FAIDA SABA ZA KUMSHUKURU MUNGU.
FAIDA YA KWANZA
1. NI ISHARA YA ROHO MTAKATIFU KWAKO KUKUONYESHA KUWA UNATEMBEA
KATIKA MAPENZI YA MUNGU.*
Hii tunaipata kwa kusoma 1 Thesolanike 5:19
“shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu
kwenu katika Kristo Yesu Msimzimishe Roho;”_
Maana yake Roho Mtakatifu yuko kazini kwa sababu unaweza
kupita mazingira ambayo kwa jinsi ya kawaida unaweza kushindwa kushukuru lakini
Roho Mtakatifu anapokaa ndani yako anatamani kushukuru ili kila mahali
unapopita utembee ndani ya mapenzi ya Mungu kwa kuwa na maisha yaliyojaa
shukrani mbele za Bwana.
Kama mahali unapopita
kwa mazingira ya nje yanaweza yakakataa kuwa hili si la Mungu kwa sababu
unapita pagumu. Lakini Mungu anakuambia kuwa hili ni jambo sahihi kwako
kulipitia. Ukiona hali ya namna hiyo ndani ya moyo wako Roho Mtakatifu atakupa hali ya kuwa na moyo wa shukrani.
Mahali unapopita saa nyingine hapafananii na kushukuru
lakini ni mapenzi ya Mungu upite hapo. Ndio maana kila wakati kama unajua
umeokoka (maana yake Roho Mtakatifu anakuongoza kutoka ndani) kwa sababu
ukiokoka agano jipya linaanzia ndani (kutahiriwa moyo wako) ndipo linaenda nje.
Agano la kale lilikuwa linaanzia nje kwa kutahiriwa nje
ndipo mtu anatafuta msaada wa kubadilika ndani. Ila agano jipya unatahiriwa
ndani na unazaliwa kiumbe kipya kwa Mungu Baba. Roho Mtakatifu anakuja na
sheria za Mungu kukaa ndani yako ili utembee katika Bwana. Kwa sababu hiyo Roho
Mtakatifu anapoongoza watu, atakuongoza kutoka ndani kwanza bila Yeye kutazama
kwanza mazingira ya nje kwa kile Mungu anachokueleza.
Mazingira ya nje yanaweza kukuambia hapa Mungu hayupo
(hutembei kwenye mapenzi ya Mungu) lakini Roho Mtakatifu alieko ndani yako
atakupa moyo wa shukrani. Ukisikia ndani yako kuwa na moyo wa kushukuru hata
kama mazingira ya nje hayafananii kushukuru, pokea na shirikiana na Roho
Mtakatifu na wala usimzimishe anapokuja kushukuru kwa Mungu ndani yako.
Hali ya kushukuru ni ishara kwako kuwa ni mapenzi ya
Mungu yako pamoja nawe hata kama akili yako inakataa kwa sababu mapenzi ya
Mungu si mapenzi yako wala si lazima uyafurahie kwa jinsi ya kibinadamu kwa
sababu _“mawazo yake si kama yetu, njia zake si njia zetu”_ Kwa hiyo usijaribu
kumfananisha Mungu ni kama sisi.
2. INAONGEZA UNYENYEKEVU ULIOAMBATANA AU UNAOAMBATANA NA
HOFU YA MUNGU.*
Hii tunaipata tunaposoma. Waefeso 5:20-21
“na kumshukuru Mungu Baba sikuzote kwa mambo yote, katika
jina lake Bwana wetu Yesu Kristo; hali mnanyenyekeana katika kicho cha
Kristo.”_
KICHO ni HOFU au UCHAJI. Unapomshukuru Mungu kwa mambo
yote kuna kitu kinachoambatana na hali ya shukrani kwa Mungu kuachilia moyo wa
unyenyekevu ndani yako. Kwa sababu kuna
mapito mbali mbali ambayo watu wanapitia na kwa jinsi ya kibinadamu mtu
mwingine anaweza kujikweza au akajishusha sana kutokana na hali anayoipitia. Lakini ukijua ni Bwana
anakuongoza kwa kila hatua, utajua si wewe bali Bwana ndani yako na hutachukua
na hali ya kuchukua utukufu wake. Bali utajua ni Mungu aliyekusaidia mpaka hapo ulipofika.
Biblia inasema
katika .Yohana 15:5b
“maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote.”
