HATUA KUMU NA MBILI (12) ZA KUOMBEA HALI YA KIROHO YA ARDHI ILI UWEZE UFANIKIWE KWENYE MAISHA.
1. PELEKA OMBI HILO KWA MUNGU
Mtu akileta
hitaji lake kwako sio kwamba hana Mungu, bali anahitaji msaada wa maombi kutoka
kwako. Sasa Mungu anaweza akakusemesha moja kwa moja wakati huyo anakuambia
hitaji lake au akakusemesha mapema kabla hajaja. Muhimu fikra zako zifikiri
kuwa hilo jambo unalipeleka kwa Mungu kwa eneo ulipokwama kimafanikio.
2. POKEA NENO LA MUNGU UNALOPEWA NA
MUNGU KWA AJILI YA HUYO ANAYEOMBA UMWOMBEE
Zaburi 107:19 - 20 “Wakamlilia BWANA katika dhiki zao,
Akawaponya na shida zao. Hulituma neno lake, huwaponya, Huwatoa katika
maangamizo yao.”
Isaya 55:11 “ndivyo litakavyokuwa neno langu,
litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi
yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma.”
Hapo utaona
kuna neno la Mungu ambalo ndani yake kuna wazo la Mungu ambalo lina mkakati wa
Mungu ambalo ndani yake kuna mvua inayotakiwa kuotesha. Ikimaanisha kila neno
linalokuja ndani yake kuna upako wake na linahakikisha linafanikiwa katika lile
lilokusudiwa.
Watu wengi
wanafikiria maombi peke yake yatawafanikisha, hapana, maombi yanabeba mahitaji
yako kwa Mungu na Mungu akitaka kukufanikisha atakupa neno. Ndio maana ni
hatari sana unapoenda kanisani, unahitaji maombi na sio neno. Au unafika kwenye
mkutano muda wote unawaza ataomba saa ngapi lakini hutaki kukaa chini ili
usikilize neno.
Yesu alisema
katika Mathayo 4:4 “Naye akajibu akasema, Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate
tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.” Usije ukabadilisha
sehemu ya neno ukaweka maombi kwa sababu maombi peke yake hayawezi
kukufanikisha. Jaribu kutafuta waombaji wazuri halafu ona na maisha yao. Nchi
inaweza ikawa na waombaji wazuri sana lakini wasipokuwa na neno la Mungu
hawatakuwa na maendeleo. Pia viongozi wasiopokea neno la Bwana katika nchi yao,
wasahau kuwa na maendeleo kabisa.
3. OMBA MUNGU AKUPE KUSIKIA MWONGOZO
WAKE KWAKO KUTOKA KWENYE NENO ULILOPEWA NA MUNGU KWA AJILI YA KUMWOMBEA HUYO
MTU AU WAKATI ULIPOJIOMBEA MWENYEWE
Warumi 10:17 “Basi imani, chanzo chake ni
kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo.” Kuna kusikia sauti ya neno, na
hiyo sauti ndiyo inakutengenezea uhakika ambao unakupa imani. Sawasawa na Waebrania 11:1 na Waebrania 11:3“Imani haiji kwa neno, bali huja kwa kusikia.”
Haijalishi
ni imani ya namna gani. Imani yako kwa mganga wa kienyeji au kwa hospitali
fulani na daktari fulani zote zilikuja kwa kusikia. Sasa ili ujue ni imani ya
namna gani, lakini lazima ujue ulisikia kwa namna gani. Kama ni imani kwa Mungu
kupitia Yesu Kristo lazima utasikia kwa kuletwa na neno lake.
Imani humpa
mtu ufahamu na kujua kwa hiyo utajua namna ya kuomba ipasavyo ili uweze kutoka
mahali ulipo. Ndio maana hiki kipengele cha tatu ni cha muhimu sana kuwa Mungu
akupe kusikia kutoka kwenye neno ulilopewa ili imani yako ijengeke na uje
ufanye nini.
Tuangalie
mfano hapa. Kumbukumbu la Torati 8:7,
11-12 “Kwa kuwa BWANA, Mungu wako, yuakuingiza katika nchi nzuri, nchi
yenye vijito vya maji, na chemchemi, na visima, vibubujikavyo katika mabonde na
milima; Jihadhari, usije ukamsahau BWANA, Mungu wako, kwa kutozishika amri
zake, na hukumu zake, na sheria zake, ninazokuamuru leo. Angalia, utakapokuwa umekula na kushiba, na kujenga nyumba nzuri na
kukaa ndani yake;”
Anapozungumzia
ujenzi na kuhusisha na ardhi inamaanisha anazungumzia kumwingiza huyo katika
nchi. Nchi maana yake ni ardhi yenye mipaka halali ya kiumiliki.
Maana yake
anampa eneo la kujenga kwa hiyo kuna suala la kumiliki ardhi kihalali kiroho na
kimwili kabla ya kujenga. Kwa mfano wale wanaojenga karibu na barabara
wasisahau kuwa barabara ina haki kuliko wao. Barabara ikiamua kupita, utaipisha
tu haijalishi umejenga nini hapo.
