MAMBO 7 YA KUFANYA IKIWA MAFANIKIO YAKO YAMEFUNGWA NA NGUVU
ZA GIZA.
1. KUMPA BWANA YESU MAISHA YAKO: Hiki ni kipengele muhimu
sana kwa mtu anayetaka kutembea kuishi sawa na kusudi la Mungu. Kuokoka ni
kumpokea Yesu kama Bwana na Mwokozi wa maisha yako. Pia mwamini Yesu kama
Mfalme wa wafalme (Ufunuo 19:16). Unapookoka, ya kale yanapita na unakua kiumbe
kipya (2 Warorintho 5:17). Ukiokoka Mungu anayatupilia mbali maovu yako yote
(Mika 7:19) na hakumbuki tena dhambi zako (Isaya 43:25).
Lakini mtu kama hajaokoka Roho wa Mungu anakuwa hayupo ndani
yake na kibiblia mtu huyo anakuwa amekufa (Yakobo 2:26). Biblia inazumgumzia
juu ya kufufuliwa pamoja na Kristo (Waefeso 2:6). Huwezi kufufuliwa kama
hujafa. Maandiko yanasema “Mauti na Kuzimu zikatupwa katika lile ziwa la moto.
Hii ndiyo mauti ya pili, yaani hilo ziwa la moto. Na iwapo mtu ye yote
hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la
moto” (Ufunuo 20:14—15). Je mauti ya kwanza ni ipi?
Nimekuonesha mistari hiyo makusudi kwani mtu kama hajaokoka
kuna vitu Mungu hawezi kukupa katika maisha yao. Lakini ukiwa na Yesu unakuwa
mtoto wa Mungu na Roho Mtakatifu anashuhudia pamoja na roho yako (Warumi
8:16). Unapokuwa mtoto wa Mungu,
unaingizwa kwenye agano na Mungu lenye muhuri wa Roho Mtakatifu na unapewa
kurithi pamoja na Kristo katika ulimwengu wa roho. Yesu anakutoa kutoka katika
ufalme wa giza kwenda ufalme wa Mwana wa pendo lake (Wakolosai 1:13).
Unapokuwa ndani ya agano hili, baraka zote za rohoni unapewa
(Waefeso 1:3). Lakini kumbuka kupewa baraka na kutembea ndani ya baraka ni vitu
viwili tofauti. Siyo kila aliyepewa baraka anazifaidi. Yakobo alikuwa ndani ya
baraka za agano lakini Yusufu akaondoka nazo kwenda Misri. Mungu akabariki
nyumba ya akida kule Misri badala ya Yakobo aliyeko ndani ya agano. Kuna baraka
za kiagano katika Kristo Yesu ambazo huwezi kuzipata mpaka uwe mtoto wa Mungu.
Ukiwa mtoto wa Mungu, Roho Mtakatifu anaingia ndani yako na kukufunulia
maandiko (Yohana 14:26). Na Roho huyu anakupa macho ya kuona chimbuko la
kutokufanikiwa kwako kimaisha.
2. FAHAMU WAPI UMEFUNGWA: Huwezi kujifungua kutoka kwenye
kifungo ambacho hukijui. Na huwezi kujua kilichokufunga kama huijui sheria
iliyokufunga katika ulimwengu wa roho. Na huwezi kujifungua kama hujui sheria
inayoweza kuitangua ile sheria iliyokufunga katika ulimwengu wa roho. Na huwezi
kujifungua kama hujui kipengele au vipengele vilivyoko katika ile sheria ambayo
shetani ametumia kufunga mafanikio yako. Lakini je, utaijuaje sheria
iliyokufunga?
Ili uweze kuijua sheria hii, lazima uwe na neno la Kristo.
Kumbuka “imani chanzo chake ni kusikia. Na kusikia huja kwa neno la Kristo”
(Warumi 10:17). Sauti ya Neno la Kristo ndiyo inakupa mafunuo ya kujua eneo au
maeneo ambayo umefungwa katika ulimwengu wa roho. Kama huna neno, Mungu anaweza
kukuambia kifungo chako kilipo lakini usielewe au usisikie wakati anasema nawe.
Hivyo ili uweze kukijua kifungo chako kilipo, lazima uwe na maarifa ya neno la
Kristo.