Kwa kawaida tawi haliwezi kuzaa peke yake, kuna kitu
kimeunganishwa nalo (liwe limeungana na mzabibu). Unapotembea kwenye mapenzi ya
Mungu, haijalishi mazingira ya nje yamekaaje, utakuwa unajifunza na kumshukuru
Mungu katika yote. Mambo mengine inakuwa vigumu sana kumshukuru Mungu
kibinadamu lakini Biblia inatuambia
katika
1 Wathesalonike 5:18
“shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu
kwenu katika Kristo Yesu.”
Unapoendelea kushukuru unyenyekevu unashuka. Kama ni
mhubiri au mwalimu kama mimi Mwakasege, jaribu uone; ukitoka kuhubiri mshukuru
Mungu kwamba *“Mungu ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kusimama, kunipa maneno
ya kusema, nisamehe mahali nilipofikia na wewe hukutaka…”* Jifunze kumshukuru
Mungu uwe na uhakika kuwa unyenyekevu utaendelea kushuka juu yako kwani
haitatokea siku ukijivunia ufunuo uliopata wala kujivunia watu waliopona kwa
sababu utajua si wewe hakuna hata siku utafurahia watu wanayokupigia makofi kwa
sababu utajua si ya kwako bali ni ya Bwana, utukufu ni wake Bwana kwa
alichofanta ulipotumika.
Kila wakati ule unyenyekevu unaposhuka, unashuka na hofu
ya Mungu (hali ya uchaji). Hivi vitu vinaambatana Pamoja (Unyenyekevu na Moyo
wa shukrani). Watu wengi hawajajua kwa sababu wanashukuru kwenye vitu vikubwa
vikubwa tu. Mshukuru Mungu kwa vitu vyote hata kama ni vidogo sana wewe shukuru
tu. Pia shukuru kwa mambo ambayo akili yako inachukia au inakataa kuwa hili halistahili shukrani.
Unaposhukuru namna hiyo amani ya Mungu ipitayo fahamu zote ghafla inakufunika.
Maana unapoendelea kushukuru ndani yako kuna kitu Mungu
anateremsha unyenyekevu ndani yako. Huwezi kumshukuru Mungu na ukawa na kiburi.
Shukrani zinaondoa kuburi kabisa.
Haijalishi umesoma kiasi gani ukienda ofisini na ukasema
Mungu nakushukuru kwa sababu ya kazi hii. Hakuna hata siku moja utajivunia
degree yako kazin balii utajua ni Mungu alikupa ili kurahisha utendaji
3. MUNGU ANAKUPA CHA ZAIDI KULIKO UNACHOSHUKURU KWA
KUKIPOKEA*.
Luka 17:11-19
“11 Ikawa walipokuwa njiani kwenda Yerusalemu, alikuwa
akipita katikati ya Samaria na Galilaya. 12 Na alipoingia katika kijiji kimoja,
alikutana na watu kumi wenye ukoma; wakasimama mbali, 13 wakapaza sauti
wakisema, Ee Yesu, Bwana mkubwa, uturehemu! 14 Alipowaona aliwaambia, Enendeni,
mkajionyeshe kwa makuhani. Ikawa walipokuwa wakienda walitakasika. 15 Na mmoja
wao alipoona kwamba amepona, alirudi, huku akimtukuza Mungu kwa sauti kuu; 16
akaanguka kifudifudi miguuni pake, akamshukuru; naye alikuwa Msamaria. 17 Yesu
akajibu, akanena, Hawakutakaswa wote kumi? Wale kenda wa wapi? 18 Je!
Hawakuonekana waliorudi kumpa Mungu utukufu ila mgeni huyu? 19 Akamwambia,
Inuka, enenda zako, imani yako imekuokoa.”_
Hili neno *imani yako imekuokoa* ni tofauti na jinsi
ambavyo tunafikiri juu ya wokovu. Kabla Yesu hajafa na kufufuka watu walikuwa
hawaokoki kama sisi tulivyokuwa tunaokoka . Neno Wokovu ni pana na lina vitu
vingi sana ndani yake. Hawa wakoma walikuwa na ukoma uliokuwa unakula viungo
vyao au ngozi. Aliposema nendeni mkajionyeshe kwa makuhani wakatii. Walipokuwa
wanaenda walitakasika maana yake ule ukoma ulipona. Viungo kama na ngozi
vilivyokuwa vinalika vikaacha kulika.