Katika
misingi sheria ya nchi mbalimbali, sheria ya barabara ina nguvu kuliko sheria
ya kumiliki kwako nyumba. Barabara iko tayari ikulipe ili utoke kwenye njia
hiyo na kuna muda wanajua kuwa barabara itapanuka patawekwa na eneo la akiba ya
barabara sasa nawe usijifanye mjanja ukajenga huko. Haya mambo yote yapo kwenye
Biblia ila nitakuonyesha pole pole.
Mungu
anapowaambia kuwa atawaingiza katika nchi, kabla kisheria haijawa ya kwao
kimwili, ilikuwa ya kwao kwa jinsi ya sheria kiroho.
Agano ni
sheria mama ya sheria zote. Ni sawa na katiba ambayo ni sheria juu ya wananchi
wote walioko katika mipaka hiyo ya kiutawala. Sasa kiroho kuna kitu kinaitwa
agano la Mungu au la miungu ambayo ni sheria mama inayobeba sheria ndogo ndogo
kuweko na ndani yake inakuwa na vipengele vya ardhi.
Hakuna agano
lolote lisilo na kipengele cha ardhi. Ndio maana Mungu anasema utakapokuwa
umekula na kushiba, na kujenga nyumba nzuri na kukaa ndani yake;”
Kwa hiyo
kuna suala la kujenga na siyo kujenga tu bali hata kiwango cha ujenzi huo
inapaswa iwe nzuri. Je nyumba nzuri ni ipi? Wewe unaweza ukasema hiyo nyumba ni
nzuri lakini Mungu anaona sio nzuri. Maana yake kuna kiwango fulani cha nyumba
za watu wake alizoziweka.
Si suala tu
la kujenga nyumba au barabara bali ni kwa kiwango kipi cha ubora ambacho nyumba
hiyo au barabara hiyo imejengwa? La sivyo baada ya miaka michache
imeshaharibika.
USHUHUDA
Wakati
fulani tulienda kwenye shule ya msingi ambayo mke wangu alisoma zamani.
Tulipoenda kuangalia jengo la darasa la kwanza na la pili tukakuta kilichoanza
kubomoka ni milango. Madawati yalikuwa yamebaki machache sasa. Cha ajabu
tuliona ukutana na sakafu bado vikiwa imara.
Walimu
walioko pale wakatupeleka kwenye darasa lingine ambalo ndio limemaliza miaka
miwili tangia limejengwa. Na sakafu na ukuta wake ulikuwa umeanza kutoboka
toboka. Fedha zilizotumika kujenga jengo hilo lililotimiza miaka miwili ni
kubwa sana kuliko fedha jengo la zamani.
Suala la
ubora wa jengo ni suala la kiroho kabla halijawa la kimwili. Sasa anazungumza
suala la kukaa ndani yake. Haupaswi tu kujenga bila kukaa ndani yake lazima
utumie hilo jengo vizuri.
Kwa hiyo
kuna umuhimu wa kusikia kwenye mistari ya Biblia unayosoma kila mara.
Utakapoomba kwa Mungu kuwa kwa nini umekwama katika ujenzi, Mungu atakujibu kwa
kutumia neno kwa kukupa mistari iliyoko kwenye Biblia kwa sababu imani na mbinu
yako inajengeka hapo. Ukikosea hapo (kwenye misingi) utapata wakati mgumu sana
la sivyo uombe kwa kunena kwa lugha ili Roho Mtakatifu akusaidie kuomba (Warumi
8:26). Pia Roho Mtakatifu anaweza akakupa neno ili ujue mahali pa kukanyaga.
Kwa hiyo
Mungu anapokupeleka katika eneo fulani anajua unatakiwa kukaa hapo kwa muda
gani sawa na vile alivyowaambia wana wa Israeli kuwa watakapofika Babeli
wajenge kwa sababu watakaa muda mrefu kwa sababu hakuwa na mpango wa kuwaondoa
haraka (Yeremia 29).
Mungu
akishakupa uhamisho atakuambia na la kufanya, mojawapo ni kukuambia ujenge
nyumba yako ili ukae kwani sio mpango wa Mungu ukae kwenye nyumba ya kupanga.
4. OMBA MUNGU AKUPE KUTAMBUA MASHARTI
YA KIROHO YALIYOPO KWENYE ARDHI UNAYOKUSUDIA KUJENGA AU UNAYOJENGA JUU YAKE
Ukisoma tena ile Kumbukumbu la Torati
8:7, 11-12 utaona
cha msingi kukumbuka ni kuwa kuna suala la kufahamu masharti ya kiroho ya ardhi
hiyo unayotaka kujengea au ya yule mtu anayetaka kujenga. Katika kumiliki kuna
umiliki wa kisheria wa kiroho kwanza kabla haujawa umiliki wa kawaida.
Sheria za
kiroho za ardhi zina nguvu kuliko sheria za kimwili za ardhi.
