Mchungaji Laurent Mpoma
VITU VYA MSINGI KUJUA KUHUSU IMANI
Katika Waebrania 11:1 Biblia inasema “Basi imani ni kuwa na hakika na mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana”.
Biblia inasema “Akapanda chomboni wanafunzi wake wakamfuata. Kukawa msukomsuko mkuu baharini, hata chombo kikafunikizwa na mawimbi; naye alikuwa amelala usingizi. Wanafunzi wake wakamwendea wakamwamsha, wakisema, Bwana, tuokoe, tunangamia. Akawaambia mbona mmekuwa waoga, enyi wa imani haba? Mara akaondoka akazikemea pepo na bahari; kukawa shwari kuu, Wale watu wakamaka wakisema, Huyu mtu ni wa namna gani hata pepo na bahari zamtii?” (Mathayo 8:23-27).
1: Imani ipo katika viwango mbalimbali vinavyopimika.
Mfano huu wa Yesu unatusaidia kujua kwamba kumbe imani ipo katika viwango mbalimbali, mfano imani ndogo na kubwa. Ni wazi kwamba imani ndogo/haba haiwezi kutengeneza jibu la mahitaji yako.
2: Unaweza ukawa na Yesu na usiamini kwamba anaweza kukusaidia.
Ukweli huu tunaupata baada ya kusoma habari hii kama ilivyoandikwa katika Marko 4:36-41. Ule mstari wa arobaini unasema ‘Akawaambia, mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado?
Ni imani yangu kwamba Yesu aliwauliza swali hili huku ndani yake akijaribu kufikiri sababu ya wanafunzi kushindwa kunyamazisha ile dhoruba. Si kana kwamba wanafunzi wa Yesu hawakumuamini yeye kabisa. La hasha, walimwamini ndio maana waliacha kazi zao na familia zao kumfuata Yesu.
Imani ambayo wanafunzi waliikosa ni ile ya Yesu kuweza kuwaokoa na dhoruba iliyokuwa inawakabili. Ndivyo ilivyo hata leo, licha ya maelfu ya watu kumwamini Yesu kama Bwana na mwokozi wao, wengi hawana imani naye kwamba anaweza kuwaponya magonjwa yao, ndoa zao, familia zao, nchi zao nk au jaribu lolote mfano wa hili la wanafunzi.
3: Unaweza kuwa na imani lakini ipo pengine na si kwa Yesu.
Naam ukweli huu unathibitika baada ya kusoma habari hii katika kitabu cha Luka 8:22-25. Ule mstari wa ishirini na tano unasema ‘Akawaambia, imani yenu iko wapi? Wakaogopa, wakamaka, wakisema wao kwa wao, Ni nani huyu basi hata anamuru pepo na maji, navyo vyamtii?
Kwa mujibu wa Luka, Yesu alitambua kwamba imani ya wanafunzi wake haikuwa kwake bali mahali pengine. Na ndiyo maana aliwauliza iko wapi imani yenu? Kwa lugha nyingine aliwaambia najua imani mnayo, lakini haipo kwangu.
4: Imani inaweza kuhamishika tegemeana na nini unasikia
Kwa mujibu wa Warumi 10:17, chanzo cha imani ni kusikia. Imani katika Kristo inakuja kwa kusikia habari za Kristo, imani kwa Shetani inakuja kwa kusikia habari za Shetani nk. Kwa hiyo mtu mwenye imani katika Kristo imani yake inaweza kuhama kutoka kwa Yesu kwenda kwa Shetani tegemeana na ameruhusu nafsi yake kusikia na kutafakari vitu gani. Jambo hili ndilo lililowatokea Adam na Hawa katika bustani ya Edeni (Mwanzo 3:1-8).
Ili imani yako isihamishike jenga mazingira ya kusikia na kusoma neno la Mungu ukitafakari kila iitwapo leo. Naam kwa mapato yako yote jipatie ufahamu wa neno la Kristo. Hakikisha unaongeza imani yako katika kila eneo ambalo unajua imani yako imepungua au ipo kwa kiwango kidogo.
KWA MAHITAJI YA MAOMBI NA MAOMBEZI
MCHUNGAJI LAURENT MPOMA
0763652896
WATSAP: 0763652896
>>>KATIKA MKUTANO WA INJILI , DADA ALIYE TESEKA KWA MUDA MREFU AFUNGULIWA.....KUONA BOFYA KATIKA VIDEO
0 Comments