Biblia inasema ni mmoja tu Msamaria aliyerudi kumshukuru Mungu. Yesu aliuliza
wamepona wangapi na wamerudi wangapi kushukuru. Yule Msamaria aliambiwa imani
yako imekuokoa. Ina maana aliongezewa cha zaidi maana yake kama wengine
walipona ukoma la
kini viungo vyao viliharibika, wanakuwa wamepona tu ila
viungo vimebaki vile vile.
Lakini huyu Msamaria kama mikono yake vidole vilikuwa
vimetoka kama wale wengine lakini kwa kurudi kwake kushukuru Mungu alimrudishia
na vidole vyake. Wengine wanakuwa wamepona ukoma lakini vidole vyao havijarudi.
Aliyeshukuru anaongezewa vidole.
4. UKIMSHUKURU MUNGU KWA HATUA ILIYOPITA ANAKUPA HEKIMA
YA KUTUMIA KATIKA HATUA INAYOFUATA
Kutoka 18:8
8 Musa akamwambia mkwewe mambo hayo yote Bwana
aliyomtenda Farao na Wamisri kwa ajili ya Israeli, na mambo mazito yote
yaliyowapata njiani, na jinsi Bwana alivyowaokoa.
Baba mkwe wa Musa hakuwa Myahudi maana Musa hakuoa
myahudi alioa mtu wa Midiam na baba mkwe wake alikuwa Kuhani wa dini ya Midian
ambayo ni dini nyingine mbali na Mungu wa Musa.
Walipoenda kumpokea mzee Yethro wakati anamrudisha binti
yake na wajukuu zake kwa Musa ( Biblia haijasema Musa aliwapeleka lini lakini
walirudishwa kwake). Musa alimweleza mkwewe namna Mungu alichowafanyia na
kuwaokoa na Farao na namna alivyowazuia wamisri kupita bahari ya Shamu.
Ukiendelea mbele Biblia inasema Mzee Yethro alifurahi
sana na ndani yake alijaa moyo wa
shukrani, maandiko yanasema akatoa sadaka na chakula akakusanya viongozi wa
dini yake wakaenda kuleta sadaka na chakula mbele ya Mungu wa Musa na
wakamshukuru Mungu wa Musa kwa jinsi alivyomsaidia Musa na watu wake na wakala
mbele za Bwana.
Na walipomaliza kesho yake Musa akasimama asubuhi… kwa
sababu ni hatua nyingine ya maisha vita vimepungua sasa watu wanashida mbali
mbali wanataka mwongozo wamesimama mahali kwenye hema ya Musa, mstari umekuwa
mrefu sana wanasubiri zamu yao. Baba mkwe alipo amka asubuhi akamuuliza Musa
unafanya nini na akamweleza Neno gumu sana ambalo watumishi wengi wasingependa
kukisikia.
Kutoka 18:17
Mkwewe Musa akamwambia, Jambo hili ufanyalo si jema. Huna
budi utadhoofika wewe, na hawa watu walio pamoja nawe pia; maana jambo hili ni
zito mno kwako; huwezi wewe kulitenda peke yako.
Jambo hili si jema kuwapanga kwenye mstari asubuhi mpaka
jioni ,lingine ni kukaa na kuwafanyia watu counseling kuanzia asubuhi mpaka
jioni na akamwambia utadhoofika wewe!
Ndipo akampa hekima ya kwamba chagua watu ambao watabeba
mambo madogo madogo halafu yale mambo makubwa yataletwa kwako na kwa sababu
hiyo utapata nafasi na wenzako pia watapata nafasi na hata wale wanao hudumiwa
watarudi nyumbani wakiwa na amani na furaha
Maana yake alimwambia agawe majukumu. Na maandiko
yanasema huyu ndugu aligawa majukumu na foleni ikapungua
Sasa kama hujajifunza kumshukuru Mungu akakupa
unyenyekevu na ukujua si wewe unayefanya mambo yatokee bali ni Bwana. Sasa
kitakachokusumbua utasema nikiwaruhusu wengine si wataonekana kuliko mimi au
itajulikana kumbe kuna wanaofahamu hapa kanisani kuliko mimi.