Maana yake
unaweza ukahalalishwa kwa sheria za kimwili kumiliki ardhi, sheria za kiroho
zikakunyima uhalali. Na sheria za kiroho zikikunyima nafasi huwezi ukakata
rufaa kule sheria za kimwili zinapowekwa lazima uende kwa aliyeweka sheria za
kiroho.
Sasa kwenye
mistari hiyo hapo juu, Wanaisraeli walipewa agano zito sana ambalo Mungu
alifunga na Ibrahimu, Isaka na Yakobo. Hawakupewa ardhi tu kwanza bali Mungu
alichukua kwanza ile ardhi ikawa ya kwake kisheria. Ndio maana Biblia inasema
na wao wasipokaa vizuri kule, walioko pale na wao wataondolewa kwa sababu
hawajakaa sawasawa na sheria na taratibu alizojiwekea Mungu ili wapate kuenenda
(ardhi itawatapika) kwa hiyo walioko pale wanatakiwa wafuate sheria na taratibu
zote za Mungu.
Ishmaeli
alibarikiwa na Mungu kwa sababu ni mtoto aliyetoka katika viuno vya Ibrahimu
lakini alibarikiwa nje ya agano. Wakati Mungu anamwambia Ibrahimu, Ishmaeli
alikuwa ameshazaliwa na Ibrahimu akajitetea kuwa Mungu ambariki Ishmaeli kwa
sababu Ibrahimu na Sara wanaona hali zao haziruhusu wao kupata mtoto hata kwa
mwaka unaofuata.
Ndipo Mungu
akamwambia kumbariki Ishmaeli atambariki, lakini agano lake atalifanya imara na
Isaka. Kwa hiyo inamaanisha kuna baraka ndani ya agano na kuna baraka nje ya
agano. Kitu kimojawapo ambacho kipo ndani ya agano ni umiliki wa ardhi ambayo
Mungu aliyeweka agano, anawamilikisha watu anaotaka wabarikiwe kuliko wengine,
kihalali.
Ishmaeli na
uzao wake walibarikiwa lakini hawakupewa ardhi ya Ibrahimu, na Isaka na Yakobo.
Wakati Ibrahimu alipokufa na anazikwa, walikuwepo wake zake rasmi wawili na
masuria zake. Mke wa kwanza rasmi ni Sara na wa pili baada ya Sara kufa aliitwa
Ketura na alikuwa na watoto watano
(Mwanzo 25:1-6).
Katika mgawo
Isaka alipewa ardhi, Ishmaeli hakupewa hata watoto wa Ketura hawakupewa. Baada
ya Ibrahimu kufa watoto wa Hajiri walielekea eneo tofauti na pale walipokuwepo
mwanzoni. Haki mojawapo ya mwananchi wa nchi fulani ni juu ya umiliki wa ardhi,
wageni hawawezi wakamiliki ardhi kirahisi rahisi. Ardhi ni sehemu ya baraka
katika nchi husika na katika ulimwengu wa roho ni vivyo hivyo. Wale ambao Mungu
amewakusudia hao ndio wa muhimu kumiliki eneo hilo kuliko wanaokuja.
Wana wa
Israeli wakati wanaingia katika nchi ya Kanaani walikuwa chini ya sheria ya
kumiliki na kukaa kwenye ardhi ile. Watu wengi sana wanashindwa kumiliki au
wanashindwa kujenga nyumba nzuri kwenye ardhi ile kwa ubora unaotakiwa kwa
sababu ya kukiuka masharti ya kiroho yaliyoko kwenye ardhi.
Yoshua 6:26 “Naye Yoshua akawaapisha kiapo
wakati ule, akasema, Na alaaniwe mbele za BWANA mtu yule atakayeinuka na
kuujenga tena mji huu wa Yeriko; ataweka msingi wake kwa kufiliwa na mzaliwa wa
kwanza wake, tena atayasimamisha malango yake kwa kufiliwa na mtoto wake
mwanamume aliye mdogo.”
1 Wafalme 16:34 “Katika siku zake, Hieli Mbetheli
akajenga Yeriko; akatia misingi yake kwa kufiwa na Abiramu mzaliwa wake wa
kwanza, na kuyaweka malango yake kwa kufiwa na mwana wake mdogo Segubu;
sawasawa na neno la BWANA alilolinena kwa Yoshua mwana wa Nuni.”
Ukipewa huu
mstari kwa ajili ya wanaoshindwa kujenga nyumba au kushindwa kumiliki ardhi
ujue kwenye msingi na malango kuna kiapo cha laana kinachotakiwa kishughulikiwe
kwanza. Sasa kwa sababu Roho Mtakatifu yuko ndani yako atakupa uzito ndani ya
moyo wako muda ambao unataka kujenga hapo ili uingie katika maombi.
Ndipo
tukashikana mikono tukaomba kuvunja laana katika lango lile na kinazuia wale
watu kujenga. Wakati tunaomba Mungu akanioneshea mifupa, nikafungua macho na
kuwauliza kuwa wakati wanachimba msingi wa ukuta huo walikuta mifupa ya watu?
Wakasema ndio.
