SOMO: UMUHIMU WA KUFANYA MAOMBI.
Bwana YESU KRISTO ASIFIWE.
Mathayo 21:22 Biblia inasema yeyote tunayoyaomba tukiamini tutayapata, hiyo inaonyesha maombi ya jambo la muhimu sana na tukiomba kwa imani tutapokea kutoka kwa MUNGU kile tulichoomba kilicho ndani ya kusudi lake.
Mathayo 21:22 "Na yo yote mtakayoyaomba katika sala mkiamini, mtapokea."
Maombi ni kitu cha muhimu sana kwa kila Mteule wa KRISTO YESU.
Bwana wetu YESU KRISTO hakuwa na haja sana ya kufanya maombi ila alikuwa na ratiba za maombi hivyo kutupa kielelezo sisi tuwe watu wa maombi.
Marko 1:35 Biblia inasema Bwana YESU "Hata alfajiri na mapema sana akaondoka, akatoka akaenda zake mahali pasipokuwa na watu, akaomba huko."
Bwana YESU alikuwa na maombi ya asubuhi, hiyo inatufundisha hata sisi wateule wake tuwe watu wa maombi.
Marko 6:46 "Hata alipokwisha kuagana nao akaenda zake mlimani kuomba."
Desturi ya Bwana YESU alipokuwa duniani katika mwili wa kibinadamu ilikuwa ni kuomba.
Hata sisi Biblia inatutaka tujifunze kwa YESU maana yeye ndiye kielelezo chetu.
Mathayo 11:29 "JITIENI NIRA YANGU, MJIFUNZE KWANGU; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;"
Ndio maana leo tuko hapa ili kujifunza umuhimu wa kufanya maombi na ili tuombe.
NDUGU, maombi yako ya leo yanaweza kukuacha huru katika eneo ambalo nguvu za giza zlikushikilia.
Kumbuka kazi mojawapo zilizomleta Bwana YESU duniani zimewekwa wazi katika Luka 4:18-19 kwamba wafungwa wa kiroho wafunguliwe.
Vipofu wa kiroho wafunguliwe.
Kuwaacha huru waliosetwa na nguvu za giza na kutangaza muda wa ushindi.
Luka 4:18-19 " ROHO wa BWANA yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa BWANA uliokubaliwa."
Inawezekana na wewe unahitaji kufunguliwa na Bwana YESU, inawezekana ni ndoa yako au kazi yako au afya yako ndivyo unahitaji vifunguliwe na Bwana YESU, Maombi yako yanaweza yakafanya kweli kabisa ufunguliwe katika maeneo hayo na ukawa huru kabisa.
Inawezekana ni akili yako ndio unataka ifunguliwe, inawezekana uzao wako au Kanisa au uchumi ndivyo vifunguliwe, maombi yako yanaweza kufanya hakika maeneo yako hayo yakafunguliwa na ukawa huru kabisa.
Inawezekana wewe umeshafunguliwa tayari lakini wapo wanaokuhusu ambao bado hawajafunguliwa wanateswa na nguvu za giza, leo katika jina la YESU KRISTO omba ili wafunguliwe na MUNGU wetu wa miujiza yuko tayari wakati wote kutenda miujiza, omba ndugu na utamuona MUNGU.
Muhimu tu katika maombi yako ya kila siku au kila Mara usisahau kuzingatia mambo haya matatu muhimu.
1. Kumbuka kutubu kwa ajili ya chanzo cha tatizo ambalo unataka liondoke.
Kwanini uombe toba juu ya chanzo cha tatizo?
Isaya 59:1-2 " Tazama, mkono wa BWANA haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia; lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na MUNGU wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia."
Inawezekana ulionywa kiroho lakini haukusikia hivyo ni wewe ukasababisha kifungo cha giza, ukimwendea MUNGU akusaidie tubu kwanza.
Inawezekana ni makosa ya Babu zako au Baba zako, hivyo anza na toba kwanza.
Inawezekana MUNGU aliwatumia watumishi kwake kwa namna mbalimbali ili wakuonye lakini hukuwasiikiliza bali ukaendelea na dhambi na kujikuta katika vifungo vya giza, sasa katika maombi yako wakati huu sio tu kufuta tatizo kwa maombi bali anza na toba kwanza.
Kutubu ndio mlango wa kwanza unaomfanya MUNGU akuangalie hata akusaidie.
2. Omba hitaji lako kwa MUNGU.
Yohana 14:14 "Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya."
Kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO kwa maombi fungua pailipofungwa kipepo na patafunguliwa.
3. Mshukuru MUNGU.
Wakolosai 4:2 "Dumuni sana katika kuomba, mkikesha katika kuomba huku na shukrani;"
Ni muhimu sana katika maombi yako uwe unahusika na vipengele hivyo vitatu kama unahitaji matokeo sahihi.
Tubu, ombea hitaji na mshukuru MUNGU.
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
MUNGU AKUBARIKI SANA.
0762756542

0 Comments