Kama pia ndani yako kulikuwa na moyo wa kupata sadaka na
umeleta wasaidizi kama ishirini uwe na
uhakika sadaka zote hazitakuja kwako tena zitaenda kwa hao wengine na ukianza
kufikiria juu ya sadaka utabadilisha utaratibu utasema watu wote kwangu. Hii ni
kwa sababu moyo wako hauna hofu ya Mungu, hauna roho ya uchaji, hauna
unyenyejevu, haujajua namna ya kupokeana huduma na wengine kujua ya kwamba
katika mwili tunaviungo tofauti hakuna kiungo kimoja kinaweza kujiita mwili na
viungo vinashikiriana pamoja katika kuujenga mwili na kwa sababu hiyo hakuna
kiungo kinaweza kikajisifia, kitamsifia Mungu aliyemweka kwenye hiyo nafasi na
kumuunganisha na mtu mwingine. Kwa huduma ya yule na wewe unafaidika,
kuongezeka na unajulikana.
Waliosoma masomo ya management wanajua kitu kinachoitwa
delegation-- mambo ya delegation hayakutoka kwenye darasa la management
yalitoka kwenye Biblia ni ufunuo wakati wa kumshukuru Mungu.
Huyu ndugu ndiye aliyepewa ufunuo na hiyo hekima kwa
sababu yeye ndiye aliyeenda kumshukuru Mungu, aliyekuwa anaingia hatua ya pili
ni Musa sio Yethro lakini Musa alipomaliza hatua ile na kueleza mambo makubwa
Mungu aliyoyafanya hakurudi kwa Mungu kushukuru. Na kwa sababu hakurudi kwa
Mungu kushukuru hiyo hekima hakupewa yeye.
Lakini kwa kuwa shukrani inashuka na unyenyekevu utajua
kabisa hii hekima si yako ni ya Mungu na utajua si ya kukusaidia peke yako
lakini na Musa pia. Hata hivyo Yethro alimwambia unaweza kuchukua hiyo hekima
au ukaacha lakini unachofanya si sawa.
Kumbuka unapovuka hatua moja mshukuru Mungu kwa sababu
unapokuwa unamshukuru atakupa hekima ya kutembea kwenye hatua ya pili, kama
Mungu amekusaidia umefika 2020 mshukuru Mungu kwa hatua ya 2019 uwe na uhakika
atakupa hekima kwa ajili ya 2020.
Hiyo ndiyo inayowasukuma watu wengi wanapofiwa kwenda
kumshukuru Mungu, hakuna mtu anayeshukuru kwa kufiwa Ila wanashukuru wakisema
“Mungu asante kwa sababu umetusaidia katika kipindi hiki, umetutia nguvu
umetuvusha salama”. Wanaposhukuru namna hiyo hekima ya Mungu unaingia katikati
yao kwa ajili ya kuwasaidia katika hatua mpya ya maisha ambayo sasa hawana huyo
mtu, gape iliyobaki hekima ya Mungu inakuja kwa ajili ya kukusaidia wakati
ndani ukisema nitafanya nini kwa kuwa flani hayupo au nani atanisaidia.
Unapoenda mbele za Bwana kushukuru uwe na uhakika Roho
Mtakatifu atashusha hekima kwa ajili ya kukusaidia kwa ajili ya hatua
inayofuata
5. UNAPOMSHUKURU MUNGU KWA IMANI KWA AJILI YA USHINDI
AMBAO HAUJADHIHIRIKA BADO ANAKUPA HUO USHINDI.
2 NYAKATI 20:1-22_
1. Ikawa baadaye, wana wa Moabu, na wana wa Amoni, na
pamoja nao baadhi ya Wameuni, wakaja juu ya Yehoshafati vitani.
Kwa hiyo Yehoshafati mfalme wa Yuda alijikuta amezungukwa
na majeshi na alipojipima kwa jinsi ya kibinadamu hakuwa na namna ambayo
angeweza kupigana nao, akaitisha mbiu ya maombi na kufunga. Wakakusanyika watu
kuomba na wakamlilia Mungu sana wakijua kabisa hapo wanahitaji msaada wa Mungu
na kumbuka wakati wanamlilia Mungu majeshi yamewazunguka pande zote na katika
kuomba kwao Mungu akasema nao ujumbe ukashuka katikati yao kwamba vita hii si
vyenu Bwana atawapigania na kuwapa ushindi ( Soma hiyo habari yote).