Wakanionyeshea
mahali hapo tukaomba hapo, wakamalizia kujenga nyumba yao na sasa wanakaa
kwenye hiyo nyumba yao. Hivi ni vitu halisi na usipojua unaombaje utasumbuka
sana. Kiapo cha laana hakikuachiliwa kwenye eneo lote la nyumba hiyo bali
kiliachiliwa kwenye misingi tu na kwenye lango. Lazima ujue kila kiwanja kina
misingi na kina mlango na isimfungulie katika ulimwengu wa roho kila mtu anayeingia
hapo.
Mungu akupe
kuona masharti yaliyoko mahali hapo. Kwa mfano unapewa Mwanzo 28 : 10 - 20,
Hapa kuna habari za Yakobo kulala katika eneo linaloitwa Luzu baadaye akapaita
Betheli baada ya kugundua ya kwamba pale ni malango ya mbinguni kwa kuona kwenye
ndoto, malaika wakipanda na kushuka. Halafu Mungu akajifunua na kusema nchi au
ardhi alipolala Yakobo, ina umiliki wa kiroho (sio ya kawaida) na atampa yeye
sawasawa na agano la Mungu na Ibrahimu na Isaka.
Ukipewa
mistari ya namna hiyo na haisemi kitu cha kujenga pale inamaanisha Mungu
anajaribu kusema ardhi ile ina madhabahu ya Kimungu na inamilikiwa na Mungu
kimkataba/kiagano. Iwe ni Mungu huyu tunayemwabudu katika Kristo Yesu au miungu
mingine ila ardhi tayari ilionesha ina madhabahu. Lazima mtu ajue pale kuna
mlango wa kiroho na haitakiwi kujenga tu.
Marko 5 : 1 - 17 inazungumza habari za Yesu kwenda
katika mji wa Wagerasi na kumkuta yule anayekaa makaburini, akamfungua na
akapona. Yule mtu alipona baada ya kuhakikisha kwamba nguruwe wameenda kwenye
ziwa yule mtu akapona. Wale wafugaji wa nguruwe wakakimbia kwenda kwenye kijiji
chao na kueleza habari ya mambo yaliyotokea na kijiji kizima kikaenda pale
wakakuta yule mtu miguu pa Yesu na ni mzima kabisa.
Hofu
ikawaingia watu wote sasa wakamwomba Yesu aondoke katika mipaka yao; hawana
shida na Yesu anayekuja kwenye mipaka yao bali wana shida na Yesu anayebaki
kwenye mipaka yao.
Lile neno
mipaka lina maana kubwa sana ndio maana hata yale mapepo yaliyojiita jeshi
yaliomba asiwaondoe kwenye lile eneo walijua katika ulimwengu wa roho Yesu ana
sheria kubwa ambayo inaweza ikawaondoa mapepo kwenye eneo lile.
Yesu naye
alijua utaratibu na sheria ya kwamba yale mapepo hayakuingia vivi hivi, lazima
kuna chanzo iwe ni ardhi ya pale au wenyeji wa pale ndio walitoa mipaka yao kwa
nguvu za giza. Yesu akatii ile shuruti na akaondoka katika mipaka yao. Na
alipofika ng'ambo ya pale kuna wengine walikuwa wanamsubiri ili awahudumie.
Wewe
unanunua kiwanja kwenye eneo fulani ambapo mipaka yake ipo chini ya himaya ya
mungu mwingine halafu unafika pale na Yesu wako bila kushugulikia sheria itakayoondoa
mapepo hapo halafu ukabaki na sheria inayosema Yesu akifika aondoke katika
mipaka hiyo.
Mwingine
ananunua kiwanja halafu anawaambia watu wa nyumbani kwake na kuwaambia waende
pale kumshukuru na wanafika na kuomba kuweka wakfu kwa Mungu, siku inayofuata
mwenye kiwanja anakuja na kusema amebadilisha mpango, uchukue hela yako.
Saa nyingine
unapanga nyumba sehemu halafu unaanza kumshukuru Mungu na kumkaribisha Yesu
akae mahali hapo. Hujui misingi na mipaka ya hiyo nyumba angalia baada ya mwezi
kidogo wakiona hawana namna ya kukufukuza unapandishiwa kodi kubwa kabisa.
Halafu unatishiwa kuwa usipolipa ndani muda huo unafukuzwa lakini kwa wengine
hazungumzi kitu chochote nawe unabaki kujiuliza.
Shida yako
ni kwamba umemkaribisha Yesu; hawana shida na wewe bali na Yesu uliyemleta.
Sasa hawawezi kumfukuza Yesu bila wewe kwa hiyo na wewe lazima uondoke tu ili
na Yesu wako aondoke. Iko sheria iliyoko juu ya sheria ndio maana kuna mahakama
ya rufaa yaani kuna mtu anaweza akapangua hukumu iliyowekwa.
Ukisoma Ezekieli 45:1,4 utaona neno patakatifu. Patakatifu
maana yake ni eneo lililotengwa kwa ajili ya Mungu. Kazi yake ni mahali
watajenga makuhani, watajenga pa kufanyia ibada yaani patakatifu pa patakatifu.
