MAOMBI YA MGUSO WA MUNGU SEHEMU YA KWANZA:
Katika mguso wa kwanza Bwana Yesu Kristo anaingia katika mji uitwao Naini lakini alipokaribia lango la mji anakutana na watu wenye msiba wa kufiwa na mpendwa wao.
Pamoja na msiba huo wapo wengine walikuwa na msiba magonjwa, madeni na pia uchungu mioyoni mwao.
Msiba huu unatokana na sababu ya kuwa kila walichokuwa wakijaribu kukifanya kinakufa kwa kuzaa mapooza hivyo BWANA YESU alipomwona yule mama aliyefiwa, akamwonea huruma na akamwambia asilie.
“Akakaribia, akaligusa jeneza wale waliokuwa wakilichukua wakasimama.”
Huu ndio mguso wa kwanza ambapo kijana aliyekufa na kubebwa na watu ndani ya jeneza na wakiwa njiani walikutana na Yesu langoni na akaligusa jeneza.
Swali la kujiuliza Kwanini Yesu aligusa jeneza?, jibu lake ni hili , jeneza ndicho kizuizi cha kwanza kinachomfanya aliye kufa asiguswe moja kwa moja na Yesu Kristo ili apokee muujiza.
Hii ndio maana ya jeneza, “Tazama mkono wa Bwana haukupunguka hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito hata lisiweze kusikia lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia.” Isaya 59:1-2
Neno hili linatudhihirishia ni nini maana ya jeneza ,ambapo ni dhambi na uovu ambazo humziba mtu wa Mungu asiguswe na Yesu Kristo.
Wapo watu wengi ambao ni wakristo lakini wamo kwenye majeneza ya ulevi, uzinzi,uongo, dhuluma , fitina na mambo yote yanayofanana na hayo , elewa ya kuwa majeneza hayo ni mazito na lazima yakutane na Yesu Kristo katika mguso wa kwanza ili ayasimamishe yasiendelee na safari ya kwenda makubirini maana mshahara wa dhambi ni mauti.
“Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti, bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.” Warumi 6:23
Mkristo lazima uache kutenda dhambi maana huwezi kuendelea kufanya dhambi na ukataka kuona baraka za Mungu , fahamu ya kuwa Mungu hadhihakiwi na apandacho mtu ndicho atakachovuna.
“Msidanganyike Mungu hadhihakiwi kwa kuwa cho chote apandacho mtu ndicho atakachovuna. Maana yeye apandaye kwa mwili wake katika mwili wake atavuna uharibifu bali yeye apandaye kwa Roho katika Roho atavuna uzima wa milele.” Wagalatia 6:7-8
Hivyo yakupasa usidanganyike ya kuwa unaweza kuwa na maisha ya dhambi ndani mwa kanisa na bado ukapata baraka katika maisha yako, tambua ya kuwa hakuna atakayemwona Mungu katika maisha yake ya sasa na ya baadaye asipokuwa na huo utakatifu
“Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao;” Waebrania 12:14
Hivyo huu ni wakati wako wa kuacha dhambi na kuokoka,“Kwa maana atakaye kupenda maisha na kuona siku njema auzuie ulimi wake usinene mabaya, na midomo yake isiseme hila. Na aache mabaya atende mema atafute amani, aifuate sana. Kwa kuwa macho ya Bwana huwaelekea wenye haki, na masikio yake husikiliza maombi yao bali uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya.” 1Petro 3:10-12
Hivyo kwa maneno haya ni wazi kuwa katika mguso wa kwanza ndipo tunapookoka na kuanza maisha mapya ya kimaombi. Hivyo zingatia kweli hii ya kuwa afichaye dhambi hatafanikiwa hata kama ana mipango ya mafanikio bali yule aziungamaye atapata rehema.
“Afichaye dhambi zake hatafanikiwa bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.” Mithali 28:13.
MUNGU AKUBARIKI SANA KWA KUJIFUNZA ZAIDI NA KUENDELEA KUFUATILIA MASOMO HAYA.
>>Maombi na maombezi piga: 0762756542, 0782859946, 0714890889
>>Tuma hitaji lako kwa namba hapo juu AU Watsap: 0762756542
>>E-mail: mchungajilaurent@gmail.com
>>Jifunze masomo mbalimbali hapa>>>"upenyowamungu.blogspot.com"
>>Kupata video za mafundisho na mahubiri youtube ingia hapa>>"https://bit.ly/2wNLG8j" kisha usisahau "SUBSCRIBE" Kisha bofya kengele, ili uwe wa kwanza kupata video zetu zote.

0 Comments