Mungu alipo wajibu ndani yao walipata amani kiasi ambacho
walienda kulala wakiwa wamezungukwa na majeshi pande zote. Biblia inasema
2 Mambo ya Nyakati 20:20
20 *Wakaamka asubuhi na mapema*, wakaenda nje katika
jangwa la Tekoa; nao walipokuwa wakitoka, Yehoshafati akasimama, akasema,
Nisikieni, enyi Yuda nanyi wenyeji wa Yerusalemu; mwaminini Bwana, Mungu wenu,
ndivyo mtakavyothibitika; waaminini manabii wake, ndivyo mtakavyofanikiwa.
Wakaamka asubuhi na mapema_ maana yake yale walilala
kwanza ndipo wakaamka
Walipoamka jeshi lilikuwa limewazunguka maana walijua
hamna namna ambavyo wanaweza wakashambuliwa na kushindwa. Waliweka imani yao
mikononi mwa Mungu.
Ni watu wachache
sana wana imani za namna hiyo. Mtu kama Yona alikuwa na imani kama hii maana alikuwa
na uhakika na Mungu wake kuwa
anamfuatilia maana alipoona wenzake
wanahangaika kuwa merikebu itazama yeye
alilala. Ndio maana walimuuliza kuwa
tuambie wewe ni wa Mungu yupi na mmekorofishana nini na Mungu wako.
Yona alikuwa na uhakika sana na kitu cha kufanya na
alijua kabisa na kitu cha kufanya kuwa atupwe baharini na bahari itatulia. Basi
walipoamua kumrusha baharini na alipofika kule vilindini akakutana na Samaki
kaandaliwa kummeza.
Yesu alipokuwa ndani ya Boti na kulipotokea upepo
baharini yeye alilala kwenye shetri kwa sababu alikuwa na amani na uhakika kuwa
hatazama. Kuna kitu cha imani kinaa ndani ya mtu maana unapo omba juu ya jambo
fulani Mungu anakupa uhakika ya kwamba amejibu japo kwa nje huoni lakini ndani
yako unapata amani ipitayo fahamu zote inakupa usingizi wakati mazingira ya nje yanapiga kelele.
Turudi sasa kwenye hii habari ya Mambo ya Nyakati tunaona
hawa watu waliweza kulala na walipoamka asubuhi mfalme hak
upanga watu wa kupigana bali aliwapanga waimbaji ili
watangulie kushukuru kwa Mungu kwa ajili
ya ushindi na walikuwa na maneno ya pambio.
Waliimba mshukuru “Bwana kwa maana fadhili zake ni za
milele”. Waliimba kwa kurudia na kurudia.
Sasa Katika mstari
wa 22 biblia inasema katika
2 Mambo ya Nyakati 20:22
22 Nao walipoanza kuimba na kusifu, Bwana akaweka
waviziao juu ya wana wa Amoni, na Moabu, na wa mlima Seiri, waliokuja juu ya
Yuda; nao wakapigwa.
Bwana alisubiri mioyo yao na vinywa vyao vikutane na
Bwana wakati wanashukuru ndipo Bwana aliachilia ushindi kwao. maana walikuwa
wanashukuru kwa ushindi ambao haujadhihirika bado na Bwana akawapa huo ushindi.
Inawezekana kuna vitu ambavyo mwaka jana ulikuwa unaomba na havijatokea lakini moyoni mwako
una amani na utulivu maana yake hiyo ni dalili kuwa Mungu amekujibu kwa hiyo
fungua kinywa chako na anza kumsukuru Mungu kwa ushindi huo na atakupa huo
ushindi. Usisubiri hadi uone kwa nje bali kwa kuwa imani yako imeona basi anza
kumshukuru Mungu maana imani ni bayana ya mambo yasiyo onekana. Imani inaweza
kukupa kuona kitu ambacho macho hayawezi kuona.
FAIDA YA SITA
6. UKIAMUA KUSHUKURU WAKATI UNASHINDWA KUOMBA MUNGU
ANAKUFUNGULIA MLANGO WA KUSIFU NA KUOMBA.