Unganisha na Ezekieli 48:8, 10, 14 “Na mpakani mwa Yuda, toka upande wa
mashariki hata upande wa magharibi, yatakuwapo matoleo mtakayotoa, upana wake
mianzi ishirini na tano elfu, na urefu wake sawasawa na moja la mafungu hayo,
toka upande wa mashariki hata upande wa magharibi; na mahali patakatifu ni
katikati yake. Matoleo hayo matakatifu yatakuwa kwa watu hawa, kwa makuhani;
upande wa kaskazini urefu wake ishirini na tano elfu, na upande wa magharibi
upana wake elfu kumi, na upande wa mashariki upana wake elfu kumi, na upande wa
kusini urefu wake ishirini na tano elfu; na mahali patakatifu pa BWANA patakuwa
katikati yake. Wala hawatauza sehemu yake, wala kuibadili, wala hawatawapa
wengine malimbuko ya nchi; maana ni matakatifu kwa Bwana.”
Ukisoma mistari yote ya Ezekieli 48:8
- 14 utapata maelezo mazuri zaidi. Hapo
utaona ardhi imezuiwa kuuzwa kisheria katika ulimwengu wa roho halafu wewe
unanunua bila kujua masharti yake lazima utapoteza hela yako bure. Aliyezuia
kuuza ni Mungu au mungu anayemiliki mahali hapo.
Kama eneo
limeuzwa kwa miungu na huna namna ya kuyabandua hayo mapepo mahali hapo katika
mapatano ya namna hiyo kwa kufanya shughuli zao na kutolewa sadaka ujue hilo ni
zuio katika ulimwengu wa roho.
Ukianza
kuomba Mungu atakupa mstari kama huo ili ujue kuna zuio katika ulimwengu wa
roho na ametaka kujua Mungu anataka ulimiliki la sivyo utapata shida sana.
USHUHUDA
Mtu mmoja
alipata eneo la kujengea nyumba yake na mahali alipopata ni eneo la mlima. Sasa
alipoanza kujenga mafundi wanajenga vizuri kabisa lakini sehemu iliyojengwa
kesho yake wanakuta imebomolewa na hali hiyo ikatokea siku kadhaa. Ndipo
wakaenda kwa wenyeji kujua labda kuna watu sio wazuri na wanawafanyia fujo.
Wenyeji
wakasema hakuna anayewafanyia fujo bali ule mlima ni wa miungu, hautolewi vivi
hivi una masharti. Kama mtu anataka kuchukua lazima mapatano ya amani yawepo
kwa kutoa sadaka.
Sasa yule
mtu akasema yeye ni Mkristo kwa hiyo hawezi akatoa hiyo sadaka. Wale wenyeji
wakasema sio lazima yeye atoe bali awape wao hiyo pesa halafu wao watatoa.
Akakubali na kuwapa hela ya sadaka hiyo. Hao wenyeji wakatafuta ng'ombe na
kufanya taratibu zingine za kwao wakatoa sadaka ili miungu ya ule mlima
imkubalie yule mtu kujenga.
Baada ya
kumaliza wakampa taarifa yule ndugu kuwa miungu imekubali sadaka yake sasa
anaweza kuendelea kujenga. Akapeleka tena mafundi wakajenga kuanzia siku ya
kwanza mpaka alipomaliza ule ujenzi, nyumba haikubomoka. Lakini baada ya pale
aliugua. Sasa utajiuliza kwanini aliugua? Pia alifikilisika kabisa. Wakati
namwombea Mungu akanipa hii mistari nikapata ufahamu ndipo nikaanza kumhoji
maswali akanieleza kila kitu. Nilipaswa kupata ufahamu wa ki-Mungu ili
kumsaidia hapo.
Watu wengine
walijenga kabla hawajaokoka au wengine hawajajenga kabisa ingawa wana viwanja,
au wanaanza kujenga ila hawamalizi au wanajenga ila hawakai ndani yake. Sasa
kuna haja ya kufuatilia hili somo kwa mfululizo unaofuata ili tuone kwa undani
namna ya kupata msaada wa Mungu kukuokoa.
5. MUULIZE ALIYEHITAJI KUOMBEWA IKIWA
AMEWAHI KUTAFUTA KUPATANISHWA KIROHO NA KUFUATA MASHARTI YALIYOPO KATIKA ARDHI
ANAYOJENGA
Ukisoma 2 Wafalme 17:24–29 utaona mfalme wa Ashuru alipoenda
kupambana na mfalme wa Israeli. Na akashambulia eneo la Samaria na alishinda.
Kwa hiyo alichofanya aliwahamisha wa Israeli walikuwa kwenye mji wa Samaria na
kuwapeleka kama mateka alikowapeleka. Na badala yake aliwaleta watu wengine
ambao wametajwa ya kwamba ni watu kutoka Babeli, na Kutha, na Ava, na Hamathi,
na Sefarvaimu na kuwaweka kwenye Mji wa Samaria badala ya wana wa Israeli.