3. TOBA: Ukishajua vifungo vyako vilipo, fanya toba thabiti
itayokufungua kutoka kwenye vifungo hivyo. Kushindwa kufanya toba kunaweza
kukufanya uendelee kuishi katika kifungo hicho. Lakini je ni toba ipi ambayo
unatakiwa uifanye katika kifungo fulani? Utajuaje kama Mungu amekubali toba
yako? Ukisoma habari za wana wa Israel walipoabudu miungu mingine utaona kuwa
ilimgarimu Musa toba za 4. Pia soma habari za Gidion katika kitabu cha Waamuzi.
Wakati mwingine inakulazimu ufunge na kuomba ili uweze kufunguliwa (Matayo
17:21). Je utajuaje toba ambayo lazima ufunge na kuomba?
Kumbuka Damu ya Yesu inanena mema (Waebrania12:24).
[Waebrania 9:11—27 inaeleza zaidi juu ya damu ya Yesu]. Damu ya Yesu ni damu
pekee inayofuta maagano pamoja na sahihi za mashahidi wa kipepo katika
ulimwengu wa roho. Damu ya Yesu ikishafuta [toba yako imepokelewa], shetani
anakosa uhalali wa kushikiria mafanikio yako. Lakini hii haina maana huwezi
kufungwa tena maeneo mengine. Kumbuka toba inakurudisha tena kwa Mungu. “Nao
watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao” (Yeremia 32:38).
4. RUDISHA MAFANIKIO YAKO: Toba yako ikishakubaliwa mbele za
Mungu, milango ya mafanikio yako inafunguliwa tena. Unaweza kurudishiwa
mafanikio yote ambayo shetani alikuwa ameyafunga katika maisha yako. “Nami
nitawaruishia hiyo miaka iliyoliwa na nzige” (Yoeli 2:25).
Lakini je utawezaje kurudisha mafanikio yako? Napoongelea
“mafanikio” siongelei kupata hera, kupata kazi fulani, au kuwa na elimu fulani.
Nazungumzia kutenda kusudi katika maisha yako ili kuujenga ufalme wa mbinguni.
Hivyo unatakiwa kuomba Mungu ili akufunulie nini kusudi la maisha yako. Haya ni
maombi muhimu kwa kila aaminie. Lakini je unaombaje ili ujue kusudi lako katika
maisha yako? Utajuaje kama maono uliyonayo ni maono ya Mungu au maono yako?
Kumbuka unapokuwa unaomba, siyo kila sauti utayoisikia
inatoka kwa Mungu. Wakati mwingine unapoenda kuomba na shetani naye anakuwepo.
“Ilikuwa siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda kujihudhurisha mbele za
BWANA, Shetani naye akaenda kati yao” (Ayubu 1:6). Shetani anaweza akafanya
usisikie maono Mungu anakuambia juu ya maisha yako. Badala yake ukaisikia sauti
ya shetani ukidhani ni sauti ya Mungu. Kama sauti siyo ya Mungu, utakosa amani
katika moyo wako kwa njia ya utofauti. Ndo maana ni muhimu sana kila unapokosa
amani kujua sababu.
Lakini ukiwa na neno, Mungu atakuelekeza wapi pana mafanikio
aliyokukusudia na utaisikia sauti yake. Kumbuka mafanikio yako hayategemi maono
uliyo nayo na wala hayategemei maono ya mtu mwingine juu yako. Mafanikio yako
yanategemea maono ya Mungu katika maisha yako. JE UNAYAJUA MAONO YA MUNGU
KATIKA MAISHA YAKO? [Hakikisha jibu la swali hili ni ndio]. Mungu alimwambia
Isaka asiende Misri na kuwa atambariki mahali alipo (Mwanzo 26:2—3). Wengi
wanadhani mikoa au maeneo fulani ndo kuna mafanikio. Muulize kwanza Mungu kwani
unaweza kwenda Misri na kuacha baraka zako ulipotoka.
5. FUNGA MLANGO WA ADUI ASIKUVAMIE TENA: Ukisharudisha
mafanikio yako, hakikisha unafunga milango yote ya adui katika ulimwengu wa
roho ili nzige wasirudi kula ghala yako. Unafunga mlango wa adui na kumkabidhi
BWANA awe mmiliki wa kila ulichonacho. Ukimpa Yesu amiliki kila kitu, adui
hawezi kukushinda. Mungu atawatupilia nje adui zako wote (Sefania 3:15).