Zaburi 100:1-5
1 Mfanyieni Bwana shangwe, dunia yote; 2 Mtumikieni Bwana
kwa furaha; Njoni mbele zake kwa kuimba; 3 Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu;
Ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake; Tu watu wake, na kondoo wa malisho
yake.4 Ingieni malangoni mwake kwa kushukuru; Nyuani mwake kwa kusifu;
Mshukuruni, lihimidini jina lake; 5 Kwa kuwa Bwana ndiye mwema; Rehema zake ni
za milele; Na uaminifu wake vizazi na vizazi.
Hapa nataka utazame sana mstari “.4 Ingieni malangoni
mwake kwa kushukuru; Nyuani mwake kwa kusifu; Mshukuruni, lihimidini jina
lake” ndani yako kama unasikia kuomba na
huwezi kuomba.
Sio kwamba huwezi kuomba ila ni hujisikii kuomba. Maana
unaweza kufunga kula na usiombe maana si kila aina ya kufunga kunakurudishia
maombi kifuani. Biblia inasema nikajitesa nafsi yangu kwa kufunga nafsi maombi
yangu yakarejea kifuani. Sio kufunga katika mwili bali ni katika nafsi maana
yake kuizuia nafsi katika vitu inavyoona. Maana yake Mungu anakubana
kukurejeshea maombi ndani yako.
Ukifunga kwa mwili ukaacha kula chapati mchana au
maharage na ugali jioni utajikuta
hujaweza kuomba. Kuna watu wengi sana wanafunga kula na hawaombi.Ikifika
jioni unaanza kujilaumu kuwa ulifunga nini sasa na haujaomba kwa hiyo umejitesa
bure hapa na umeshinda njaa na hujaweza omba.
Pia unahitaji kufahamu kuwa Mungu anaweza kukuletea
Zaburi ya 100:1-5,ina maana kuna kitu kingine anakupa. Ingieni malangoni mwaka
kwa kushukuru maana yake kuna mlango katika ulimwengu wa roho ambao umefungwa
na unatakiwa upite hapo.
Ndio maana kuna wakati ukiingia kuomba unaona Mungu kama
hakusikii ni kwa sababu mlango umefungwa. Lakini utakapoanza kushukuru milango
inafunguka kwa sababu biblia inasema ingieni malangoni mwake kwa kushukuru
maana kushukuru kunafungua mlango wa kupita.
Jifunze kushukuru kwa kila jambo, shukuru kuwa tu umepata
nafasi ya kumfikiria Mungu, Shukuru kwa kile Mungu kakupa saa hiyo, shukuru pia
kwa kupita kwenye matatizo. Kama unapita kwenye matatizo na Mungu anataka
kukufungulia mlango basi atakupa kushukuru. Ukianza kushukuru hakutakuja kuomba
bali kutakuja kumsifu Mungu ndani yako.
Unapoenda kanisani au kwenye semina kama hii. Ukikaa anza
kumshukuru Mungu kwa kukupa nafasi ya kuja ibada. Sasa ukianza kumshukuru Mungu
namna hiyo haijalishi umetoka nyumbani uko namna gani au umekasirika huko
moyoni, haijalishi uhusiano wako na Mungu ni mgumu kiasi gani lakini ukifika
kanisani na ukaanza kushukuru malango yanafunguka. Ghafla ndani yako utatoka wimbo wa kuanza kumsifu
Mungu unabaki kushangaa imetokeaje hiyo hali. Kumbe katika ulimwengu wa roho
uko wimbo na hapo waimbaji wa kanisani wameanzisha wimbo huo huo, na wewe
utashangaa kumbe uko katika ulimwengu wa roho na unadaka wimbo ule ule
wanaoimba waimbaji. Ikiwa namna hiyo sasa inakuwa rahisi sana kwako kuomba
lakini kilichokufungulia mlango ni kushukuru.
7. KUSHUKURU KWAKO KUNAMFANYA MUNGU AJULIKANE HASA
UNAPOMSHUKURU MBELE ZA WATU.
Zaburi 50:23a
Atoaye dhabihu za kushukuru, Ndiye anayenitukuza
Kutukuza maana yake ni kumfanya Mungu ajulikane,kutukuza
maana yake ni kujulisha. Unapotoa ushuhuda wako na shukrani zako mbele za watu
kuwa Mungu kakufanyia jambo fulani, unamfanya Mungu ajulikane katika hilo eneo,
juu ya uweza wake na nguvu alizonazo au katika hilo eneo ambalo umepata nafasi
ya kumshukuru Mungu mbele za watu.
0 Comments