Biblia
kwenye mistari hiyo inasema Mungu wa nchi, maana yake ni Mungu anayemiliki
ardhi yenye mipaka halali (maana nchi ni ardhi yenye mipaka halali). Ni Mungu
mwenye umiliki kiroho juu ya hilo eneo wanalokaa na ana watumishi wake wanaojua
taratibu na sheria za kiroho juu za hiyo ardhi wanaoitwa makuhani.
Na ndiyo
maana mfalme aliagiza makuhani hao wakaletwe na kupelekwa kukaa kule Samaria na
kuweza kuwaeleza wenyeji walioshindwa kukaa kule kawaida ya Mungu wa nchi ile
ili wasije kumalizwa na simba. Maana hawa watu walikuwa hawamwabudu huyu Mungu
lakini walilazimika kupatana naye, wafuatane masharti yake juu ya ardhiili
wakae salama.
Sasa basi
ile kwamba mtu amehama basi haina maana Mungu wake amehama. Na ndiyo maana
lazima uwe mwangalifu kuuliza kwanza juu ya kiwanja unachonunua je huyo mtu
alikuwa nani au ni nani aliyekaa kabla yako kwenye hiyo nyumba ya kupanga. Na
hii ni kwa sababu wengine wanapokuja kukaa huwa wanakuja na miungu yao na
kuikabidhi yale maeneo na wanapohama hawahami na miungu yao wanaiacha hapo hapo
na mtu mwingine atakayekuja kumiliki hilo eneo kama mgeni atakutana na masharti
ambayo yanatoka kwa mungu mwingine ambaye si wa kwake. Na hampi kibali cha
kuendelea kukaa kwa amani kwenye eneo hilo bila kujua masharti na kuyatimiza.
Kwa hiyo
unapofika mahali kwa kukabidhi ardhi kwa miungu mingine halafu roho yako na
mwili wako umeukabidhi kwa Mungu aliye hai ni kujitafutia ugomvi kwenye hilo
eneo unalokwenda kulala na kujenga hapo na huo ugomvi hutaweza kujua namna hata
ya kuwa refa. Usitegemee utalala vizuri kwa sababu hiyo miungu lazima itapigana
tu na Mungu aliye hai na ikipigana ni lazima tu utapata shida. Na ndiyo maana
watu wengi sana ukiwauliza swali la namna hii au watakufika au hawatakujibu au
hawatakujibu vizuri. Lakini ukikaa vizuri na Roho Mtakataifu atakupa ufahamu
juu ya eneo hilo.
6. OMBA TOBA KWA MUNGU KWA AJILI YA
MAENEO YAFUATAYO:-
KWA KUVUNJA
NA KUTOFUATA MASHARTI YA MUNGU YANAYOHUSU ARDHI INAYOTUMIKA KUJENGA. NA HII NI
PAMOJA NA KUCHANGANYA MIUNGU — KWA KILICHO SABABISHA SHETANI AKAPATA NAFASI YA
KUMILIKI ENEO NA KUWEKA MASHARTI YAKE.
Ukisoma
Danieli 9:16 na Maombolezo 5:7 utaona hili ni suala la kisheria la ki-Biblia la
msingi sana. Wazee watu wakifanya dhambi sisi hatuchukui dhambi zao bali
tunachukua maovu yao yanayotokana na dhambi walizofanya. Kwa hiyo unatubu kwa
ajili ya dhambi zako, bali huwezi kutubu kwa ajili ya dhambi za baba au babu
zako. Bali unatubu kwa ajili ya uovu wa baba au babu zako.
Kwa mfano Malaki 1:3–4 Anazungumza juu ya watu wawili hapa
Esau na Edomu. Sasa ngoja kwanza tuwajue hawa walikuwa ni watu wa namna gani,
tusome kile kitabu cha Mwanzo 36:40,43 Kwa hiyo Biblia inapozungumza kwenye
Malaki inasema “nimemchukia Esau na kwa sababu hiyo mahali pale pamekuwa ukiwa
na nimepazuia pasijengwe na sehemu yake nimewapa mbweha wa nyikani, nimemzuia
asijenge”.
Sasa mtoto
wake Edomu anasema pamoja na kwamba tumepondwapondwa na hali zetu za kimaisha
sina shida tutajenga. Ni mtoto akisema hayo mahali ambapo baba yake alishindwa
kupajenga baada ya kubomolewa.
Na Mungu
anasema wakijenga atabomoa. Kosa la baba aliyekutangulia hapo lakini sasa baba
amekufa hajajenga maana alichojenga kilibomoka. Sasa kiwanja kakuachia na wewe
unataka kujenga bila kujua kilichosababisha kubomolewa kwa kile alichojenga.
Pamoja na kiwango kidogo cha pesa ulichonacho ukishajenga Mungu anakuja
kubomoa. Na ndiyo maana wako wengi tu walioachiwa viwanja na mashamba na baba
zao lakini wameshindwa kujenga. Au wana nyumba ambazo wameshindwa kuzimalizia
ambazo wazazi wao walianza kujenga na kuishia katikati au walijenga zikabomoka.