Kushindwa kufunga mlango wa adui kunaweza kukusababishia
kukwama tena kimaisha na kuwa na hali mbaya zaidi ya ile ya mwanzo. Hujawahi
kuona mtu anafilisika halafu baadae anafanikiwa kimaisha. Halafu baada ya muda
anafilisika tena na anakuwa na hali mbaya zaidi ya mwanzo. Unadhani tatizo
linaweza kuwa nini? Moja ya sababu inaweza kuwa kushindwa kufunga mlango wa
adui. Je unafungaje mlango wa adui katika ulimwengu wa roho na adui asiweze
kuufungua tena?
6. TENDA MAPENZI YA MUNGU: Ni muhimu sana kuishi maisha ya
kumpendeza Mungu ili kuhakikisha kuwa hurudi kwenye hali yako ya kutofanikiwa.
Kuishi katika dhambi kunaweza kukusababisha ukwame tena kimaisha hata kama
ulikuwa tayari umeshanguliwa. Yesu baada ya kumponya yule mtu aliyekuwa hawezi
kwa miaka 38 (Yohana 5:5—9) alimwam
bia: “usitende dhambi tena, lisije likakupata jambo lililo
baya zaidi” (Yohana 5:14).
Unapofunguliwa kutoka kwenye vifungo vya giza, kuendelea
kuishi maisha ya dhambi kunaweza kukurudishia mapepo wabaya zaidi ili
wakukwamishe kimaisha zaidi ya mwanzo. “Pepo mchafu, amtokapo mtu, hupitia
mahali pasipo maji akitafuta mahali pa
kupumzika, asipate. Halafu husema, Nitarudi nyumbani kwangu nilikotoka; hata
akija aiona tupu, imefagiliwa, na kupambwa. Mara huenda, akawachukua pamoja
naye pepo wengine saba walio waovu kuliko yeye mwenyewe, nao huingia na kukaa
humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza” (Matayo
12:43—45). Kwa nini huyu pepo awalete pepo 7? Kumbuka 7 na namba ya utimilifu
katika ulimwengu wa roho hivyo unaweza kuelewa kitachotokea.
Hivyo dhambi ni ufunguo shetani anautumia ili kuharibu zaidi
mafanikio yako. “Kwa maana wale waliokwisha kuyakimbia machafu ya dunia kwa
kumjua Bwana na Mwokozi Yesu Kristo, kama wakinaswa tena na kushindwa, hali yao
ya mwisho imekuwa mbaya kuliko ile ya kwanza” (2 Peter 2:20).
7. MZALIE MUNGU MATUNDA: Mungu akikurudishia mafanikio yako
na ukayatenda mapenzi yake, lazima utamzalia matunda. Mungu anatutambua kwa
matunda yetu (Mayato 7:16). Ukiona bado unashindwa kumzalia Mungu matunda,
yamkini bado unaishi nje ya kusudi la Mungu. Kipimo cha mafanikio yako kipo
kwenye mavuno siyo kwenye mbegu wala kwenye eneo unalopanda. Kiasi cha mavuno
uvunayo hakitegemei kiasi cha mbegu uliyopanda; wala hakitegemei kile
unachotegemea kuvuna. “Mmepanda mbegu nyingi, lakini mkavuna kidogo; mnakula
lakini hamshibi… Mlitazamia vingi, kumbe vikatokea vichache” (Haggai 1:6,9).
Hivyo matunda yako yawe kipimo kujua kama unatembea katika nafasi Mungu
aliyokupa katika ulimwengu wa roho ili kuujenga ufalme wa mbinguni.
Je utajuaje kama unaishi chini ya kiwango Mungu amekukusudia? Na ukijua unaishi chini ya kiwango Mungu amekukusudia unafanya maombi gani ili uweze kuishi sawa na kusudi la Mungu?
MAOMBI NA MAOMBEZI
WASILIANA NA MCHUNGAJI KIONGOZI LAURENT MPOMA
NCHI YA UKOMBOZI MINISTRY
(HEMA LA MAOMBI NA MAOMBEZI)
MWAJA KITOPE SINGIDA MJINI
PIGA/TUMA MAHITAJI YAKO
0763652896, 0714890889
WHATSAP: 0762756542
0 Comments