu wa kumshukuru Mungu kwa mengi anayokutendea .
Efeso 5:20 na
kumshukuru Mungu Baba siku zote kwa mambo yote, katika jina lake Bwana wetu
Yesu Kristo.
Kolosai 3:17 Na
kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu,
mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye.
2. Shukuru kwa mambo
madogo ya kawaida
Mazoea huleta kujisahau hasa baraka ndogo ndogo za kila
siku. Tunapaswa kumshukuru Mungu kwa mambo yote anayotutendea kila siku, kwa
ajili ya familia zetu, kwa ajili ya kanisa, marafiki n.k.
3. Mshukuru Mungu
katikati ya magumu
Mungu hatuambii tushukuru kwa sababu ya matatizo tuliyonayo
bali tumshukuru katikati ya matatizo kwa kutambua kuwa wema wake bado upo nasi
na ataonekana kututetea na kutuvusha.
4. Usiangalie
matatizo uliyonayo b ali mpango wa Mungu katika maisha yako
Ili tuweze kuyaona yale ambayo Mungu anatenda katika maisha
yetu na kuweza kumshukuru ni lazima tuone mbali, kule ambapo Mungu anatupeleka
na yale ambayo ameahidi kuyafanya na sio kuangalia hali uliyonayo sasa.
Ukilitambua hili kila wakati utakuwa mtu wa shukrani maana unajua nini Mungu
anafanya katika maisha yako.
5. Waangalie wale
ambao kwao utaona umuhimu wa baraka zako
Wakati mwingine tunashindwa kuonyesha shukrani kwa yale
tuliyonayo kwa sababu hatuoni ukubwa au umuhimu wa baraka tulizonazo. Kama unalalamika
kwasababu ya bosi wako ambaye anakusumbua
angalia jinsi watu wasio na kazi wanavyotaabika, unalalamika kwa sababu
mtoto wako amechelewa kuongea, angalia wale wasio na watoto kabisa walivyojaa
huzuni. Mshukuru Mungu kwa kile ulichonacho badala ya kulalamika na kulaumu kwa
kile ulichokosa.
6. Uwe na muda wa
kumshukuru Mungu kila siku
Wana wa israeli walikuwa na tabia ya kumshukuru Mungu kila
siku. Nasi yatupasa kuwa na tabia hii katika maisha yetu.
1 Nyakati 23:30 nao
wasimame kila asubuhi kumshukuru na kumsifu BWANA, na jioni vivyo hivyo;
7. Mshukuru Mungu
mbele za watu
Tunapomshukuru Mungu mbele ya waamini wengine tunawatia moyo
kuwa Mungu ni muweza na pia tunaliinua jina la BWANA kati ya mataifa.
Zaburi 35:18 Nitakushukuru
katika kusanyiko kubwa; Nitakusifu kati ya watu wengi.
8. Zihesabu baraka
zako
Andika yale yote Mungu anayokutendea na uwe unapitia mara
kwa mara utaona jinsi ulivyo na mambo mengi ya kumshukuru Mungu. Prayer journal
inafaa sana kwa hili ukiwa nayo
itakusaidia kuandika maombi yako na majibu yake.( ukiihitaji tuwasiliane).
9. Onyesha shukarani
kwa watu wanaokuzunguka
Onyesha shukrani kwa familia yako na marafiki zako kwa kuwa
nawe kwa nyakati zote na kwa yale wanayokutendea. Pia onyesha shukrani kwa watu
wanaofanyika msaada katika maisha yako iwe ni kazini, sokoni, kanisani,
barabarani n.k na kwa kufanya hivyo utajikuta unaonyesha shukrani zaidi kwa
yule aliyewaweka ambaye ni Mungu.
10. Toa kwa wenye
mahitaji
Unavyotoa kwa wenye uhitaji unaonyesha shukrani kwa Mungu
aliyekupatia na pia unawawezesha na wengine kumshukuru Mungu kwa ajili yako.
2 Korintho 9: 11-12 mkitajirishwa katika vitu vyote mpate kuwa na
ukarimu wote, umpatiao Mungu shukrani kwa kazi yetu. Kwa maana utumishi wa
hufuma hii hauwatimizii watakatifu riziki walizopungukuwa tu, bali huzidi sana
kuwa na faida kwa shukrani nyingi apewazo Mungu.
Tukiyafanya haya tutaweza kuwa kama yule mwenye ukoma aliyerudi kuonyesha shukrani na kuepuka kuwa kama wale tisa ambao hawakuona umuhimu wa kumshukuru Mungu aliyewaponya.
Mungu akubariki sana
maombi na maombezi
piga: +255762756542
watsap: +255762756542
0 Comments