Na hii yote
ni kwamba bila toba huwezi kujenga. Hapawezi kujengeka na si kwamba shetani
anazuia bali ni Mungu anayezuia si kwa ajili ya ajili yako bali kwa ajili ya
baba zako.
7. OMBA MUNGU AONDOE MAZINGIRA YA
UKIWA ILI ZUIO LA KUJENGA LIONDOKE NA MADHARA YAKE KWAKO/AU KWAKE YEYE
UNAYEMUOMBEA YAONDOKE/YAKUACHIE/YAMUACHIE UNAYE MUOMBEA
Ukisoma Ezekiel 35:9 Kwa hiyo tafsiri moja ya ukiwa ni
watu kutokukaa kwenye hilo eneo lenye ukiwa. Ukiwa unaondoa watu wasiweze kukaa
hapo.
ukisoma Isaya 5:9 utaona ya kwamba kule kwenye Ezekeli
tumeona ya kwamba Mji hautakuwa na watu. Na hapa kwenye Isaya imelenga moja kwa
moja kwa watu waliokwisha maliza kujenga nyumba na nyumba zao ni nzuri lakini
hazina watu. Ukiwa unazuia na kuondoa mpaka wapangaji na hata watu wa kukodisha.
Lakini pia Ezekieli 33:28 inasema Eneo lenye ukiwa hata mtaani
unaweza usione watu, hawalitembelei wala kwenda eneo hilo.
Na ukisoma 2 Samweli 13:20 utaona ya kwamba Tamari alikaa
kimaombolezo na uchungu uliomfanya awe mzito kutoka ndani ili kufanya kazi nje
na kujishughulisha na mambo mengine. Ukiwa huwa unakufurahisha kukaa ndani hata
kama huna kazi. Ukiwa unakuhalalisha kutokufanya kazi hata kutokutoka nje.
Kule kwenye Malaki 1:4 tulikosoma utaona ya kwamba ukiwa
unazuia ujenzi. Ukiwa aliopewa Esau ulizuia ujenzi. Na ndio maana Edomu
alipotaka kujenga ukiwa ulitoa uhalali wa kubomoa kilichojengwa kwa sababu
kimejengwa wakati kuna zuio. Na kile kitabu cha Amosi 6:11 kinasema Ukiwa
unasababisha na kutegeneza mazingira ya nyumba kubomoka na kupigwa na ufa ili
isikaliwe kabisa.
Hata ukiongezea kusoma Yeremia
51:26,29 utaona ya
kwamba kama unajenga nyumba na kunakuwa na jiwe na pembeni au lile la msingi
Biblia inasema utazuiwa. Kutakuwa nakizuizi fulani. Unaweza kuwa na kiwanja na
kuchimba mitaro kabisa lakini nyumba yako itakwamia kwenye msingi. Na hii ndiyo
gharama ya ukiwa.
Na ukimalizia kusoma Ezekieli 15:8 kwa hatua hii utaona ikisema kwa
maana nyingine anasema “Nami nitaifanya ardhi yenye mipaka halali kuwa ukiwa”
kwa hiyo ukiwa ni matokeo ya kukosa. Na ndiyo maana baada ya kuomba toba cha
msingi kinachofuata ni KUOMBA MUNGU AONDOE ZUIO KWA SABABU KINACHOZUIA NI UKIWA
8. VUNJA NA ONDOA LAANA ILIYOPO
KATIKA ARDHI YA ENEO LA UJENZI
Hii
itakusaidia sana kama ulipokuwa ukiomba Mungu alikupa mstari unaofanana kwa na
ule wa Yoshua aliposema ataachilia laana kwa mtu yeyote atakayejenga Yeriko,
atakayejenga malango na kuta basi watoto wake watakufa wa kwanza na wa mwisho.
Ukisoma Yoshua 6:26 na hata ule wa kitabu cha 1 Wafalme
16:34 kuwa haya mambo yalitokea sawasawa na jinsi ambavyo Yoshua alisema. Kwa
hiyo Mungu anapokupa mstari wa namna hii maana yake shughulika na laana iliyopo
vunja kwa Damu ya Yesu.
9. KEMEA ILI VIONDOKE VYOTE
VILIVYOKAA KWENYE ENEO UNALOLIOMBEA LILILOSHINDIKANA KUJENGWA AU HALIKALIKI
HATA BAADA YA KUWA UMEKWISHA MALIZA UJENZI
Kitabu cha Isaya 13:19–22 utaona ya kwamba ukiwa ukishuka
mahali si tu kwamba unazuia watu wasikae bali unaweka zuio watu wasijenge,
unaweka zuio waliojenga zibomoke na unaweka zuio kwa wale waliokamilisha nyumba
zisikalike lakini pia wale walioamua kubaki kupoteza nguvu za kufanya shughuli
mbalimbali wanakuwa mjini lakini mji(nchi) umejaa ukiwa.
Na maandiko
yanasema kwamba ukiwa ukiingia mahali ni kama vile Mungu anakuwa anaswaga hivi
vitu yaani kuna kibali kinatolewa, linawekwa zuio na si tu zuio lakini
kinawekwa kitu kingine cha kusaidia, na maandiko yanasema “hayawani wakali wa
nyikani” Isaya 13:21a, ili ukitaka kwenda kujenga wapambane na wewe. Na Biblia
inazidi kusema “na nyumba zao zitajaa bundi; mbuni watakaa huko; na majini
watacheza huko” Isaya 13:21b.
Kwa hiyo
ukiona nyumba haijakaliwa muda mrefu unajua sasa kitu cha kufanya kwa sababu
yawezekana kuna majini yamewahi huko ndani. Kwa mfano unapoamua kununua gofu au
nyumba ambayo haijaisha usije ukafikiri liko/iko yenyewe tu.
10.OMBA MUNGU AKUJULISHE IKIWA UKIWA
UMEONDOLEWA NA WAKAAJI HAO WABAYA NA WAMESHALIACHIA ENEO HILO
Hii
inamaanisha umeshafanya maombi sasa unataka kujua ya kwamba ukiwa umeondoka.
Kwanini basi unataka kujua hili? Kwa sababu ukiwa ni zuio na ni zuio
linalotumia kuzia kitu fulani na kumwambia yule mtu aliyewekewa zuio apate
kufanya matengenezo.
Sasa si kila
mahali kwenye tatizo la ardhi Mungu anatumia ukiwa kama zuio. Maana inategemea
na hii ni kutokana na mstari nilioanza nao. Kwa hiyo ukitaka kujenga kwenye
kiwanja ambacho kina zuio ni lazima kwanza uweze kuondoa zuio ili uweze
kuendelea, kwa sababu zuio liko kisheria.
Ukisoma Yeremia 4:27–28 Biblia inasema Mungu atakupa ndani
yako maombi ya kimaombolezo. Kuna mzigo fulani utakuja ndani yako na ukiwa
unakuja utakuja na kitu cha maombolezo na maombolezo hayo yatakusukuma kuomba.
Hayatakusukuma kukaa ndani bila kufanya kitu.
11. WEKA WAKFU KWA MUNGU HILO
ENEO/MKABIDHI MUNGU KWA MAOMBI HILO ENEO
Inawezekana
kabisa umemwomba Mungu na ndiye aliyekupa hilo eneo lakini bado anataka uweze
kumkabidhi yeye kwa njia ya maombi pia. Mwambie Mungu nakupa ili eneo ni la
kwako lifunike kwa damu yako, lilinde na kulitumia jinsi unavyotaka. Ukifanya
namna hii na kuwa na nidhamu ya namna hii kwenye eneo hilo ambalo unataka
kujenga kila ukikanyaga na kusema maneno hayo ya kumkabidhi Mungu ndani yako
Mungu anakupa plan (mpango).
2 Mambo ya Nyakati 6:12–42 Biblia inasema Sulemani alipokwisha
kumaliza kujenga nyumba ya Bwana na nyumba yake mwenyewe sawasawa na yote
yaliyoingia ndani mwake moyoni mwake kuyafanya. Sulemani aliwekewa moyoni namna
ya kujenga nyumba ya Bwana na namna ya kujenga nyumba yake. Kwa hiyo unapoweka
wakfu usiweke wakfu kijumla jumla bali weka wakfu ardhi, mipaka na kiwanja,
weka wakfu misingi ya kiwanja, weka wakfu malango ya kiwanja, ramani
utakayochora mahali hapo.
12. VISEMESHE ARDHI NA MBINGU
VISIKWAMISHE UENDELEZAJI WA UJENZI NA UTUMIAJI WA KILICHOJENGWA
Kumbukumbu ya Torati 32:1 “Sikilizeni, enyi mbingu, nami
nitanena; Na nchi isikie maneno ya kinywa changu.” Nchi au ardhi inaweza
kusikia. Kwa hiyo ni vizuri kuitangazia kwamba zuio limeondoka. Kwa hiyo ardhi
ijue kwamba ardhi hiyo sasa ni mali ya fulani kihalali katika ulimwengu wa
roho. Au kama ni wewe mwenyewe unaiombea hiyo ardhi jifunze kuisemesha ardhi
kuwa ni mali yako kwamba isijaribu kukupinga bali yenyewe ni mali yako ambayo
Mungu amekupa kwa sababu umesha pita hatua zile nyingine zote na kukemea hata
yake majini yaliyokuwa yakikaa humo na kuwa umeshaiweka wakfu kwa Mungu na
Mungu ameshatamalaki hapo.
Ukishasemesha
namna hiyo ardhi inasikia na mbingu inasikia. Na Biblia inasema Mungu anapokuja
mahali anaita nchi na mbingu na vitu vyote vinasimama kwa pamoja. Maana yake
vinategemeana. Na ndiyo maana ukisoma kwenye Biblia utakuta ikisema mbingu
kufunuka na mbingu kumfunukia. Sasa mbingu ikifunuka ni kwa ajili ya watu wengi
lakini mbingu kumfunukia mtu ni kwa ajili ya mtu mmoja au wawili au eneo.
MUNGU AKUBARIKI SANA KWA KUJIFUNZA MANENO YA MUNGU KUPITIA BLOG HII.
0 Comments